
Mthamini
Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha akiangalia moja ya nyumba iliyofanyiwa
uthamini kwa ajili ya kulipwa fidia katika kijiji cha Matongo wilaya ya
Tarime mkoa wa Mara kupisha upanuzi wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara
kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la taka sumu jana. Kulia ni Mthamini kutoka
wilaya ya Serengeti Bariki Ileta.

Mthamini
Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha (Nyuma) akiwa na wataalamu wa Uthamini
kutoka Serengeti Bariki Ileta (Mbele) na Bisare Charles kutoka Tarime
wakati wa zoezi la Uthamini linaloendelea katika kijiji cha Matongo
wilaya ya Tarime mkoa wa Mara ili kulipwa fidia kupisha upanuzi wa Mgodi
wa Dhahabu wa North Mara kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la taka sumu jana.

Mthamini
Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha (kushoto) akitoa maelekezo kwa
wataalamu wa Uthamini wakati wa zoezi la Uthamini katika kijiji cha
Matongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara ili kulipwa fidia kupisha upanuzi
wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la taka
sumu jana.

Mkazi
wa kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara Marwa Mangora Mube
akiwaoongoza wataalamu wa Uthamini kukagua eneo lake kwa ajili ya
kufanyiwa tathmini ili kulipwa fidia kupisha upanuzi wa Mgodi wa Dhahabu
wa North Mara kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la taka sumu jana.

Wataalamu wa Upimaji kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakiandaa vifaa tayari kwa upimaji wakati wa zoezi uthamini katika kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara ili kulipa fidia kwa wananchi kupisha upanuzi wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la taka sumu jana. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
************************************
Na Munir Shemweta, WANMM NYAMONGO
Serikali
imeanza kusikiliza kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Nyamongo katika
wilaya ya Tarime mkoani Mara kwa kuanza kufanya tathmini ya fidia ya
kutwaa eneo la ardhi kwa ajili ya kupanua Mgodi wa Dhahabu wa ACACIA
North Mara ili kujenga Bwawa la Maji Taka.
Tayari
timu ya wataalamu 25 kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi inayojumisha Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali pamoja na idara
ya Upimaji na Ramani iko eneo la Nyamongo kijiji cha Matongo wilaya ya
Tarime mkoani Mara kutathmini mali za wananchi ili kulipwa fidia na
kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Maji Taka.
Akizungumza
wakati wa zoezi hilo jana katika kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime
mkoa wa Mara Mthamini Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha alisema, zoezi la
uthamini linalofanyika ni kwa ajili ya kutwaa eneo la ujenzi wa Bwawa
la Maji Taka katika eneo la Nyamongo lenye ukubwa wa hekta 237 ambalo
linahusisha vitongoji vitatu vya Kigonga A, Kwinyunywi na Kigonga B
ambapo uthamini wake ulishaanza toka mwezi julai mwaka huu.
Mugasha
alisema, uthamini huo unaangalia mali inayohamishika na ile
isiyohamishika na kufuata sheria ya ardhi na ile ya kijiji na kusisitiza
uthamini huo umekuwa ukifanyika kwa uwazi na hauna lengo la kumnufaisha
au kumpunja mtu yeyote.
‘’
Eneo la Nyamongo tunalichukulia kama eneo la mfano hasa baada ya
kufanyika tathmni maeneo mbalimbali ya mgodi miaka ya nyuma na kubaini
udanganyifu wa baadhi ya wananchi na Wathamni wasiowaaminifu kutumia
zoezi kama hili kujinufaisha’’ alisema Mugasha.
Kwa
mujibu wa Mthamini Mkuu wa Serikali, udanganyifu wowote utakaofanyika
kwa nia ya mmiliki wa nyumba ama eneo kujinufaisha Ofisi yake
haitamvumilia kwa kuwa baada ya uthamini wanafanya uhakiki kujiridhisha
usahihi wa taarifa na mali za wananchi.
Mthamini
kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu Lazaro Mayumba anayeshiriki
zoezi hilo alisema, zoezi hilo linafanyika kwa kasi kwa kuwa serikali
ina jukumu la kulinda mali na afya za wananchi waliokuwa wakilalamikia
kwa muda mrefu kuhusu kutiririka maji yenye sumu katika Mgodi wa Dhahabu
wa ACACIA North Mara.
Alieleza
kuwa, katika kuhakikisha wananchi wanaozunguka mgodi huo hawaathiriki
na wakati huo mgodi haufungwi kutokana na madhara yanayopatikana dhidi
ya taka sumu, serikali iliona iko haja kutwaa eneo litakalosaidia mgodi
kupata eneo kwa ajili ya ujenzi bwawa kubwa na lenye ubora ambalo
halitaleta madhara yanayodaiwa na wananchi.
”Mbali
na madai ya wananchi wanaozunguka mgodi wa North Mara lakini pia athari
za taka sumu zinaweza kufika mto Mara ambao uko umbali wa takriban
kilometa tatu kutoka katika Mgodi na kama hatua za haraka
hazitachukuliwa unaweza kuharibu uoto wa asili pamoja na mbuga za
wanyama”’ alisema Mayumba.
Baadhi
ya wananchi wa kijiji cha Matongo linakofanyika zoezi la Uthamini
wameonesha kufurahishwa na hatua ya serikali kuamua kutafuta eneo kwa
ajili ya ujenzi wa Bwawa jipya la taka sumu za Mgodi wa Dhahabu wa North
Mara kwa madai kuwa wamekuwa wakiathirika sana na maji yanayotiririka
katika mgodi huo.
Gaga
Sita Kishashila mmoja wa wakazi wa kijiji cha Matonga alisema pamoja na
zoezi la uthamini linaloendelea sasa lakini shauku kubwa ya wakazi hao
ni kutaka kujua wanalipwa lini ili waweze kuondoka maeneo hayo mapema na
hofu yao ni kukwama kwa zoezi hilo kama ilivyotokea huko nyuma.
Mkazi
mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Simion Kirario aliomba uthamini
unaofanyika kuangalia na hali za wananchi hao kwa kuwa baadhi yao wana
hofu ya kulipwa kiasi kidogo kutokana na aina ya nyumba wanazomiliki za
Msonge huku wakihitaji kuwa na fedha nzuri itakayowawezesha kununua eneo
lingine na kufanya maendelezo.
Mwenyekiti
wa Kitongoni cha Kigonga A Kibwabwa Mwita Kibwabwa alisema kazi ya
uthamni katika kitongoji chake imeenda vizuri kwa kuwa zoezi hilo
linafanyika kwa kasi na wananchi wake wanataka kujua wanalipwa lini.
Hata hivyo alisema baadhi ya wananchi wamelalamikia kiasi watakacholipwa
na kukiona kidogo ukilinganisha na matarajio yao.
Kwa
muda mrefu wananchi wa Nyamongo wilaya ya Tarime mkoa wa mara hasa wale
wanaoishi vitongoji vinavozunguka Mgodi wa Dhahabu wa ACACIA North Mara
wamekuwa wakilalamikia uchafuzi wa mazingira hasa maji yanayovuja kutoka
Mgodi huo kuwa yana sumu inayoathiri afya zao jambo lililomlazimu Rais
John Pombe Magufuli wakati wa ziara yake katika eneo hilo kuagiza
kufanyika utafiti ili kubaini ukweli huo.
0 comments:
Post a Comment