Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akiwa na mgeni wake Rais wa Uganda Mheshimiwa Yoweri Museveni kabla ya
kuanza mazungumzo yao Chato mkoani Geita mapema Julai 2019. PICHA NA
IKULU.
Na Mwandishi Wetu.
MTANZANIA mwenzangu, najua
unajua kuwa siku za karibuni nchi za Tanzania na Uganda zinatarajia
kufanya Kongamano la kibiashara la pamoja ambalo litakuwa ni mara ya
kwanza kufanyika nchini kwetu.
Kwa kukumbusha tu, kongamano
hilo linatarajia kufanyika kuanzia Septemba 6 hadi Septemba 7 mwaka huu
katika ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo baina ya Tanzania na Uganda linatarajia kuwashirikisha wafanyabiashara wa nchi hizo.
Kongamano hilo kwa namna moja au
nyingine itakuwa fursa nzuri kwa wafanyabiashara wa nchi hizo
kubadilisha uzoefu wa kibiashara na namna nzuri ya kuendelea
kushirikiana kwa maslahi ya pande zote mbili.
Serikali ya Awamu ya Tano chini
ya utawala wa Rais mzalendo na mwenye upendo kwa nchi Dkt. John Pombe
Magufuli pamoja na mambo mengine ameweka msingi imara katika kuhakikisha
bidhaa zinazozalishwa nchini zinapata soko kwenye nchi nyingine
zikiwemo za Afrika Mashariki.
Kauli mbiu ya Tanzania ya
viwanda ambayo imekuwa ikihimizwa na Rais wetu imekuwa chachu kwa
Watanzania kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa viwanda sambamba na
utengenezaji wa bidhaa zenye ubora ambazo zinaweza kushindana kwenye
soko la Dunia, Afrika na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Kabla ya kuendelea kuzungumzia
umuhimu wa kongamano hilo la kibiashara kati ya Tanzania na Uganda
naomba kutumia walau dakika moja ama mbili kutoa pongezi zangu za dhati
kwa Rais Dk. Magufuli kwa namna ambavyo ameamua kufungua milango ya
kuzikaribisha nchi mbalimbali kuja nchi kuwekeza.
Kwa upendo mkubwa kwa nchi yake,
amehakikisha anaweka mkazo katika ujenzi wa miundombinu ya uwekezaji na
kibiashara na matokeo yake muamko kwa watanzania katika kuwekeza na
kufanyabishara umekuwa mkubwa na wenye tija. Hongera Rais wetu kwa kazi
nzuri ambayo unaifanya kwa maendeleo ya nchi yetu.
Hata hivyo kupitia kongamano la
biashara ambalo linahusisha nchi hizo mbili, ni wazi Tanzania itatumia
nafasi hiyo kama fursa ya kutangaza bidhaa zake na wakati huo huo Uganda
nayo itaonesha bidhaa zake.
Ni kongamano ambalo kwangu
naliona limekuja wakati muafaka hasa kwa kuzingatia chini ya Rais
Magufuli nchi yetu imekuwa na mazingira mazuri ya kibiashara. Ni wakati
muafaka kwa nchi zote mbili kutumia maonesho hayo kujengeana ujuzi
katika utengenezaji wa bidhaa bora na utafutaji masoko.
Pamoja na mambo mengine kupitia
kongamano hilo la kibiashara itakuwa sehemu sahihi ya kuweka mbinu na
mikakati itakayofanikisha kuongeza thamani kwa bidhaa zinazotokana na
mazao.Sina shaka na hilo hata kidogo na ukweli kwa Tanzania imedhamiria
kuongeza thamani kwa bidhaa za mazao.
Katika maisha ya kawaida najua
unaweza kujiuliza hivi , je Tanzania tunauza nini zaidi kwa nchi ya
Uganda? Jibu vyovyote lakini hili ambalo nitakueleza ni muhimu
zaidi. Iko hivi mpaka sasa Tanzania inauza bidhaa za mazao na bidhaa za viwandani nchini Uganda.
Takwimu zilizopo zinaonesha kwa
kipindi cha miaka miwili iliyopita Tanzania imeweza kuuza bidhaa za
mazao ya chakula na viwandani zenye thamani ya Sh. bilioni 300 kutoka
Sh. bilioni 100. Hilo ni ongezeko mara mbili zaidi ya fedha
zilizopatikana huko nyuma.
Ninaposema Rais Magufuli ameweka
mazingira mazuri ya kibiashara naaminisha na takwimu zinaeleza wazi
namna ambavyo nchi yetu ilivyoweka mazingira mazuri katika sekta ya
biashara na viwanda.
Nikiri kwa namna ambavyo
Tanzania unauza bidhaa zake nchini Uganda na kuingiza kiasi hicho cha
fedha, kongamano litakalofanyika nchini litaongeza wigo zaidi wa
kibiashara.
Hata hivyo kutokana na umuhimu
wa kongamano hilo la kibiashara, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya
Viwanda na Biashara imejipanga vema kuhakikisha kongamano hilo linakuwa
na tija na ushiriki wa Watanzania unakuwa mkubwa zaidi.
Nakumbuka wakati anazungumzia
kongamano hilo Waziri wa Viwanda na Biashara Waziri wa Viwanda na
Biashara Innocent Bashungwa amesema kongamano hilo litasaidia kuweka
mazingira wezeshi ya kuongeza wigo wa kujenga viwanda zaidi nchini hasa
vya usindikaji wa mazao ili kuongeza thamani ya mazao hayo.
Naomba nitoe rai kwa
wafanyabishara na wawekezaji na wote wanaojihusisha na sekta ya biashara
waliopo nchini Tanzania kuhakikisha wanashiriki kikamilifu na kwa
vitendo katika kongamano hilo. Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais
Magufuli imejikita katika msingi wa kufanya kazi kwa bidiii.
Hivyo kwa wafanyabiashara
kupitia kongamano hilo wataendelea kunoa vichwa ili kujiimarisha zaidi
kibiashara ana kiuwekezaji kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake kwa
ujumla. Nihitimishe kwa kukumbusha tena kongamano la kibiashara kati ya
Tanzania na Uganda litafanyika Septemba 6 na Septemba 7 mwaka huu. Sote
tushiriki bila kukosa.
0 comments:
Post a Comment