
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema ahadi zote zilizotolewa na Rais Dkt. John Magufuli ikiwemo
ujenzi wa barabara ya Mikumi-Ifakara kwa kiwango cha lami zitatekelezwa,
hivyo amewataka wananchi waendelee kuiamini Serikali yao.
Ametoa kauli hiyo jana
(Jumanne, Septemba 17, 2019) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na
wananchi wa Mji wa Ifakara pamoja na wilaya ya Kilosa alipokuwa katika
siku ya nne ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.
“Kila alichokiahidi Mheshimiwa
Rais Dkt. John Magufuli nitakisimamia kuhakikisha kinatekelezwa, hivyo
wananchi endeleeni kuiamini Serikali yenu. Serikali yenu ipo makini na
ina dhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo kama Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ya 2015-2020 inavyoelekeza.”
Waziri Mkuu alisema Serikali ya
Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli iko makini na
inaendelea kuchapa kazi kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabili
wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini yakiwemo na mkoa wa Morogoro.
Pia, Waziri Mkuu alisema kila
mtumishi wa umma anatakiwa ahakikishe anafanya kazi kwa bidii ili
kuiwezesha Serikali kutimiza lengo lake la kuboresha maendeleo ya
wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini hususani ya vijijini.
Waziri Mkuu alisema iwapo
watumishi wa umma watatimiza majukumu yao ipasavyo changamoto nyingi
zinazowakabili wananchi kama upatikanaji wa maji zitakuwa historia kwa
kuwa Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
hiyo.
Alisema watumishi wa umma
wanapaswa kuwa na nidhamu ya fedha za Serikali zinazopelekwa katika
maeneo kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo ikiwemo ya afya,
elimu na maji. “ Sina mzaha na watakaotafuna fedha hizo.”
0 comments:
Post a Comment