METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, September 11, 2019

MHE HASUNGA AWASILISHA BUNGENI AZIMIO LA KULINDA HAKIMILIKI ZA WAGUNDUZI WA AINA MPYA ZA MBEGU

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwasilisha Bungeni Jijini Dodoma azimio la kuridhia itifaki ya Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika kuhusu kulinda hakimiliki za wagunduzi wa aina mpya za mbegu za mimea (Protocol for Protection of New Varieties of Plants (Plant Breeders’ Rights) in southern African Development Community-SADC) leo tarehe 11 Septemba 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwasilisha Bungeni Jijini Dodoma azimio la kuridhia itifaki ya Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika kuhusu kulinda hakimiliki za wagunduzi wa aina mpya za mbegu za mimea (Protocol for Protection of New Varieties of Plants (Plant Breeders’ Rights) in southern African Development Community-SADC) leo tarehe 11 Septemba 2019. 
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akijiandaa kwa ajili ya kuwasilisha azimio la kuridhia itifaki ya Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika kuhusu kulinda hakimiliki za wagunduzi wa aina mpya za mbegu za mimea (Protocol for Protection of New Varieties of Plants (Plant Breeders’ Rights) in southern African Development Community-SADC) Bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 11 Septemba 2019. 

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amewasilisha Bungeni Jijini Dodoma azimio la kuridhia itifaki ya Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika kuhusu kulinda hakimiliki za wagunduzi wa aina mpya za mbegu za mimea (Protocol for Protection of New Varieties of Plants (Plant Breeders’ Rights) in southern African Development Community-SADC) leo tarehe 11 Septemba 2019. 

Akizungumza wakati wa uwasilishaji huo Waziri Hasunga amesema kuwa Chimbuko la Azimio hilo ni Mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Southern African Development Community -SADC). Ibara ya 22 ya Mkataba wa SADC- (SADC Treaty), wa mwaka 1992 ambao umebainisha umuhimu wa kuandaa Itifaki za kutoa miongozo ya ushirikiano kwenye masuala ya maendeleo.

Alisema nchi wanachama wa SADC ziliandaa Itifaki ya SADC ya Kulinda Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea Mwezi Mei, 2017. Itifaki hiyo iliidhinishwa na  Mawaziri wa Katiba na Sheria wa nchi za SADC Julai, 2017 na baadae ilithibitishwa na Baraza la Mawaziri wa Kilimo la SADC Agosti, 2017 mjini Ezulwini, eSwatini. Lengo kuu la Itifaki hiyo ni kutoa mwongozo kuhusu kulinda Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya ya Mbegu za Mimea ili kuhamasisha ugunduzi wa mbegu mpya katika Ukanda wa SADC

Mhe Hasunga amesema kuwa hadi sasa nchi zilizosaini Itifaki hiyo ni saba (7) ikiwemo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ilisaini tarehe 18 Agosti, 2018 wakati wa Mkutano wa nchi wanachama wa SADC uliofanyika Windhoeck, Namibia. Ambapo, mnamo tarehe 31 Oktoba, 2018 Baraza la Mapinduzi Zanzibar liliridhia mapendekezo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha Itifaki hiyo Bungeni ili iweze kuridhiwa.

Alisema kuwa itifaki hiyo ina sehemu 10 ambazo ni sehemu ya kwanza yenye Ibara 5 inabainisha malengo na mawanda (scope) ya Itifaki hiyo, Sehemu ya Pili yenye Ibara 5 ambapo Ibara ya 7 inaweka vigezo na masharti ya kuzingatia katika utoaji wa hakimiliki za wagunduzi wa aina mpya za mbegu za mimea, Sehemu ya Tatu na Nne zenye Ibara kumi na nne (14) inabainisha utaratibu utakaotumika katika utoaji wa hakimiliki za wagunduzi wa aina mpya ya mbegu za mimea na namna ya kushughulikia maombi ya hakimiliki.

Aliongeza kuwa Sehemu ya Tano inahusu muda wa hakimiliki iliyotolewa chini ya Itifaki ambayo itadumu kwa miaka ishirini na tano (25) kwa mazao ya miti na jamii ya mizabibu na miaka ishirini (20) kwa mazao mengine, Sehemu ya Sita, Saba na Nane inahusu utoaji wa leseni na uhawilishaji wa hakimiliki hizo ambapo Ibara ya 34 inaweka masharti kwa ajili ya uhaulishaji wa hakimiliki, na Sehemu ya Tisa na Sehemu ya Kumi inahusu masuala ya jumla ambapo Ibara ya 43 inahusu usuluhishi wa migogoro (Dispute settlement) na inabainisha kuwa, migogoro kati ya nchi wanachama wa SADC kuhusu utekelezaji wa Itifaki hiyo iliyoshindwa kupata usuluhishi kwa mazungumzo, itawasilishwa kwa Mawaziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula wa nchi wanachama wa SADC. 

Aidha, Mhe Hasunga amesema kuwa pamoja na mapendekezo ya kuridhiwa kwa Itifaki hiyo, Azimio hilo linaweka sharti (Reservation) litakaloiwezesha Tanzania kutolazimika kutekeleza masharti ya Itifaki ambayo yanaweza kuathiri maslahi ya Taifa. Utaratibu huu unatambuliwa kimataifa kupitia Sehemu ya Pili ya Itifaki ya Vienna Convention on the Law of Treaties uliosainiwa mwaka 1969 ambapo Tanzania ni mojawapo ya nchi zilizoridhia kutumia Mkataba huu tangu tarehe 12 Aprili, 1974.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni miongoni mwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (The Southern African Development Community -SADC) kwa mujibu wa Mkataba ulioianzisha Jumuiya hii ambao ulisainiwa na Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika mnamo 1992;

MWISHO.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com