*Ataka Watanzania wachangamkie soko la
nafaka nchi za SADC
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa ameiagiza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ifuatilie
kwa karibu miradi nane iliyowasilishwa na kuombewa fedha za ufadhili kupitia mkutano
wa saba wa TICAD uliofanyika Agosti 28-30, 2019 jijini Yokohama, Japan.
“Kupitia Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo
Kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7), Serikali
ya Japan imetenga kiasi cha dola za Marekani bilioni 20 kwa kipindi cha miaka
mitatu kwa ajili ya nchi za Afrika. Ninaielekeza Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki ishirikiane kwa karibu na Wizara zenye dhamana
kuratibu vema utekelezaji wa miradi nane ya maendeleo ambayo tayari
imewasilishwa kupitia TICAD 7,” amesema.
Waziri Mkuu
ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Septemba 13, 2019) katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa kuahirisha Mkutano wa 16 wa Bunge
jijini Dodoma. Bunge
limeahirishwa hadi Novemba 5, mwaka huu.
Amesema fedha hizo zimetengwa
ili kuziwezesha nchi za Afrika zitekeleze miradi ya kimkakati ya maendeleo
itakayoleta mageuzi ya kiuchumi. “Kiasi hicho kitatolewa ili kuendeleza miradi
mbalimbali katika sekta za elimu, afya, kilimo, maji, nishati, ujenzi wa maeneo
maalumu ya viwanda na miundombinu ya usafiri na usafirishaji.”
Amesema lengo la Serikali
ya awamu ya tano ni kuhakikisha Tanzania inanufaika na fedha hizo zilizotengwa
na Serikali ya Japan ili iweze kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda
ifikapo mwaka 2025.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka Watanzania watumie
fursa ya upungufu wa nafaka katika nchi za Kusini mwa Afrika kwa kuzalisha
zaidi mazao hayo ikiwa ni pamoja na kujiwekea akiba zaidi.
Amesema hali ya usalama wa chakula katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika
(SADC), imetetereka kutokana na athari mbalimbali ikiwemo ukame
katika upande wa magharibi wa ukanda, mvua zilizokithiri, mafuriko na vimbunga
vya IDAI na Kenneth pamoja na wadudu waharibifu wa mazao na magonjwa.
Waziri Mkuu amesema kuwa Agosti 29-30, mwaka huu, Wizara
ya Kilimo iliratibu mkutano na wadau mbalimbali wenye kujihusisha na uzalishaji
na biashara ya nafaka ili kujadili fursa zilizopo katika mazao ya nafaka,
changamoto wanazokabiliana nazo na kutafuta utatuzi wake.
“Ninaigiza Wizara husika ihakikishe inashirikiana na
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili kutumia vema
fursa ya uwepo wa masoko ya nafaka kwenye ukanda huu wa SADC na hivyo, kukidhi
mahitaji katika ukanda sambamba na kuboresha biashara na maisha ya wananchi wa
vijijini,” amesema.
Pia ameitaka wizara hiyo iendelee kuhamasisha uzalishaji
wa mazao hayo kwa wingi ili nchi iweze kujitosheleza kwa chakula na kuwa na
ziada.
0 comments:
Post a Comment