
Na Ismail Ngayonga,MAELEZO
DAR ES SALAAM
SERIKALI kupitia Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inatekeleza Mkakati
maalum unaolenga kuziwezesha Halmashauri kujitegemea kimapato ili kutoa
huduma bora zaidi na zenye uhakika kwa wananchi.
Katika kutekeleza Mkakati huu,
Wizara ya Fedha na Mipango imetoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za
Mitaa kuhakikisha zinatumia kwa ukamilifu fursa za kimapato zilizopo
katika maeneo yao na hivyo kuongeza uwezo wa kujitegemea kimapato.
Takwimu zinaonesha kuwa bajeti za
Mamlaka za Serikali za Mitaa hutegemea ruzuku kwa zaidi ya asilimia 88
kutoka Serikali Kuu katika kuchangia utekelezaji wa bajeti pamoja na
kugharamia utekelezaji wa majukumu mbalimbali.
Kwa kuzingatia sababu hizo, Wizara
ya Fedha na Mipango imeanzisha utaratibu kwa Halmashauri mbalimbali
nchini kufanya mawasilisho ya miradi yao ya kimkakati katika eneo la
kujijenga kimapato kwa madhumuni ya kujitegemea na kuboresha utoaji wa
huduma.
Msingi wa utaratibu huu unatokana
na ukweli kwamba upatikanaji wa mapato ya kutosha na yenye uhakika
katika Halmashauri ni nguzo imara katika kuboresha utoaji huduma nzuri
na zenye uhakika kwa wananchi.
Akiwasilisha Makadirio ya Hatuba
ya Bajeti kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo anasema Ofisi ya
Rais TAMISEMI ilianza utaratibu wa utekelezaji wa miradi ya kimkakati
katika Mwaka wa Fedha 2017/18.
Anasema miradi hiyo inapaswa kuwa
na sifa ya kuiwezesha Halmashauri kuongeza mapato ya ndani ya
Halmashauri ili kuziwezesha kujitegemea kimapato na kupunguza utegemezi
wa Ruzuku ya Serikali Kuu.
Anaongeza kuwa hadi Februari, 2019
jumla ya Halmashauri 29 zenye miradi 37 zimekidhi vigezo vya kupatiwa
jumla ya Tsh Bilioni 268.84 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati
ambapo katika awamu ya kwanza Halmashauri 18 zenye miradi 23 zilikidhi
vigezo vya kupatiwa jumla ya Tsh Bilioni 131.46.
“Kati ya Fedha hizo Tsh Bilioni
31.36 zimepokelewa kwenye Halmashauri hizo ambazo zimesaini mikataba ya
utekelezaji wa miradi ya kimkakati zitakazotumika kutekeleza miradi ya
ujenzi wa masoko, viwanda, machinjio, vituo vya mabasi na maghala ya
kuhifadhia mazao” alisema Jafo.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo anasema
katika Awamu ya Pili, Halmashauri nyingine 12 zenye miradi 15 zimekidhi
vigezo vya kupatiwa jumla ya Tsh Bilioni 137.37 mwezi Januari, 2019 na
kusaini mikataba ya utekelezaji wa miradi hiyo itakayohusisha ujenzi wa
masoko ya kisasa, machinjio ya kisasa, vituo vya mabasi, uendelezaji wa
ufukwe wa Oysterbay.
Waziri Jafo anasema Ofisi ya Rais –
TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango inaendelea
kujenga uwezo kwa Halmashauri kuziwezesha kuibua miradi, kufanya
upembuzi yakinifu ili miradi hiyo iweze kukidhi vigezo na kupata fedha
na kuitekeleza kwa ufanisi.
Upatikanaji wa mapato ya kutosha
na yenye uhakika katika Halmashauri ni nguzo imara katika kutatua
changamoto za mapato katika ngazi ya halmashauri ni pamoja na uwezo
mdogo wa kubaini na kutumia fursa zilizopo pamoja na usimamizi hafifu
katika ukusanyaji, utunzaji na matumizi ya mapato ambazo zina athari
katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Matumizi mazuri na yenye tija ya
fursa hizi katika vyanzo vya mapato yataziwezesha Halmashauri kuwa na
vyanzo vya uhakika ili kujijengea uwezo wa kujitegemea na hivyo
kuiwezesha Serikali Kuu kuongeza nguvu na msukumo katika Halmashauri
zenye uhitaji zaidi.
0 comments:
Post a Comment