Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa Tatu kutoka kulia) akikagua maendeleo ya mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Mtera.Wengine katika picha ni watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Kituo cha kupoza umeme cha Mtera ambacho kinafanyiwa upanuzi ili kuweza kuhudumia Vijiji takribani 70 katika mkoa wa Iringa na Dodoma.
Teresia
Mhagama na Hafsa Omar
Mkandarasi
anayetekeleza mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Mtera, ameagizwa
kumaliza kazi hiyo ifikapo tarehe 4 Oktoba mwaka huu ili kuwezesha vijiji
takribani 70 katika mkoa wa Iringa na Dodoma kupata umeme wa uhakika kwani sasa
wanapata umeme wenye nguvu dogo.
Maagizo hayo
yalitolewa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani tarehe 10 Septemba, 2019
mara baada ya kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika kituo hicho na kutoridhishwa
na kasi ya mkandarasi, kampuni ya SUNIR kutoka Iran.
“Mwaka 2017,
Novemba tulimpa mkandarasi huyu kazi ambayo alipaswa kumaliza ndani ya
miezi 18 lakini hajafanya kazi vizuri na kazi zinazofanyika hapa haziendani na
hatua ambayo ilibidi ifikiwe kwa sasa.” Alisema Dkt Kalemani.
Aidha, baada
ya kufika kwenye eneo la mradi huo, Dkt Kalemani alikuta vibarua wanne tu wapo
kazini na mkandarasi wa kampuni hiyo kutoka nchini Iran hakuwepo eneo la kazi,
hivyo alimuagiza msimamizi wa mradi huo kutoka TANESCO kuhakikisha kuwa
mkandarasi huyo anaongeza vibarua.
Vilevile
aliagiza kuwa, Mkandarasi huyo kutoka Iran ahakikishe anafika nchini ndani ya
siku tatu ili kuweza kuchukua hatua zitakazowesha mradi huo kutekelezwa kwa
kasi.
Alisema
kuwa, kituo hicho kitafungwa transfoma mbili zenye uwezo wa 10MVA kila
moja na fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo ni Dola za Marekani milioni
3.2.
“Transfoma
hizi kwa sasa bado zipo bandarini lakini natoa maelekezo kwa TANESCO na Wakala
wa Nishati Vijijini (REA), kuhakikisha kuwa transfoma hizo zinatolewa bandarini
ndani ya siku Tano ili zifungwe na ziweze kufanya kazi.”Alisema Dkt Kalemani.
Alieleza
kuwa, awali Kituo cha kupoza umeme cha Mtera kilijengwa kwa ajili ya kuhudumia
eneo hilo lenye mitambo ya kuzalisha umeme pekee lakini Serikali iliamua
kukipanua kituo hicho ili kuweza kuhudumia pia maeneo na Vijiji vya jirani.
Katika
ukaguzi huo wa kushtukiza, Waziri wa Nishati, aliambatana na Kamishna Msaidizi
wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi
Amos Maganga.
0 comments:
Post a Comment