Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa ufunguzi wa
Mkutano wa wadau wa Elimu ya Ualimu kuhusu usimamizi na uendeshaji bora
wa Elimu ya Ualimu uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Wadau wa Elimu ya Ualimu wakifuatilia
hotuba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt.
Leonard Akwilapo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau hao uliofanyika
jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya
Ualimu Augusta Lupokela akizungumza wakati wa Mkutano wa Wadau wa Elimu
ya Ualimu ambapo amesema matokeo ya Mkutano huo yatasaidia katika
maandalizi ya mpango mkakati wa maboresho ya usimamizi wa mafunzo ya
ualimu.
Wadau wa Elimu ya Ualimu wakiwa
wameshikana mkono huku wakiimba wimbo wa “solidarity” kuashiria umoja
katika utekelezaji wa majukumu ili kufikia malengo mapana ya kutoa elimu
iliyo bora.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akiwa katika picha ya pamoja na wadau
wa mkutano wa wadau wa elimu ya ualimu baada ya kufungua mkutano huo
jijini Dar es Salaam.
………………………
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania inakusudia kufanya maboresho ya mtaala
wa elimu ya ualimu ili iendane na mitaala mipya ya elimu ya Sekondari
na msingi ambayo imeanza kutumika mwaka 2015.
Hayo yamesemwa Jijni Dar es Salaam na
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo wakati wa ufunguzi wa
mkutano wa wadau wa Elimu ya Ualimu ambao wamekutana kwa lengo la kutoa
maoni yatakayosaidia kuboresha usimamizi na maendeleo hususan maboresho
ya mtaala wa elimu ya ualimu.
Dkt.Akwilapo alisema mtaala wa mafunzo ya
ualimu uliopo sasa ni wa zamani akitolea mfano mtaala wa mafunzo ya
ualimu kwa walimu wa diploma ambao ni wa mwaka 2008 huku ngazi ya cheti
ukiwa wa mwaka 2009 hivyo kutoendana na mtaala mpya wa elimu msingi
ambao unazingatia ufundishaji wa KKK.
“Elimu ni suala la Kitaifa hivyo serikali
haiwezi kujifanya haisikii jamii inasema nini ndio maana kikao cha
wadau kimeitishwa na pia Waziri wa elimu yupo mbioni kuitisha mkutano wa
wadau kwa lengo la kupata maoni ya namna bora ya kuboresha
Elimu,”aliongeza Dkt Akwilapo.
Aidha Katibu Mkuu huyo amewataka wadau
hao kutumia mkutano huo kujadili na kutafakari kwa kina mfumo wa
maandalizi ya walimu nchini kwa kuzingatia mada ya Usimamizi na
Maendeleo ya Elimu ya Ualimu, Fursa na Changamoto pamoja na upimaji na
tathmini yake.
“Tumieni mkutano huu vizuri na mambo
mtayakojadili yajikite katika kuona ni namna gani mnaboresha mahiri
zinazohitajika kwa mwalimu, ama mkufunzi, mazingira na miundombinu
wezeshi, uongozi na usimamizi wa mafunzo, upimaji na tathmini ya mafunzo
pamoja na maendeleo endelevu ya mwalimu,” alisisitiza Dkt Akwilapo.
Akizungumza katika Mkutano huo Kamishna
wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema mkutano huo wa wadau wa elimu
utachochea mabadiliko katika sekta nzima ya elimu kwani ili kufanikiwa
katika sekta hiyo ni lazima kuwe na ushirikishwaji wa wadau wa elimu.
“Tumekutana kwa ajili ya kuongelea moyo
wa Taifa letu, Elimu ni moyo wa taifa unaposema elimu unapozungumzia
elimu ya ualimu katika kuleta mabadiliko ya sekta nzima ya elimu,”
aliongeza Dkt Mtahabwa.
Dkt Mtahabwa anasema unaweza kujenga
shule nyingi, ukawa na vifaa vya kutosha lakini kama hauna walimu bora
ni kazi bure hivyo tunataka walimu wawe na waledi, wawe kioo cha jamii
kuanzia uvaaji wake, kutembea, kuongea na namna anaivyoishi shuleni na
hata kijijini awe mfano wa kuigwa katika jamii.
Awali Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa
Mafunzo ya Ualimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Augusta
Lupokela alimweleza Katibu Mkuu kuwa mkutano huo, pamoja na mambo
mengine umelenga kujadili masula yanayohusu usimamizi wa mafunzo ya
ualimu na kwamba mada zitakazowasilishwa zitahusu usimamizi na maendeleo
ya Elimu ya ualimu, fursa zilizopo pamoja na changamoto.
Aliongeza kuwa matokeo ya mkutano huo ni
maandalizi ya mpango mkakati wa maboresho ya usimamizi wa mafunzo ya
ualimu ili kufikia malengo ya serikali ya kutoa elimu bora ya ualimu.
Nae Mratibu wa mradi wa Elimu kwa Walimu
(TESP) Ignasi Chonya amesema kupitia mradi anaousimamia wamekuwa wakitoa
mafunzo kwa walimu kazini na walimu tarajali kuhusu matumzi ya TEHAMA,
ualimu kwa vitendo kwa vyuo vyote vya Serikali na binafsi ili kuwajengea
uwezo wa namna ya kufundisha kwa vitendo.
Mkutano wa wadau wa Elimu ya Ualimu
unafanyika kwa siku tatu kuanzia Agosti 08, 2019 na umehusisha wadau
kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na
Taasisi zake, Viongozi na Mameneja wa shule, vyuo vya ualimu kutoka
sekta binafsi, Washirika wa Maendeleo na Wizara ya Elimu.
0 comments:
Post a Comment