Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akishuhudia wakati Mkurugenzi wa Kampuni ya Nsagali,
Emmanuel Gangu Silanga (kushoto) alipomkabidhi fedha Katibu Mkuu wa Chama
cha Ushirka cha Msingi cha Maendeleo Luguru na Itubilo, Bibi Buzo
Hussein kwa ajili ya kuwalipa walikuma watakaouza pamba kwenye chama
hicho. Kampuni hiyo imeahidi kununua pamba yote mkoani Simiyu na
imemhakikishia Waziri Mkuu kuwa inazo pesa za kutosha. Mheshimiwa Majaliwa
alikuwa katika ziara ya kukagua ununuzi wa pamba, Agosti 8, 2019. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama pamba wakati alipotembelea ghala la Chama
cha Ushirika cha Msingi cha Kumalija cha wilayani Maswa Agosti 8,
2019. Waziri Mkuu alikuwa katika ziara ya kukagua ununuzi wa pamba katika mkoa
wa Simiyu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekerwa
na kitendo cha Mamlaka ya Maji wilayani Maswa kupandisha bili ya maji kutoka sh
5,000 hadi sh. 28,000 jambo ambalo amesema halikubaliki na amemuagiza Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka akutane na wahusika leo.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana
jioni (Alhamisi, Agosti 8, 2019) wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha
Kumalija, wilayani Maswa mara baada ya kutembelea ghala la pamba la Chama cha
Msingi cha Kumalija.
“Haiwezekani bili ikapanda kwa kiasi
hicho. Hapo utakuwa unamsaidia mwananchi myonge au utakuwa unamnyonga. Bili
haiwezi kupandishwa kwa asilimia kubwa kiasi hicho yaani imetoka shilingi elfu
tano hadi shilingi elfu ishirini na nane.”
Waziri Mkuu alisema Serikali
inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani,
inayolenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na
salama, hivyo upandishaji huo wa bili hauna tija kwa wananchi wanyonge.
Wakati huo huo,Waziri Mkuu alisema
Serikali imetoa sh. milioni 440 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la
upasuaji, ukarabati wa wodi na duka la dawa, upanuzi wa wodi ya watoto na
ujenzi wa wodi ya wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa, ambapo ujenzi
wake unaendelea.
Alisema mbali na fedha hizo, pia
Serikali imepeleka sh. milioni 881 wilayani Maswa ambapo kati yake sh. milioni
481 ni kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa kituo vya afya cha Malampaka, kwa
ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya kituo cha afya cha Mwabayanda.
Akizungumza kuhusu elimu msingi bila
malipo, Waziri Mkuu alisema kuanzia mwaka 2016 hadi 2019 Serikali imepeleka
wilayani Maswa jumla ya sh. bilioni 2.1, kwa ajili ya ukarabati, utawala,
michezo, mitihani na posho kwa Maofisa Elimu wa kata na Walimu Wakuu katika
shule 28 za msingi.
Pia Waziri Mkuu alisema Serikali
kuanzia mwaka 2016 hadi 2019 imepeleka wilayani Maswa jumla ya sh.
bilioni 2.7 kwa ajili ya fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya
madaraka kwa Wakuu wa Shule katika shule 16 za Sekondari.
0 comments:
Post a Comment