

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akitoa taarifa kuhusu uamuzi wa Serikali wa kuridhia misitu ya hifadhi
iliyopoteza sifa itolewe kwa mwananchi kwa ajili ya shughuli za Kilimo
na Mifugo ili kuwandolea kero za uhaba wa ardhi. Kauli hiyo aliitoa
kwenye ukumbi wa Waziri Mkuu, jijini Dar es salaam, Septemba 23,
2019.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………..
*Ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli la Januari 2019
*Maeneo yote kutolewa kwa wananchi, vijiji 920 kubaki ndani ya hifadhi
Serikali imeridhia kufuta mapori
tengefu 12 yenye ukubwa wa ekari 707,659.94 ambayo yamepoteza sifa na
imeamua yagawiwe kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za makazi, kilimo na
mifugo.
Uamuzi huo umefikiwa leo
(Jumatatu, Septemba 23, 2019) kweye kikao cha Baraza la Mawaziri
kilichoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Dkt. John
Joseph Pombe Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akitoa taarifa mara baada ya kikao
hicho, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Mawaziri wa kisekta
wakiongozwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw.
William Lukuvi walichambua na kuandaa taarifa ya mapendekezo ya utatuzi
wa migogoro ya matumizi ya ardhi nchini iliyowasilishwa katika kikao cha
Baraza la Mawaziri cha leo.
“Mawaziri walichambua na kubaini
kuwa vijiji vyenye migogoro ni 975 na siyo 366 kama ilivyotangazwa
awali, Baraza limeamua kwamba vijiji 920 vitabaki ndani ya hifadhi,
mipaka irejewe upya, vipatiwe vyeti vya ardhi vya kijiji pamoja na
kupangiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi,” amesema na kuongeza kuwa
orodha ya vijiji hivyo itatangazwa baadaye.
Waziri Mkuu amesema Serikali
imeridhia Misitu ya Hifadhi saba yenye ukubwa wa ekari 46,715
iliyopoteza sifa itolewe kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za makazi,
kilimo na mifugo ili kuwaondolea kero za uhaba wa ardhi.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema
Serikali imeridhia kumega hifadhi za misitu 14 kwa ajili ya kilimo na
mifugo na kufuta mashamba 16 yasiyoendelezwa ili yapangiwe matumizi ya
kilimo na mifugo.
“Vijiji 55 vilivyobaki vinaendelea
kufanyiwa tathmini ya kina maeneo yaliyobaki ndani ya hifadhi na
kuwasilisha mapendekezo yake kwa ajili ya uamuzi. Uchambuzi na taarifa
itatolewa,” amesema na kuongeza kuwa orodha ya maeneo ya vijiji, mapori
ya wanyama, misitu na mashamba yaliyofutwa itatangwa baadaye.
Pia amesema Baraza limeamua ardhi ya mita 500 zilizotengwa kama buffer zone
(eneo kinga) kwenye maeneo ya vijiji vinavyopakana na hifadhi za
wanyama ziachiwe vijiji husika na wananchi wasiondolewe kwenye maeneo
hayo.
Ameyataja maamuzi mengine
yaliyofikiwa kwenye kikao hicho kuwa ni Ofisi ya Makamu wa Rais
imetakiwa ikamilishe mwongozo utakaobainisha matumizi ya ardhi ndani ya
hifadhi ya mita 60 za mito, vyanzo vya maji, maziwa na bahari.
Maamuzi mengine ni kuzitaka Wizara
na taasisi zote za Serikali zilinde maeneo yao kwa kuweka alama za
kudumu zinazoonekana; na kwamba wananchi hawaruhusiwi kuvamia maeneo
mapya na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya uvamizi wowote
kuanzia leo.
Januari, mwaka huu, Rais Magufuli
alitoa maagizo kwa Mawaziri nane wa sekta zinazohusika na matumizi ya
ardhi wachambue na kuandaa taarifa ya mapendekezo ya kutatua migogoro ya
matumizi ya ardhi nchini.
Maagizo hayo yalikuwa ni pamoja
na: Kutoviondoa vijiji na vitongoji 366 vilivyomo ndani ya hifadhi;
Kubainisha maeneo ya hifadhi ambayo yamepoteza sifa ili yaweze kugawiwa
kwa wananchi kwa shughuli za ufugaji na kilimo na kuhakiki na
kurekebisha mipaka baina ya hifadhi za misitu, wanyama na makazi.
Mengine ni kumega baadhi ya
hifadhi za Taifa, mapori tengefu na misitu, kuwagawia wafugaji na
wakulima; Kufanya mapitio ya sheria mbalimbali zinazohusiana na matumizi
ya ardhi; Kupitia upya Sheria ya Vyanzo vya Maji inayozungumzia
uhifadhi ndani ya mita 60; Kuwasilisha mapendekezo ya kufutwa mashamba
yasiyoendelezwa na kugawa kwa wananchi kwa ajili ya uzalishaji wa mazao
ya kilimo na mifugo na kuendelea kulinda na kuhifadhi maeneo ya hifadhi
za misitu, wanyamapori na vyanzo vya maji.
0 comments:
Post a Comment