
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo amewataka wananchi wa mkoa huo kushiriki katika zoezi la
kuchangia damu litakalofanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 14
hadi 18.8.2019 katika halmashauri nne za mkoa, ili kusaidia majeruhi
walioungua na moto uliosababishwa na kulipuka kwa lori la Mafuta katika
ajali iliyotokea eneo la Msavu mkoani Morogoro, na kusababisha vifo vya
watu 76 na majeruhi 54.
Mh. Wangabo amesema kuwa zoezi
hilo litawajumuisha Waendesha Bodaboda na Bajaji, Madereva wa Magari,
Vijana, Watumishi wa Serikali, Wanafunzi, Vyama za Siasa, Madhehebu ya
Dini, Viongozi mbalimbali na wale wote wenye mapenzi mema na moyo wa
kujitolea kwaajili ya majeruhi hao.
“Nafahamu kuwa mtu yeyote
aliyeungua sehemu yoyote ya mwili, miongoni mwa madhara makubwa
anayoyapata ni pamoja na kupoteza kiasi kikubwa cha maji mwilini
(Dehydration) na kupungukiwa damu mwilini (Anaemia). Kwa hiyo natoa
wito na kuwaomba Wananchi wa Mkoa wa Rukwa kuchangia Damu kwa ajili ya
wenzetu majeruhi wanaoendelea na matibabu. Damu hiyo pamoja na salamu
zetu za pole tutaiwasilisha kwa Dkt. Kebwe Steven Kebwe, Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro,” Alisema.
Aidha Mh. Wangabo kwa niaba ya
Wananchi wa Mkoa wa Rukwa anaungana na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa pole kwa Mkuu wa
Mkoa wa Morogoro pamoja na Viongozi wa Mkoa huo, Familia za Marehemu,
Ndugu, Jamaa na Marafiki kwa kuondokewa na Wapendwa wao. Na kumuomba
Mwenyezi Mungu awape Moyo wa Subira na Uvumilivu katika kipindi hiki
kigumu.
“Mungu awape pumziko la milele
waliopoteza uhai na awaponye Majeruhi wote wanaoendelea na matibabu
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili pamoja na hospitali ya Rufaa Mkoa
wa Morogoro. ‘Bwana Alitoa na Bwana Alitwaa Jina lake lihimidiwe’.”
Alimalizia.
Mh. Wangabo ametoa maelekezo
hayo kabla ya kuanza kwa kikao cha baraza la madiwani katika Halmashauri
ya Manispaa ya Sumbawanga kilichohusu utekelezaji wa hoja za ukaguzi na
mapendekezo ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali nchini.
0 comments:
Post a Comment