![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/FC4A4795.jpg)
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adamu
Malima (kulia)akisalimiana na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi alipowasili Ofisi ya Mkuu huyo wa Mkoa
wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Mara.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/FC4A4806.jpg)
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adamu Malima
akimuelezea jambo Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt.
Eliezer Mbuki Feleshi walipokuwa wakifanya mazungumzo kwenye Ofisi ya
Mkuu huyo wa Mkoa .
Lydia Churi Ntambi
…………………………..
Na Lydia Churi- Mahakama, Musoma
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ameiomba Serikali mkoani Mara
kuwahamasisha wananchi kujitokeza kutoa ushahidi Mahakamani pale
wanapohitajika hatua itakayosaidia kesi kumalizika kwa wakati.
Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa
Mara Mhe. Adamu Malima, Jaji Kiongozi amesema hivi sasa kesi nyingi
hazimaliziki kwa wakati kutokana na wadau wa Mahakama kutokukamilisha
wajibu wao kwa wakati ikiwemo polisi kutokukamilisha upepelezi wa kesi
mapema pamoja na mashahidi kukosekana Mahakamani.
“Hakimu yupo, na ukiangalia jalada
utakuta kesi imeahirishwa mara nyingi kutokana na mashahidi kutofika
mahakamani”, alisema Jaji Kiongozi.
Alisema Mahakama kwa upande wake
itatoa ushirikiano mkubwa kwa wadau wake pamoja na Serikali ili wananchi
wapate haki kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mlundikano wa
kesi mahakamani unakwisha.
Aidha, Jaji Kiongozi pia amemuomba
Mkuu wa Mkoa wa Mara kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi ambao
hawaridhishwi na huduma zinazotolewa na Mahakama kutumia mifumo ya
Mahakama iliyopo ili kufikisha malalamiko yao.
Aliitaja mifumo hiyo kuwa ni
pamoja na Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama za Mikoa
zinazoongozwa na Wakuu wa Mikoa, Kamati za Maadili za Wilaya
zinazoongozwa na Wakuu wa Wilaya pamoja na Kamati ya Maadili ya
Majaji.
Jaji Kiongozi pia amemuomba Mkuu
huyo wa Mkoa kuwahimiza wakuu wa wilaya za Mkoa wa Mara kuzisimamia
kikamilifu Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama hasa kupitia Katibu
Tawala wa Mkoa (RAS) pamoja na Makatibu Tawala wa Wilaya (DAS).
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe.
Adamu Malima ameahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa Mahakama ya Tanzania
na kuahidi kuzisimamia kikamilifu Kamati za Maadili. Aliongeza kuwa yote
ya dola inalo jukumu la kuwatumikia wananchi na kuwapatia huduma zilizo
bora.
Akizungumza na Watumishi wa
Mahakama mkoani Mara wakati akihitimisha ziara yake, Jaji Kiongozi
amewataka watumishi hao kuikana rushwa na maadili yasiyofaa na badala
yake wawe na maadili mema ndani na hata nje ya Mahakama.
Amewapongeza watumishi
wasiojishirikisha na vitendo vya rushwa na kuwataka kuwa makini na
kujilinda wasije wakaingia kwenye vitendo hivyo ambavyo ni kinyume na
maadili ya utumishi.
Aidha, aliwataka watumishi wa
Mahakama kuwakanya na kuwarejesha kwenye mstari watumishi wenzao
wanaojishirikisha na vitendo vya rushwa na maadili yasiyofaa badala ya
kufurahia pindi wanapopata matatizo.
“Mahakama ni Taasisi kubwa hivyo
watumishi wake hawana budi kuwa na upendo kati yao na endapo mtu
anakosea aambiwe na kurekebishwa na siyo kusemwa pembeni, tulindane na
kupendana sisi kwa sisi”, alisema Jaji Kiongozi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania amemaliza siaza ya siku tano ya kikazi katika Mkoa wa Mara
ambapo alikagua shughuli za Mahakama katika wilaya za Bunda, Serengeti,
Tarime na Musoma Mjini. Jaji Kiongozi pia alikagua jengo jipya la
Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma lilimalizika hivi karibuni.
0 comments:
Post a Comment