METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, September 29, 2018

MTENDAJI MKUU NFRA AMHIMIZA MKANDARASI KUONGEZA SPIDI UJENZI WA VIHENGE SONGEA

Mkandarasi wa mradi wa ujenzi vihenge (Silos) na Maghala ya kisasa Mhandisi Robert Lupinda akimuelezea Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula Bi Vumilia L. Zikankuba kuhusu hatua zilizofikiwa za ujenzi.
Uchanganyaji Wa zenge ukiendelea kwa ajili ya ujenzi wa vihenge na maghala ya kisasa Mjini Songea.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula Bi Vumilia L. Zikankuba akiwasili eneo la mradi Mjini Songea.
Uchimbaji na ujenzi wa msingi wa Vihenge ukiendelea

Na Mathias Canal, NFRA

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula Bi Vumilia L. Zikankuba amepongeza hatua za awali zilizofikiwa mpaka sasa za muendelezo wa ujenzi wa Vihenge na maghala ya kisasa huku akimhimiza mkandarasi pamoja na maendeleo hayo mazuri kuongeza kasi ili kukamilisha misingi yote ya vihenge 12 kabla msimu wa mvua kuanza.

Zikankuba ametoa hamasa hiyo Mjini Songea Mkoani Ruvuma Leo tarehe 29 Septemba 2018 wakati akiwa katika ziara ya kikazi kukagua Maendeleo ya ujenzi wa vihenge (Silos) na maghala ya kisasa.

Aliongeza kuwa, Wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula umeanza mpango wa ujenzi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula katika Kanda zote za Wakala ambapo mjini Songea NFRA inajenga vihenge vya kisasa 12 vyenye wastani wa jumla ya uwezo wa kuhifadhi tani 45,000. Pamoja na maghala mawili yenye uwezo wa kila moja tani 5,000 na kufanya ongezeko la uhifadhi kufikia 55,000.

Naye muwakilishi wa Mkandarasi wa mradi huo Mhandisi Robert Lupinda amemwomba Mtendaji Mkuu NFRA kushughulikia suala la msamaha wa kodi kwa vifaa vinavyonunuliwa hapa nchini ili kupunguza gharama za utekelezaji wa mradi.

Katika hatua ya utekelezaji Lupinda alisema kuwa Mradi wa mjini Songea unaojengwa na Kampuni ya Feerum S.A kutoka nchini Poland kwa kushirikiana na kampuni ya wazawa ya Civil Loth Enterprises Ltd ambao ni sub contractor umefikia hatua za kuridhisha.

"Kwa ujumla kazi inaendelea vizuri, mkandarasi anatarajia kuanza ufungaji wa vihenge (Silo Installation) mwishoni mwa mwezi wa kumi hivyo ni matumaini yetu kama Wakala kusimamia na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati" Alikaririwa Lupinda

Alieleza kuwa mpaka sasa kazi ya uchimbaji wa misingi kwa vihenge 8 imekamilika, mkandarasi amemwaga zege la chini (Bottom Ring) lenye unene wa mita moja kwa misingi ya vihenge 7 pamoja na kufunga nondo (Vertical Reinforcements) kwa vihenge vingine 7.
Alieza kuwa Usimamizi mzuri wa Wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula (NFRA) pamoja na Meneja mradi wa wakala wa majengo Tanzania (TBA) umepelekea utekelezaji kuwa mzuri na kiwango cha kuridhisha.

Mtendaji Mkuu huyo amemuahidi Mkandarasi kufuatilia suala hilo na kumuhakikishia kuwa limeshafikishwa katika Wizara husika na limefikia hatua nzuri. Hivyo, NFRA inataraji katika kipindi cha hivi karibuni kupatiwa ufumbuzi na Mamlaka husika na kueleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo katika Kanda ya Songea, Makambako, Mbozi, Dodoma, Arusha na Shinyanga.

Amemuhimiza Mkandarasi kuhakikisha suala la mawasilisiliano kati ya Mkandarasi, TBA na NFRA linazingatiwa na kuimarishwa zaidi ili kuhakikisha Changamoto zozote zinazoweza kuathiri utekelezaji wa mradi huo zinapata ufumbuzi wa haraka. " Lengo ni kuhakikisha kuwa mradi unakamilika ndani ya muda wa mkataba ambao ni mwishoni mwa mwaka 2019" Alisema Vumilia

Wakati huo huo, Vumilia alisema kuwa Wakala umeanza Mkakati wa kuwapata wataalamu hapa nchini ambao wataandaliwa kwa ajili ya kuendesha mitambo na kutumia technolojia hiyo baada ya mradi kukamilika. "Wataalamu hawa watashiriki zoezi la ujenzi wa vihenge na maghala na kupata mafunzo ya teknolojia hii hapa nchini na baadae nchini Poland" Alisisitiza Vumilia

MWISHO.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com