Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha vitabu baada ya kukata utepe kuzinduliwa Mfumo wa Kielektroniki
wa Kusimamia Biashara (Agricultural Trade Management Information System
(ATMIS) wakati alipohitimisha Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima Nane Nane
yaliyofanyika kwenye uwanja wa Nyakabindi mkoani Simiyu, Agosti 8,
2019. Wengine pichani kutoka kushoto ni Katibu Mkuu wa CCM, Dkt
Bashiru Ally, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, Waziri wa Kilimo,
Japhet Hasunga na kulia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameagiza
kwamba kuanzia mwakani malipo yote ya wakulima wa pamba yawe yanapitia benki
ambapo wakulima wataingiziwa fedha kupitia akaunti zao.
Hivyo, ametumia fursa hiyo kuwasihi
wakulima wafungue akaunti katika benki mbalimbali zilizopo kwenye maeneo yao
ili waweze kufanikisha mkakati huo na pia kuhifadhi fedha zao kwa
ajili ya matumizi ya baadae.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana
jioni (Alhamisi, Agosti 8, 2019) wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha
Luguru, wilayani Itilima mara baada ya kukagua ghala la pamba la Chama
cha Ushirika cha Msingi cha Maendeleo.
Alitembelea kijiji hicho kwa lengo la
kujionea mwenendo wa uuzaji wa zao la pamba katika Chama cha Msingi Maendeleo
na alihakikishiwa kwamba kwa sasa uuzaji wa pamba unaendelea vizuri
Waziri Mkuu alisema ni vizuri malipo ya
wakulima yapitie benki ili kuwawezesha kupanga matumizi mazuri ya fedha zao na
pia watapa fursa ya elimu ya matumizi mazuri ya fedha.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
alieleza miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali katika wilaya hiyo
ukiwemo mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ambao umefikia asilimia 95.
“Jumla shilingi bilioni 1.5 zimetolewa na
Serikali kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya inayojengwa eneo la Nguno,
ambapo majengo yote saba ya kiupaumbele yamekamilika.”
Alisema mwaka 2017/2018 Serikali ilitoa
sh. bilioni 2.34 kwa ajili ya miradi ya maji ya vijiji vya Lagangabilili, Mwamapalala,
Kabale, Ikungulipu na Isengwa, yote imekamilika na inatoa maji.
Alisema mwaka 2019/2020 Halmashauri
hiyo kupitia RUWASA imetengewa sh. bilioni 4.84 kwa ajili ya ujenzi na
ukarabati wa miundombinu ya maji. Mradi huo utavinufaisha vijiji 78.
Awali,Katibu Mkuu wa Chama
cha Msingi cha Maendeleo Luguru na Itubilo, Buzo Hussein alimshukuru Waziri
Mkuu kwani wakati wote amekuwa mstari wa mbele katika kufuatilia kero
mbalimbali zinazowakabili wakulima nchini na kuzitafutia ufumbuzi.
“Hii yote inatokana na kasi ya Serikali
ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli inayowataka viongozi
kufuatilia changamoto za wananchi kwa vitendo na kuzitatua.”
Alisema katika ghala la chama chao kuna
jumla ya kilo 175,235 za pamba ambazo zimekusanywa kutoka kwa wakulima ikiwa
inasubiri wanunuzi.
0 comments:
Post a Comment