Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo (wa tatu toka kushoto) akiwa na wataalamu mbalimbali wakati wa
ukaguzi wa barabara zilizopo chini ya usimamizi wa Wakala wa barabara za
Mjini na Vijijini Tanzania (TARURA) katika mji wa Namanyere katika
Wilaya ya Nkasi.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo (wa pili toka Kushoto) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga
Dkt. Khalfan Haule (kushoto) Mratibu wa TARURA Mkoa wa Rukwa Mhandisi
Boniface William ( wa pili toka kulia) pamoja na Mkurugenzi wa manispaa
ya Sumbawanga James Mtalitinya (kulia) wakitembea wakati wa ukaguzi wa
barabara zilizopo chini ya usimamizi wa Wakala wa barabara za Mjini na
Vijijini Tanzania (TARURA) katika mji wa Sumbawanga, Wilayani
Sumbawanga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo pamoja na Wataalamu wengine wakikagua mitaro katika moja ya
barabara za mji wa Sumbawanga.
…………………
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo amesifu juhudi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuhakikisha
anatekeleza ahadi zake alizoahidi kipindi cha kampeni baada ya
kutembelea barabara zinzoendelea kujengwa katika mji mdogo wa Namanyere,
Wilayani Nkasi na kuona kasi ya ujenzi wa barabara hizo ikiendelea
vizuri.
Amesema kuwa ahadi ya mheshimiwa
rais ni kujenga barabara zenye jumla ya kilometa tano katika mji na
mpaka kufikia mwezi Disemba mwaka 2019 zitakuwa zimefikia jumla ya
kilometa 3.95 ambayo ni sawa na asilimia 79 ya utekelezaji wa ahadi zake
na hivyo kumtaka mkandarasi nayeendelea na ujenzi wa barabara ya
kilometa moja afanye haraka kumalizia ujenzi huo ili wananchi waweze
kutumia barabara ambazo zimefungwa kwa muda wa mwaka ili kupisha ujenzi.
“Huyu mkandarasi anayejenga
kilometa moja kwa kiwango cha lami kazi yake inasuasua kwasababu mradi
huu ulipaswa kukamilika mwezi wa sita mwaka huu na sasa ni mwezi wa
tisa, kazi haijakamilika lakini pia kuna kero ambazo zipo ndani ya
barabara hizi, kuna vivuko vimewekwa vya muda na kwengine hakuna, watu
wanapata shida kuvuka mitaro kwenda kufanya biashara zao lakini pia
kwenye matolea ya barabara kuna vifusi, hivyo nakupa siku 12 utoe vifusi
na ujenge vivuko kwenye mitaro,” Alisisitiza.
Awali akitoa taarifa ya
utekelezaji wa ujenzi wa barabara hizo ili kutimiza ahadi za Mheshimiwa
Rais Mratibu wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijiji Tanzania (TARURA)
Mkoa wa Rukwa Mhandisi Boniface William alisema kuwa mbali na
kujitahidi kuhakikisha barabara hizo zinajengwa kwa wakati lakini
kumekuwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti pamoja na upatikanaji wa
malighafi za ujenzi wa barabara hizo hasa kokoto.
“katika utekelezaji wa hii miradi
kumekuwa na changamoto mbalimbali, changamoto mojawapo ni ufinyu wa
bajeti, fedha tunayotengewa kulingana na hali halisi ya ‘site’ unakuta
ile fedha ni kidogo kiasi kwamba kama ile barabara ya salala ilikuwa
tutengeneze kilometa moja lakini kwa milioni 350 tulishindwa kutengeneza
kilometa moja kwahiyo tukaweza kutengeneza mita 700 pekee, tatizo
jingine ni malighafi kwa maana ya kuwa na chanzo kimoja cha kokoto
katika mkoa, hii inachelewesha kazi,” Alisema.
Katika hatua nyingine, Mh. Wangabo
wakati alipomaliza kutrembelea barabara zenye jumla ya kilometa moja
katika manispaa ya Sumbawanga amewataka wakandarasi wazawa wanaopewa
kazi za ujenzi na TARURA kuhakikisha wanaheshimu na kuzingatia masharti
ya mikataba ili kufanya kazi kwa wakati na kuongeza kuwa ikiwa
wakandarasi hao hawataonyesha uaminifu katika kazi hizo ndogo itakuwa
vigumu kwao kupewa miradi mingine mikubwa.
Katika mwaka wa fedha wa 2019/2020
Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Nkasi
wametengewa bajeti ya shilingi milioni 500 wakati TARURA upande wa
Manispaa ya Sumbawanga wametengewa bajeti ya shilingi milioni 460 ili
kuendelea kukamilisha ujenzi wa barabara katika kutimiza ahadi za Rais
Dkt. John Pombe Magufuli.
0 comments:
Post a Comment