
*Yawataka wadau wajiepusha na vitendo vya rushwa, uvunjifu wa amani
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka wadau watakaoshiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa
wahakikishe wanajiepusha na vitendo vya rushwa na uvunjifu wa amani
kwani Serikali haitasita kuchukua hatua pale itakapothibitika vitendo
hivyo kufanyika.
Waziri Mkuu amesema wadau hao
mbalimbali kutoka katika Vyama vya Siasa, Taasisi za Serikali na Zisizo
za Serikali na wananchi ni vema wakahakikisha wanasoma na kuelewa
kanuni na miongozo ya uchaguzi huo ili waweze kushiriki ipasavyo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo
leo (Ijumaa, Septemba 13, 2019) , wakati akiahirisha mkutano wa 16 wa
Bunge la 11, Bungeni jijini Dodoma. Waziri Mkuu amewataka Watanzania
wote wenye sifa washiriki uchaguzi huo kwani ni haki yao ya msingi.
“Natoa wito kwa Watanzania
wote wenye sifa wajiandikishe katika orodha ya wapiga kura, wachukue
fomu za kugombea nafasi mbalimbali na kushiriki kupiga kura kwani hiyo
ni haki yao ya kikatiba kwa kuzingatia misingi ya demokrasia.”
Mbali na wadau hao, pia,
Waziri Mkuu amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama vishiriki kikamilifu
katika kuhakikisha wananchi wanafanya uchaguzi kwenye mazingira ya amani
na utulivu bila kubugudhiwa.
Waziri Mkuu amewataka
Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa uchaguzi huo wahakikishe
wanazielewa kanuni na miongozo ilitoyotolewa ili waweze kutoa tafsiri
sahihi wakati wa kusimamia uchaguzi huo.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amewahimiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya waratibu vizuri shughuli za
uchaguzi kwenye maeneo yao na wahakikishe uwepo wa ulinzi na usalama
wakati wote wa uchaguzi hasa kipindi cha kampeni na wakati wa kupiga
kura.
Waziri Mkuu amewasihi wabunge
na madiwani wawahamasishe wananchi ili watumie haki yao ya kidemokrasia
ya kuchagua na kuchaguliwa. “Natoa rai kwenu mhakikishe mnashiriki
kikamilifu katika shughuli zote za uchaguzi huo.”
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
unatarajiwa kufanyika tarehe 24 Novemba 2019. Uchaguzi huo unafanyika
kila baada ya miaka mitano kwa lengo la kukidhi matakwa ya Ibara ya 8 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, inayoelekeza
kuwa Mamlaka na Madaraka ya Serikali yanatokana na wananchi.
Kuhusu uboreshaji wa daftari
la wapiga kura, Waziri Mkuu amesema tarehe 18 Julai 2019 Serikali
ilizindua zoezi hilo mkoani Kilimanjaro na kuongeza kuwa uboreshaji
huo, unahusisha wapiga kura waliotimiza umri wa miaka 18 na wale
watakaotimiza umri huo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.
“Makundi mengine
yatakayohusika ni wapiga kura waliohamia katika kata au jimbo jingine la
uchaguzi, waliopoteza kadi au kuharibika, wanaohitaji kurekebisha
taarifa zao; mfano majina ambayo hapo awali yalikuwa yamekosewa pamoja
na kuwaondoa wapiga kura waliopoteza sifa kama vile kufariki dunia.”
Amesema kwa sasa zoezi hilo
tayari limekamilika katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara,
Simiyu, Mara na Mwanza (isipokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba).
Zoezi hilo linaendelea kutekelezwa chini ya kaulimbiu isemayo Kadi Yako,
Kura Yako, Nenda Kajiandikishe.
0 comments:
Post a Comment