Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, bunge, kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu)
Mhe.Jenista Mhagama akitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa warsha ya
siku moja ya majadiliano ya wadau kuhusu ushiriki wa Watanzania katika
miradi ya kimkakati (Local content) katika sekta ya uziduaji mkoani
Dodoma iliyofanyika tarehe 26 Agosti, 2019.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, bunge, kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu)
Mhe.Jenista Mhagama akisalimiana na mmoja wa washiriki wa warsha hiyo
Bi. Mariagorete Charles mara baada ya ufunguzi wa warsha hiyo Agosti 26,
2019.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia sera, bunge, kazi, vijana, ajira na watu wenye
ulemavu Mhe.Jenista Mhagama akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.
Dkt. Bilinith Mahenge
mara baada ya kufungua warsha ya majadiliano ya wadau kuhusu ushiriki
wa Watanzania katika miradi ya kimkakati (Local content) katika sekta ya
uziduaji mkoani Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt.
Bilinith Mahenge pamoja na sehemu ya washiriki wa warsha hiyo
wakifuatilia mada kutoka kwa mwezeshaji Bi. Mariagorete Charles kutoka
katika mradi wa EACOP (hayupo pichani) wakati wa warsha hiyo.
Sehemu ya washiriki wa warsha
hiyo wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, bunge,
kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama (hayupo
pichani) alipokuwa akitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo.
Mwasilishaji wa mada kuhusu mradi
ya bomba la mafuta – EACOP Bi. Mariagorete Charles akiwasilisha mada
wakati wa warsha hiyo kwa washiriki wa warsha iliyofanyika Agosti 26,
2019 Jijini Dodoma.
*****************
NA.MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye
Ulemavu Mhe.Jenista Mhagama amefungua warsha ya siku moja ya majadiliano
ya wadau kuhusu ushiriki wa Watanzania (Local content) katika sekta ya
uziduaji mkoani Dodoma.
Warsha hiyo imewakutanisha pamoja
wawakilishi zaidi ya 100 wa makundi mbalimbali kutoka Wilaya zote za
Mkoa wa Dodoma ili kujadili mikakati na maendeleo ya utekelezaji wa
dhana ya ushiriki wa Watanzania katika fursa za miradi ya kimkakati
ikiwemo mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP)
kutoka Hoima nchini Uganda kwenda Tanga, Tanzania na sekta ya madini kwa
ujumla.
Akizungumza wakati wa kufungua
warsha hiyo leo Agosti 26, 2019 katika ukumbi wa Kilimanjaro Hazina
Mjini Dodoma Waziri Mhagama aliwataka viongozi wa maeneo ambako bomba
litapita wawahamasishe wananchi kuchangamkia fursa zitakazokuwepo katika
utekelezaji wa mradi huo na kujiletea maendeleo.
“Ni wakati sahihi sasa kuitumia
fursa hii ya miradi mikubwa ambayo inalenga kunufaisha wananchi kwa
kuzingatia kuwa ajira zitazalishwa kwa wazawa hivyo mjiandaae kikamilifu
katika kuupokea mradi huu,” alieleza Mhagama.
Waziri Mhagama aliongezea kuwa,
Sheria ya Mafuta imeweka wazi kwamba watanzania na kampuni za kitanzania
zinatakiwa zipewe kipaumbele wakati wa ununuzi. Serikali inaamini
kwamba Sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa nchi.
Hivyo ni matarajio kwamba Mkandarasi wa mradi atazingatia matakwa ya
Sheria hii na pale ambapo kampuni za kitanzania hazina uwezo basi
ziingie ubia na kampuni za nje ili kuongeza ujuzi wa uzalishaji na
utoaji wa huduma.
Alifafanua kuwa, kwa kuzingatia
dhamira ya Serikali ya awamu ya Tano kuona Watanzania wanamiliki uchumi
wao, hivyo wataendelea kuwahamasisha watanzania kushiriki katika miradi
Mikubwa ya kimkakati na katika miradi mbalimbali.
“Serikali kupitia Baraza la Taifa
la Uwezeshaji Wananchu Kiuchumi imejipanga kuweka mazingira wezeshi kwa
watanzania ikiwa ni pamoja na kutengeneza Sera na Sheria na miongozo
inayotoa kipaumbele kwa watanzania kupata fursa za ajira, kushiriki kwa
kutoa huduma, uuzaji wa bidhaa na utoaji wa huduma kwenye miradi
inayotekelezwa hapa nchini hasa katika sekta ya uziduaji,”alisisitiza
Mhagama.
Mradi wa EACOP ni moja kati ya
miradi mikubwa ambao una manufaa mengi kwa nchi yetu na kueleza kuwa,
bomba hili la mafuta ghafi litakuwa na urefu wa km 1443 kati ya hizo km
296 zitakuwa nchini Uganda na km 1147 zitakuwa Tanzania. Hii ni fursa
kubwa kwa watanzania kwa kuwa 80% ya mradi huu utapita Tanzania.
Aidha alibainisha mikoa
itakayopitiwa na mradi huo ikiwemo Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora,
Singida, Dodoma, Manyara na Tanga na kufafanua kuwa bomba hilo litapita
katika wilaya 24, Kata 134 na vijiji zaidi ya 180 na kutoa wito kwa
wananchi kujiandaa na kuhakikisha wanaandaa mazingira wezeshi katika
kushiriki fursa zitakazotokana na uwepo wa mradi huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma Mhe. Dkt. Bilinith Mahenge alipongeza jitihada zinazoendelea
katika kuhamasisha na kutoa elimu kwa jamii juu ya ushiriki wa Watanzaia
katika fursa ya mradi bomba la mafuta na kuahidi kuzimamia kikamilifu
ili kuhakikisha jamii inashiriki kwa uhakika.
“Kipekee ninapongeza juhudi
zinazoendelea katika kuhakikisha wananchi wanajikwamua kiuchumi kwa
kuzingatia ujio wa miradi hii ya kimkakati nchini hivyo hatuna budi
kuendelea kutoa rai kwa Watanzania wote kuchangamkia fursa hizi,”alisema
Dkt. Mahenge.
0 comments:
Post a Comment