
*******************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewaonya watu wote wakiwemo wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu ambao
wanajihusisha na utoroshaji wa madini, waache mara moja, Serikali ipo
makini imejidhatiti vya kutosha na kwamba haitokuwa na huruma dhidi
yao.
Serikali imefuta kodi ya ongezeko
la thamani (VAT-18%) na kodi ya zuio (withholding tax-5%) kwa wachimbaji
watakaouza madini kwenye masoko yalioanzishwa nchini ikiwa ni mikakati
ya kuwaendeleza wachimbaji wadogo ili waweze kuongeza uzalishaji na
hivyo kujiongezea tija na kuchangia katika pato la Taifa.
Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo
(Jumapili, Septemba 22, 2019) wakati akifungua maonesho ya Teknolojia
na Uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayofanyika kwenye uwanja wa CCM
Kahangalala mjini Geita. Amesema kwa wale wasiotaka kuelewa na kuacha
kutorosha madini Serikali itashughulika nao.
Waziri Mkuu amesema Serikali
itaendelea kutatua changamoto wanazokutana nazo wachimbaji wadogo
ikiwemo matumizi ya teknolojia duni katika uchimbaji na uchenjuaji
madini. “Nitoe wito kwa wadau kuitumia fursa ya uwekezaji kwa kuanzisha
biashara ya vifaa vya uchimbaji na uchenjuaji nchini.”
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa
hiyo kuwakumbusha wadau wa madini kuwa katika mkutano wa 16, wa Bunge la
11 lilijadili na kuridhia Azimio la Kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu
kupunguza kwa kadiri iwezekanavyo matumizi ya zebaki ifikapo 2030.
Amesema lengo la mkataba huo ni
kuanza kupunguza na hatimaye kuacha matumizi ya zebaki kwenye uchenjuaji
wa dhahabu hususan kwa wachimbaji wadogo. Kwa mantiki hiyo, amewasihi
wachimbaji wadogo kuepuka matumizi ya zebaki katika uchenjuaji na kuanza
kutumia njia nyingine zilizopo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amesema kwa kipindi kirefu kumekuwepo na changamoto ya wachimbaji
wadogo kufanya shughuli za uchimbaji bila kuwa na taarifa sahihi za
kijiolojia, hivyo kusababisha wachimbaji wengi wadogo kuchimba kwa
kubahatisha na hata wengine kutumia imani za kimila katika kuchagua
maeneo ya uchimbaji.
“Kwa msingi huo, nawahimiza wadau
mbalimbali katika Sekta ya Madini hususan wachimbaji wadogo kuitumia
kikamilifu Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili
kupata taarifa muhimu na sahihi za kijiolojia pamoja na ushauri wa
kitaalamu katika utafutaji wa madini.”
Amesema sambamba na kutenga maeneo
kwa ajili ya wachimbaji wadogo kwa kuzingatia taarifa za kijiolojia
kupitia GST na STAMICO, Serikali imeendelea kuandaa machapisho yenye
kuonesha maeneo yanakopatikana madini nchini.
Waziri Mkuu amewataka wachimbaji
wadogo kutumia fursa ya uwepo wa taasisi hiyo ili kuepuka kuwekeza fedha
zao nyingi katika maeneo ambayo hayana madini na hivyo, kufanya kazi
kwa kubahatisha jambo ambalo halina tija kwao na Serikali kwa ujumla.
Amesema Serikali imeanzisha vituo
vya umahiri na vituo vya mfano kwenye baadhi ya maeneo nchini kwa ajili
ya kutoa mafunzo mbalimbali kuhusu masuala ya madini kwa wachimbaji
wadogo, pia vituo hivyo, vitatumika kufanya maonesho ya madini na vifaa
vinavyotumika katika shughuli za uchimbaji madini.
Kaulimbiu ya maonesho hayoinasema
‘Madini ni Chachu ya Ukuaji wa Uchumi wa Viwanda’ Tuwekeze kwenye
Teknolojia Bora ya Uzalishaji na Tuyalinde Masoko ya Madini.
Amesema kaulimbiu hiyo inakwenda
sambamba na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya
mwaka 2015/2020 ambayo pamoja na mambo mengine inaielekeza Serikali
kusimamia na kuhakikisha uwekezaji katika shughuli za kuongeza thamani
madini ili kukuza mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini
Doto Biteko amesema kwa sasaSerikali na makampuni yanayomiliki migodi
wanaheshimiana kwani makampuni hayo yanatii magizo na kufuata sheria za
nchi.
Waziri Doto amesema kabla ya
kuåfunguliwa kwa masoko ya madini nchini makusanyo ya dhahabu yalikuwa
kilo 101 kwa mwezi hivi sasa baada ya masoko kufunguliwa makusanyo
yameongezeka na kufikia kilo 1,974.
Hata hivyo, Waziri huyo wa
Madini amesema kwa sasa nidhamu ya Watanzaniua katika kusimamia ununuzi
na uuzaji dhahabu imevutia wauzaji dhahabu toka nchi za jirani kwani
hakuna tena wizi wala utapeli katika biashara hiyo.
Hivyo, Waziri huyo ameyataka
makampuni yanayomiliki migodi kutoa tenda kubwa kwa wazawa na makampuni
ya ndani badala ya kuyapa makampuni ya nje na kuzipa kampuni za ndani
tenda ndogondogo.
0 comments:
Post a Comment