Monday, November 18, 2019

KILIMANJARO QUEENS YATINGA KIBABE NUSU FAINALI CECAFA CHALLENGE,YAIZAMISHA 4-0 BURUNDI

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM MABINGWA watetezi, Tanzania Bara wamefanikiwa kuingia Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge Wanawake baada ya ushindi wa 4-0 dhidi ya Burundi jioni ya leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
 
  Kwa ushindi huo, Tanzania inafikisha pointi sita baada ya kushinda mechi zake mbili za mwanzo, nyingine wakiichapa Sudan Kusini 9-0 kuelekea mechi ya mwisho dhidi ya jirani zao, Zanzibar keshokutwa.
 
  Katika mchezo wa leo, mabao ya Kilimanjaro Qeens inayofundishwa na kocha Bakari Nyundo Shime yamefungwa na Deonisia Daniel Minja mawili dakika ya 35 na 65, Asha Rashid ‘Mwalala’ dakika ya 72 na Mwahamisi Omary ‘Gaucho’ dakika ya 86.
 
 
Kilimanjaro Queens wanaowania taji la tatu la mfululizo la michuano hiyo, wataingia kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya jirani zao Zanzibar wakihitaji kulinda heshima tu.
  Katika mchezo wa kwanza, Zanzibar walichapwa 5-0 na Sudan Kusini hapo hapo Azam Complez na sasa timu yoyote itakayoshinda vizuri mechi ya mwisho inaweza kuungana na Tanzania Bara katika Nusu Fainali.
  Michuano hiyo itaendelea kesho kwa mechi za Kundi B kati ya Kenya na Djibouti kuanzia Saa 8:00 mchana na Uganda na Ethiopia kuanzia Saa 10:30 jioni.
  Kikosi cha Tanzania Bara kilikuwa; Zubeda Mgunda, Julitha Aminiel, Happyness Hezron, Anastazia Anthony, Deonisia Minja, Stumai Abdallah/Fatuma Khatib ‘Foe’ dk75, Asha Saada, Asha Shaaban, Amina Ali/Janet Christopher dk85, Opa Sanga/Diana Lucas dk60 na Mwahamisi Omary ‘Gaucho’.
  Burundi; Jeanine Irakoze, Sandrine Niyonkuru, Gynette Kamwemwe, Angelique Keza, Zilfa Suzanne, Joelle Bukuru, Charlotte Irankunda, Asha Dfajari, Esther Nahimana, Aniella Umimana na Sakina Said.

No comments:

Post a Comment