WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani
Jafo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo ofisini
kwake wakati akitoa taarifa ya mapato na matumizi ya Fedha za vyanzo vya
ndani vya Halmashauri kwa mwaka wa Fedha 2018/19
………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo ametoa
wiki mbili kwa halmashauri zote zilizokusanya mapato chini ya asilimia
50 ya malengo yao kuandika barua ya kujieleza kwa Katibu Mkuu TAMISEMI
ya kwanini wasichukuliwe hatua kwa kutofikia malengo.
Pia amesema Wakurugenzi
walioshindwa kukusanya mapato watapewa vinyago vya uzembe na kutofikia
lengo kisha kutakiwa kuviweka mbele ya ofisi zao na za wakuu wa mikoa
hiyo.
Amebainisha kuwa agizo hilo
pia limewahusu wakurugenzi kutoka halmashauri zaidi ya 40 walioshindwa
kutoa fedha za mikopo kwa kwa makundi ya vijana, walemavu na wanawake
chini ya asilimia 50 zilizotakiwa kutengwa.
Hayo ameyabainisha Jijini
Dodoma wakati akizungumza na wanahabari, Waziri Jafo amezitaja
halmashauri ambazo wakurugenzi wake watapewa vinyago kwa kushindwa
kukusanya mapato.
“Vinyago nitakavyovitoa
vitakuwa na sura mbaya sana na Wakurugenzi wa halmashauri hizo
wanatakiwa kuviweka kwenye ofisi zao na ofisi za wakuu wa mikoa husika,”
amesema.
“Halmashauri ambazo zitahusika
zilizoshika mkia kwa kigezo cha wingi wa mapato yaliyokusanywa (pato
ghafi) ni Halmashauri za Wilaya za Kakonko (Sh. milioni 408.2), Buhigwe
(Sh. milioni 403.8), Kigoma (Sh. milioni 397.1), Gairo (Sh.milioni
396.2) na Halmashauri ya Mji wa Nanyamba (Sh. Milioni 257.6)” amesema.
Amezitaja halmashauri za mwisho
kwa kigezo cha asilimia ya mapato ya ndani yaliyokusanywa ukilinganisha
na makisio ya halmashauri ya mwaka ni Halmashauri za Wilaya za Newala
(27%), Masasi (26%), Msalala (19%), Tandahimba (19%) na Halmashauri ya
Mji wa Nanyamba (11%).
Pia amebainisha kuwa kuna uwepo wa
Halmashauri zaidi ya 40 ambazo zimeshindwa kuchangia katika Vikundi vya
Wanawake, Vijana, na Watu wenye Ulemavu.
“Nataka na hawa nao wajieleze
sababu za kushindwa kusimamia Kanuni za Usimamizi wa Fedha za michango
ya Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu,” amesema.
Waziri Jafo amezitaja halmashauri
tano zilizoongoza kwa kigezo cha wingi wa mapato yaliyokusanywa (pato
ghafi), Jiji la Dodoma limeongoza kwa kukusanya sh. bilioni 71.7,
Halmashauri za Manispaa za Ilala sh. bilioni 58.2, Kinondoni (Sh.Bilioni
34.0), Temeke (Sh. Bilioni 33.3) na Ubungo (Sh. Bilioni 18.6).
“Mikoa iliyoongoza ni Dar es
Salaam (Sh. Bilioni 163.6), Dodoma (Sh. Bilioni 82.7), Mwanza (Sh.
Bilioni 32.7), Arusha (Sh. Bilioni 31.9) na Mbeya (Sh. Bilioni 31.4)”
amesema Jafo.
Ameitaja mikoa mitano ya mwisho
kwa kigezo cha wingi wa mapato yaliyokusanywa (pato ghafi) ni Njombe
(Sh. Bilioni 11.5), Simiyu (Sh. Bilioni 8.8), Rukwa (Sh. Bilioni 8.2),
Kigoma (Sh. Bilioni 7.8) na Katavi (Sh. Bilioni 7.4).
0 comments:
Post a Comment