Na Josephine Majura na Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali imeeleza kuwa Sheria ya
Huduma Ndogo za fedha ya mwaka 2018 haina lengo la kuinyima jamii fursa
ya kusaidiana kwa njia ya kukopeshana bali inalenga kutatua changamoto
zilizopo ikiwemo ya utozaji wa riba kubwa.
Hayo yamesemwa Bungeni Jijini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji,
wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti maalum, Mhe. Lucy
Magereli, aliyetaka kujua Sheria ya udhibiti wa taasisi ndogo za fedha
imetekelezwa kwa kiasi gani na Serikali haioni Sheria hiyo inainyima
jamii kusaidiana.
Dkt. Kijaji alisema kuwa kutokana
na changamoto za Sekta ndogo ya Fedha ikiwemo kutoza kiwango kikubwa cha
riba na ukosefu wa utaratibu wa kuwalinda walaji na wadau kwa ujumla,
Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 itaimarisha usimamizi na
udhibiti wa sekta hiyo.
“Udhibiti wa sekta ndogo ya fedha
unaakisi matarajio na mahitaji ya wadau na hivyo kuongeza kasi ya ukuaji
na mchango wake katika sekta nzima ya fedha na uchumi kwa ujumla”,
alieleza Dkt. Kijaji.
Alisema kuwa walengwa wa Sheria
hiyo wamepewa mwaka mmoja wa mpito baada ya kanuni kutolewa ili waweze
kujiandaa kulinganana matakwa ya kanuni hizo ambazo zitaanza kutumika
rasmi baada ya kipindi hicho kupita.
Dkt. Kijaji alisema kuwa hadi sasa hakuna taasisi yoyote iliyosajiliwa kupitia Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018.
Alifafanua kuwa, baada ya Sheria
hiyo kutungwa, Serikali ilianza mchakato wa kuandaa kanuni za huduma
hiyo zilizolenga madaraja manne ya watoa huduma yaliyoainishwa kwenye
Sheria.
Mchakato huo ulihusisha ukusanyaji
wa taarifa mbalimbali za walengwa ili kuweza kutengeneza kanuni
zilizozingatia hali halisi ya biashara zao pamoja na matakwa ya Sheria.
Aidha mchakato wa kuandaa kanuni ulikamilika na hivyo kutangazwa kwenye
gazeti la Serikali namba 575 Agosti 2, 2019.
0 comments:
Post a Comment