Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na vijana watakaoshiriki Mafunzo ya
Urasimishaji Ujuzi uliopatikana nje ya Mfumo rasmi wakati wa hafla ya
uzinduzi wa Programu hiyo kwa Mwaka 2019/2020 iliyofanyika Mkoani Tanga.
Baadhi ya Wanagenzi walionufaika
kushiriki mafunzo ya urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo usio
rasmi wakisikiliza hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.
Jenista Mhagama ( hayupo pichani).
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Martin
Shingela akieleza jambo wakati wa uzinduzi wa programu ya mafunzo ya
urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi yaliyofanyika katika
Viwanja vya Tangamano, Mkoani Tanga Septemba 18, 2019.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Bi. Stella Ndimubenya akielezea
jambo wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Mafunzo ya Urasimishaji Ujuzi
uliopatikana Nje ya Mfumo rasmi kwa mwaka 2019/2020 na ugawaji vyeti kwa
wahitimu waliomaliza mafunzo hayo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Wanagenzi wanaopata Mafunzo kupitia
VETA alipowatembelea kwa lengo la kuangalia mafunzo yao ya vitendo eneo
la Raska Zone, Mkoani Tanga.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista
Mhagama akikagua Ukuta uliojengwa na Vijana wa fani ya ujenzi waliopo
kwenye programu ya mafunzo ya urasimishaji.
Mratibu wa Programu ya Mafunzo ya
Urasimishaji Ujuzi uliopatikana nje ya Mfumo rasmi kutoka VETA, Bw.
Bwire Ally akielezea jambo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista
Mhagama. Wa pili kutoka Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin
Shingela.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista
Mhagama akiangalia Sharbati “Juice” iliyotengenezwa na mmoja wa
wanagenzi wa fani ya Uhudumu wa Hoteli Bi. Irene Emmanuel ambaye ni
Mnufaika wa Programu hiyo.
PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
*********************************
Na; Mwandishi Wetu
Programu ya Ukuzaji Ujuzi
inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ni chachu ya mafanikio kwa
vijana katika kukuza ujuzi wao kupitia mafunzo mbalimbali ya ufundi
stadi ambayo yamewajengea uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi
wa Programu ya Urasimishaji Ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi Kwa
Mwaka 2019/2020 uliofanyika katika Viwanja vya Tangamano, Mkoani Tanga
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alieleza kuwa
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu iliandaa programu hii ya kitaifa
ya miaka mitano ya kukuza ujuzi kwa nguvu kazi ambapo utekelezaji wake
umeanza kutoa fursa kwa vijana kupata ujuzi katika sekta mbalimbali.
“Programu hii imewasaidia
vijana kupata kazi zenye staha na imewafanya waweze kuwa washindani
katika soko la ajira sambamba na kuongeza tija mahali pa kazi kwa kuwa
waajiri wamekuwa wakipata wafanyakazi wenye viwango vya ujuzi
unaotambulika,” alisema Mhagama.
Alisema zoezi la utambuzi na
urasimishaji ujuzi una lengo la kutambua, kutathmini na kurasimisha
ujuzi uliopatikana kupitia nje ya mfumo rasmi wa mafunzo, hivyo kupitia
programu hii taaluma na ujuzi wa vijana utatambulika na wataweza kupata
ajira.
“Serikali imekuwa na mikakati
ya kujenga taifa lenye viwanda vingi vitakavyo kuwa vinatoa asilimia 40%
ya ajira kwa vijana wasiokuwa na ajira, hivyo ili kufikia azma hiyo
nguvu kazi yenye ujuzi rasmi na unaotambulika itakuwa na manufaa katika
soko la ajira,” alieleza Mhagama
Aidha Mhe. Mhagama alitoa wito
kwa vijana wenye ujuzi katika fani mbalimbali na hawana vyeti
vinavyotambulisha ujuzi wao, wafike katika vyuo vya VETA vilivyopo
karibu yao ili waweze kujiandikisha kwa ajili ya kurasimisha ujuzi wao.
Katika uzinduzi huo, Waziri
Mhagama alitoa vyeti kwa vijana zaidi ya 500 waliopata mafunzo kwenye
nyanja mbalimbali ikiwemo Ufundi wa Magari (Makenika), Uhudumu wa
Hoteli, Ufundi Ujenzi, Upishi na Ufundi Seremala.
Aliwahimiza vijana hao
waliohitimu mafunzo kutumia fursa ya miradi ya kimkakati inayoanzishwa
katika mkoa huo. Pamoja na kuchangamkia zabuni za kutoa huduma na ufundi
katika maeneo mbalimbali.
Pia Waziri Mhagama aliwataka
Maafisa Maendeleo ya Vijana, Maafisa Biashara na Maafisa Maendeleo ya
Jamii kutoka kwenye halmashauri mbalimbali walizotoka vijana hao
waliohitimu mafunzo kupatiwa msaada wa kitaalamu utakaowawezesha
kuanzisha na kusajili vikundi na makampuni kisheria.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa
Tanga Mhe. Martin Shigela alisema kuwa amefarijika kuona vijanna wa mkoa
wa Tanga watanufaika na programu hiyo ambayo itawajengea hamasa ya
kupenda kurasimisha ujuzi wao.
“Katika Mkoa wa Tanga
wanagenzi 1015 watashiriki kwenye mafunzo hayo na takwimu zilizosomwa
hapa zinaonesha mkoa wa Tanga utakuwa umevuka malengo kwa asilimia 5.2%,
nimefarijika sana,” alisema Shigela.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Bi. Stella
Ndimubenya alisema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana pamoja na
kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwawezesha mafunzo stadi vijana
yatakayowafanya wakuze uchumi wao na kuwa na mchango katika kujenga
Tanzania mpya ya Viwanda.
“Awamu hii tumeamua kuongeza
wigo wa wanufaika kupitia fani ya ufundi umeme, uungaji wa Vyuma,
Ushonaji, Ufundi bomba na Unyooshaji wa bodi za magari,” alisema
Ndimubenya.
Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,
Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu inaratibu Programu ya Ukuzaji Ujuzi
ikiwemo Mafunzo kwa Njia ya Uanagenzi, Mafunzo ya Urasimishaji Ujuzi
uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi, Mafunzo ya Vitendo Mahala pa Kazi kwa
Wahitimu na Mafunzo ya Ukuzaji Ujuzi kwa walio Makazini.
Mpango huo wa Urasimishaji
Ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi (Recognition of Prior Learning)
ulizinduliwa na Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Mohamed Bilal Septemba 2014.
0 comments:
Post a Comment