METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, September 22, 2019

MAMA GETRUDE MONGELA KUWA MGENI RASMI KATIKA TAMASHA LA JINSIA MWAKA 2019

Ikiwa imebaki siku moja kabla ya kufanyika kwa Tamasha la 14 la jinsia, TGNP Mtandao limemtaja Balozi Mama Getrude Mongela kuwa mgeni rasmi katika tamasha la 14 linalotarajiwa kuanza September 24 hadi  27,  2019.
 Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao. Lilian Lundi akitoa ufafanuzi wa jambo fulani ,mbele ya waandishi wa habari mapema leo jijini Dar es salaam.

Haya yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Lilian Liundi wakati akizungumza na  waandishi wa habari Mapema leo Jijini Dar es Salaam.

Akifafanua sababu za kumpa heshima Mama Mongela kuwa Mgeni Rasmi katika Tamasha hilo la 14, Liundi amesema kuna sababu nyingi za kufanya hivyo lakini kubwa ni harakati zake alizozifanya hadi kufikia hatua za kuleta mageuzi ya kijinsia hapa Nchini.

“Kipekee Tanzania itakumbukwa katika historia  kwa kuweka misingi ya usawa wa kijinsia na haki za wanawake kwani katika mkutano wa Beijing Balozi Getrude mongela aliibuka kidedea katika mkutano huo”. alisema Mkurugenzi

Ameongeza kuwa zaidi ya watu 1000 kutoka ndani na nje ya Tanzania wanatarajiwa kushiriki Tamasha la mwaka huu, ambapo litaongozwa na kauli mbiu inayosema 'Wanaharakati wa Jinsia Mbioni Kubadilisha Dunia' 

Lilian Liundi amesema washiriki wa tamasha hilo watakuwa ni pamoja na wawakilishi wa asasi za kiraia kutoka ndani na nje ya nchi, viongozi mbalimbali kutoka ngazi ya halmashauri na serikali kuu, wanaharakati na wananchi wa kawaida.
Mkutano ukiendelea.

"Tunatarajia tamasha la Jinsia la Mwaka huu litakuwa la kipekee kwani kitaifa na kidunia tumeanza kusherehekea maadhimisho ya miaka 25 ya Azimio na Mpango kazi wa Beijing amabapo vitaenda sambamba na miaka 25 ya TGNP Mtandao".

Amesisitiza kuwa Tamasha hilo litaudhuliwa na wageni kutoka nchi kama Rwanda, Afrika kusini, Burundi, Swizland, Kenya, Uganda, Ghana na Zimbabwe na pia linatoa fursa kwa asasi za kiraia zilizoshiriki katika mchakato wa Beijing kutakafari na kusherehekea uwepo wa asasi hizo kwa zaidi ya miaka 25 ambapo azimio na mpango kazi Beijing ndiyo iliyoweka misingii ya usawa wa kijinsia na haki za wanawake kidunia.

"Katika kuendelea kuenzi na kuthamini mchango wa Mama Getrude Mongella,TGNP na Tapo la Ukombozi,tumeamua kumchagua Balozi Mhe. Dr. Getrude Mongella aliyeongoza mchakato wa Beijing na pia mchakato wa 'Kuileta Beijing Nyumbani' kuwa mgeni rasmi wa Tamasha la Jinsia mwaka huu",alifafanua Liundi. 

Alibainisha kuwa tamasha hilo litahusisha mawasilisho,mijadala ya pamoja, maonesho na warsha, kusherekea mchango wa mashujaa wanawake katika kufikia haki na usawa wa kijinsia.
Baadhi ya wanachama wa TGNP Mtandao wakiongea na waandishi wa habari.

Mkutano ukiendelea.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com