METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, December 7, 2025

BMH YASOGEZA HUDUMA ZA AFYA KARIBU NA WANANCHI, YAHAMASISHA UCHANGIAJI DAMU, MSALATO MNADANI - KATIKA KUADHIMISHA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA.

 

Na Meleka Kulwa- Dodoma 

Desemba 6, 2025 Jijini Dodoma 

‎Hospitali ya Benjamin Mkapa imepeleka huduma za afya katika Viwanja vya Mnadani Msalato jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia na Ukatili dhidi ya Watoto yanayoadhimishwa kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10 kila mwaka, kwa lengo la kuwafikia wananchi wasiopata kwa urahisi huduma za afya.

‎Akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala, Bw. Teophory Mbilinyi, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi, amewahimiza wananchi wa Msalato na Watanzania wenye changamoto za kiafya kufika hospitalini  kwa matibabu ya kina ya huduma za kibingwa, akisisitiza kuwa kwa pamoja watajenga taifa.

‎Awali akizungumza, Mkurugenzi wa Wauguzi, Bi. Mwanaidi Makao; aliwasisitiza wananchi kufika katika banda hilo ili kujipatia huduma mbalimbali zinazopatikana hapo, na aliahidi timu ya BMH itarudi katika awamu zingine katika kutoa elimu na huduma katika eneo hilo.

‎Pia kabla ya hapo, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Ubunifu na Mratibu wa Huduma za Masuala ya Ukatili wa Kijinsia na Ukatili dhidi ya Watoto, Bi. Hindu Ibrahim, amesema kuwa timu ya madaktari, na wataalamu wengine imefika Msalato Mnadani kutoa huduma za moja kwa moja kwa wananchi, hawakufika kwa ajili ya kutoa elimu pekee bali pia kutoa huduma za vitendo ikiwemo upimaji wa afya, uchangiaji damu na huduma za afya ya akili.

‎Bi. Hindu amesema kuwa Msalato Mnadani ni eneo lenye mkusanyiko mkubwa wa watu wanaofika kwa shughuli mwisho wa wiki; baadhi hukosa muda wa kufika hospitalini. Kusogeza huduma katika eneo hilo kumewezesha kuwafikia wananchi ambao hawajapima afya kwa muda mrefu.

‎Baadhi ya wananchi waliotembelea banda hilo, akiwemo Ratifa Abdalah mkazi wa Miyuji, amesema kuwa Watanzania wanapaswa kujitokeza kwa wingi kuchangia damu ili uokoa maisha ya watanzania Wenye matatizo na uhitaji wa damu. Aidha, amesema kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa inatoa huduma bora.

‎Kwa upande wake, Bi.Sauda Omary mkazi wa Msalato amesema kuwa  wananchi wanapaswa kupima afya na kujua hali zao. Akibainisha kuwa huduma zilizofikishwa Msalato ni msaada mkubwa kwa kuwa zimewasogezea huduma wananchi waliokuwa wakipata ugumu wa kufika hospitalini. aidha, Aliishukuru Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kuendelea kusogeza huduma karibu na jamii.










Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com