Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Katikati) akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe Job Daud Masima (Kulia) katika Ofisi za Ubalozi huo zilizopo katika mtaa wa 12, Abba Hillel Silver Jijini Tel Aviv nchini Israel. Mwingine ni Mwambata Jeshi Brigedia Jenerali Kahema Juni Mziray, Leo Tarehe 3 Septemba 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Kulia) akizungumza na Mkuu wa Mradi wa Umwagiji Afrika kampuni ya Netafim Ndg Shay Haxter mara baada ya kutembelea katika shamba la utafiti wa kilimo wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku sita nchini Israel. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe Job Daud Masima Leo Tarehe 3 Septemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa Tanzania walioshiriki mafunzo ya Kilimo nchini Israel kwenye shamba la mifugo la Jacob's Farm, Mwingine pichani ni Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe Job Daud Masima (Kulia), Leo Tarehe 3 Septemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kutembelea Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Israel zilizopo katika mtaa wa 12, Abba Hillel Silver Jijini Telaviv nchini Israel, Leo Tarehe 3 Septemba 2019.
Na Mathias Canal,
Telaviv-Israel
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema kuwa
serikali YA Tanzania imejipanga kuikabili sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na
kuona umuhimu wa kuwaandaa watanzania katika kubadilisha kilimo chao kutoka
kwenye kilimo cha kujikimu na kuwa kilimo cha kibiashara.
Waziri Hasunga ameyasema hayo leo tarehe 3 Septemba
2019 wakati akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe Job Daud Masima
katika Ofisi za Ubalozi huo zilizopo katika mtaa wa 12, Abba Hillel Silver
Jijini Tel Aviv nchini Israel.
Alisema kuwa katika ziara yake hiyo amejifunza namna
ambavyo nchi ya Israel imepiga hatua ya ujuzi katika sekta ya kilimo hivyo
kuona umuhimu wa serikali ya Tanzania kuwekeza katika skimu za umwagiliaji.
Alisema kuwa asilimia kubwa ya wakulima nchini
Tanzania wanatumia majembe ya mkono katika kilimo jambo ambalo haliwezi kuongeza
tija na uzalishaji. “Tunatumia majembe ya mkono mbaya zaidi kilimo chetu
kinategemea msimu wa mvua, hivyo kilimo cha namna hiyo bado kinatuchelewesha,
tuna wajibu wa kujifunza kwa wenzetu walioendelea” Alisema Mhe Hasunga
Alisema kwa kuanza serikali ya Tanzania kwa
kushirikiana na wadau wa kilimo inaweza kujenga mabwawa kwa ajili ya kilimo cha
umwagiliaji ili kuongeza uwezo wa kilimo cha umwagiliaji kitakachofanya kazi msimu
mzima badala ya kilimo cha kutegemea mvua.
Mhe Hasunga alisema kuwa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana
na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kadhalika wizara ya Viwanda na Biashara zitafanya
kazi kwa pamoja ili kuona namna ya kuzalisha kwa tija mazao ya kilimo na kutoa
malighafi nyingi zitakazochangia katika kuinua na kuchagiza matakwa ya serikali
ya kuwa na serikali ya viwanda.
Kuhusu masoko ya mazao yanayozalishwa nchini Tanzania
Mhe Hasunga alisema kuwa serikali inaendelea na mkakati maalumu wa kuimarisha
masoko kwani imeanzisha kitengo maalumu katika wizara ya kilimo kitakachokuwa
na wajibu wa kushughulikia masoko ya mazao ya wakulima.
Katika hatua nyingine Waziri Hasunga ameyaalika
makampuni mbalimbali ya Israel yanayojishughulisha na kilimo kutembelea nchini
Tanzania kwa ajili ya kujionea fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania.
“Tanzania ni nchi yenye rutuba nzuri, eneo kubwa kwa
ajili ya uwekezaji wa kilimo, hivyo nayaalika makampuni yote yanayohusika na
kilimo hususani yanayojishughulisha na utafiti, kutembelea Tanzania kwani ni
nchi yenye eneo zuri na kubwa kwa ajili ya uwekezaji hususani katika sekta ya
kiliumo” Alikaririwa Mhe Hasunga
Mhe Hasunga amesema kuwa Israel ni nchi yenye eneo
dogo kwa ajili ya kilimo lakini wanazalisha chakula kinachotosheleza wananchi
wake sambamba na kuuza mazao yao nje ya nchi jambo ambalo linaimarisha pato la
serikali ya nchi hiyo na kipato cha mtu mmoja mmoja.
Vilevile, waziri Hasunga ameupongeza Ubalozi wa
Tanzania nchini Israel unaoongozwa na Mhe Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe
Job Daud Masima na watendaji wengine wote kwa kazi nzuri wanayoifanya ya
uwakilishi wa Tanzania, Aidha Mhe Hasunga amemuomba Balozi huyo kutafuta fursa
zaidi za makampuni ya kilimo na viwanda kwa ajili ya kuwekeza nchini Tanzania.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe
Job Daud Masima amesema kuwa miongoni mwa mambo muhimu ya kuyafanyia kazi ni
pamoja na kutafuta namna ya kuongeza idadi ya vijana wanaoshiriki katika
mafunzo ya kilimo ya Agro Studies ili izidi kuongezeka maradufu.
Kadhalika, alisema kuwa ofisi yake inaendelea kufanya
kazi kubwa kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini Tanzania kwani idadi
kubwa ya watalii inaongeza pato la kigeni la nchi.
Balozi Masima alisema kuwa nchi ya Israel ina
mafanikio makubwa kwenye sekta ya teknolojia hivyo ni wajibu wa Tanzania
kutumia fursa hiyo muhimu katika elimu ya ujuzi wa teknolojia za kilimo
hususani umwagiliaji.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment