Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringi Macha, ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na uongozi mzima wa serikali kwa kuhakikisha amani na kudhibiti vurugu zilizojitokeza mara baada ya uchaguzi.
Akizungumza mara baada ya kutembelea mabanda ya maonesho ya Mat Builders & Contractors, Mhe. Macha amewataka wananchi wa Simiyu na watanzania kwa ujumla kuendeleza utamaduni wa kulinda amani—nguzo muhimu inayowezesha utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Akiwashukuru waandaaji na washiriki wa maonesho hayo, Mkuu wa Mkoa amesema amefanikiwa kutembelea mabanda yote na kujionea ubunifu, teknolojia na kazi kubwa zinazofanywa na makampuni na taasisi mbalimbali.
“Nilipopata habari za maonesho haya niliona kuna fursa, na kama mtendaji mkuu wa mkoa sikuwa tayari kuikosa. Nimetembelea mabanda yote na nimebeba mambo mengi ya kwenda kuyafanyia kazi Simiyu,”alisema.
Amesema maonesho hayo yamedhihirisha kuwepo kwa teknolojia na ubunifu ambao unaweza kuongeza tija katika sekta za kilimo, ufugaji, ujenzi na viwanda—sekta muhimu kwa uchumi wa mkoa wa Simiyu.
Mhe. Macha alibainisha kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia, Mkoa wa Simiyu umepiga hatua kubwa, ukiwemo ujenzi wa barabara za lami zinazoziunganisha wilaya na mikoa jirani kama Mara, Mwanza na Shinyanga.
Akitaja baadhi ya miradi mikubwa, amesema mkoa unaendelea kunufaika na mradi wa maji wa shilingi bilioni 400 kutoka Ziwa Victoria unaohudumia wilaya za Busega, Bariadi, Ntilima hadi Maswa, ukitarajiwa kumaliza kabisa changamoto ya maji.
Aidha, mkoa upo katika hatua za mwisho kupata kituo kikubwa cha kupoozea umeme, hatua inayotarajiwa kuimarisha zaidi upatikanaji wa nishati katika maeneo yote, ikiwa ni pamoja na vijiji.
“Ukiona eneo lina huduma zote za uhakika, basi jua hapo pana fursa za kiuchumi. Simiyu tunazipata huduma hizo, na uchumi wetu unazidi kukua,” alisema.
Mkoa wa Simiyu umeendelea kuwa kitovu cha kilimo cha mazao muhimu kama mpunga, dengu, choroko na hasa pamba, ambayo inalimiwa kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko mikoa mingine nchini. Pia, viwanda vingi vya kuchakata pamba vimejengwa mkoani humo, hatua inayoongeza thamani ya zao hilo.
Katika sekta ya ufugaji, Simiyu ina mifugo mingi ikiwemo ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku, hivyo teknolojia na mafunzo yanayotokana na maonesho kama hayo yanatazamwa kuwa kichocheo cha kuongeza tija kwa wafugaji na wakulima.
Mhe. Macha amesisitiza kuwa mafanikio yote yanayoonekana nchini hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa amani, akiwataka wananchi kutunza umoja na kutokurudia makosa ya nyuma.
“Kwa kweli haya tunayoona yasingewezekana bila amani. Tuishukuru serikali yetu, tuwashukuru viongozi wetu wakiongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kurejesha utulivu baada ya vurugu zilizojitokeza. Naomba wananchi wetu tujue yaliyoisha hatupendi yarudi tena.”
Mkuu huyo wa mkoa alisisitiza kuwa anaamini maonesho ya Mat Builders & Contractors yakiletwa Simiyu yataongeza fursa mpya kwa wakulima, wafugaji na wawekezaji kutokana na teknolojia na huduma walizoziona.








0 comments:
Post a Comment