Rais wa Namibia Hage Geingob
na Mwenyekiti wa zamani wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi Kusini mwa
Afrika (SADC) akimkabidhi uenyekiti Rais wa Jamhuri ya Muungano ya
Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za SADC
kwenye mkutano ulioanza leo katika ukumbi wa Julius Nyerere leo
Jumamosi Agosti 17, 2019 jijini Dar es salaam, kulia ni Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Mawaziri wa SADC na kushoto ni Katibu Mtendaji Mkuu wa SADC,Dr. Stergomena L. Tax.
Rais wa Namibia Hage Geingob
na Mwenyekiti aliyemaliza muda wake wa oungozi wa Jumuiya ya Maendeleo
ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika (SADC) akimpongeza Rais wa Jamhuri ya
Muungano ya Tanzania Dk. John Pombe Magufuli baada ya kumkabidhi
uenyekiti kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za SADC ulioanza leo katika
ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Jumamosi Agosti 17,
2019 kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa SADC na kushoto ni Katibu Mtendaji Mkuu wa SADC,Dr. Stergomena L. Tax.
(PICHA NA JOHN BUKUKU-FULLSHANGWEBLOG)
………………………………………………………..
NA JOHN BUKUKU
MWENYEKITI mpya wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ambaye pia ni Rais wa Tanzania, Dk.
John Magufuli amesema nchi za kiafrika si maasikini hivyo ziache
kujitangaza kuwa ni duni mbele ya mataifa mengine.
“Tusikubali kusafirisha tu
malighafi nje ya Afrika, hii inaatufanya tuwe tunasafirisha ajira. Nchi
zetu si masikini, narudia tena nchi zetu si masikini tunao utajiri wa
kutosha kwenye madini, mafuta na ardhi yenye rutuba. Vitu vyote
vinavyotufanya tuwe matajiri tunavyo, kwanini tushindwe kupiga hatua,”
alisema Rais Magufuli.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa
uenyekiti wa jumuiya hiyo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam leo, Rais Magufuli amesema
mbali ya kuwa na rasilimali nyingi lakini bado Afrika inalalamika hali
duni ya kiuchumi.
Rais Magufuli amesema Tunaagiza
sukari, magari na mafuta katika nchi za mbali huku tukijua baadhi ya
mataifa ya SADC yanaweza kuuza bidhaa hizo kwa bei nafuu. Ndio maana
katika mwaka wangu wa uongozi nimeamua kuongozwa na kaulimbiu ya
mazingira bora ya viwanda, ufanyaji biashara na kutengeneza ajira.
Vievile, fursa nyingi za
kibiashara zinapelekwa katika mataifa ya mbali huku baadhi ya nchi
zinazozalisha bidhaa nzuri ikiwemo magari na bidhaa nyingine za viwanda
zikiachwa mbali ya kuwa na bidhaa bora na zilizo karibu.
Aidha, Rais Magufuli aliigeukia
Sekretarieti ya SADC na kuitaka ieleze kwanini uchumi katika nchi
wanachama wa jumuiya hiyo unashindwa kufikia viwango vya kukua. Kwanini
kwa miaka 10 lengo la kuondokana na tatizo la kiuchumi halijafikiwa.
Awali Rais Magufuli akielezea
changamoto zinazoikabili jumuiya hiyo na kushindwa kufikia baadhi ya
makubaliano, Rais Magufuli alisema changamoto ya kwanza ni vurugu za
kisiasa, kutokamilika ahadi za kubadili uchumi na ukosefu wa taarifa za
fursa katika nchi wanachama.
“Bado hatujafanikiwa katika
ukuaji wa uchumi, niseme kweli bado tunasuasua. Na tusipibadilika
hatutaweza kufanikiwa katu. Bado tupo nyuma katika lengo letu la
kiuchumi, uhaba wa taarifa unasababisha tunashindwa kujua wapi pa kuuza
bidhaa zetu,” alisema Rais Magufuli.
Naye Mwenyekiti aliyemaliza muda
wake ambaye pia ni Rais wa Namibia, Dk. Hage Geingob alisema katika vitu
alivyovutiwa katika mkutano huu wa kawaida wa 39 ni namna viongozi
wastaafu walivyohudhuria wote na kuonyesha mshikamano.
“Mmeonyesha mfano mzuri kwa nchi
za kiafrika, hii ndiyo Afrika tunayoitaka kuona viongozi wanaachia
madaraka kwa mujibu wa katiba na wote wanakuwa na maelewano. Ninamuona
rais wa awau ya pili, ya tatu na ya nne. Huu ni utekelezaji mzuri maneno
ya Mwalimu Julius Nyerere,” alisema Dk. Geingob.
Katika hotuba yake ya kukabidhi
uongozi alisema, Jiji la Dar es Salaam litabaki kuwa eneo la kihistoria
kutokana na kuwa kitovu cha vuguvugu la harakati za ukombozi kwa nchi za
kusini mwa Afrika.
Alisema, anayo furaha kuachiaa
madaraka wakati nchi tano zilizo ndani ya SADC zilifanya uchaguzi huru
na wa haki ukiofuata vigezo vyote vya jumuiya hiyo ndani ya kipindi
chake.
“Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC), kwa mara ya kwanza imefanya uchaguzi huru na wa haki tangu ipate
uhuru miaka ya 1960, katika kipindi cha uongozi wangu nimeshuhudia
mabadiliko ya kiuongozi katika nchi hiyo.
“Tukisema tunataka kufanikiwa
kiuchumi lazima tuhakikishe tunaondokana na vurugu za kisiasa, ulinzi na
amani ndiyo kitu cha kwanza katika kupata maendeleo,” alisema na
kubainisha bado kunahitajika huduma muhimu katika jumuiya hiyo ikiwemo
maji safi na salama.
Alisisitiza, vijaana wanahitaji
kupewa kipaumbele katika maendeleo kwa kuwa wao ndio nguvu kazi. Pia
aligusia suala la mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha uhaba wa
chakula na vimbunga vilivyoharibu miundombinu kutokana na mvua kubwa
zilizonyesha kwenye baadhi ya nchi wanachama.
“Kujumuisha vijana katika
utungwaji wa sera na kuhuisha ufanyaji biashara baina ya nchi wanachama
ni baadi ya changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa haraka. Usafirishaji
bidhaa katika mipaka ya nchi wanachama pia ni tatizo linalohitaji
ufumbuzi wa haraka,” alisema Dk. Geingob.
Katibu Mtendaji wa SADC, Dk.
Stergomena Tax alisema kwa muda wa mwaka mmoja uliopita Tanzania ndiyo
iliyoonyesha mfano mzuri katika ukuaji uchumi na kufikia malengo ya
kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.
Alisema, ukuaji wa uchumi kwa
asilimia 7 umeonyesha mfano mzuri wakati baadhi ya nchi wanachama ukuaji
wake uchumi ulikuwa chini ya asiimia tatu. Alisema, wameonyesha mfano
mzuri kwa kutoa misaada ya kiutu wakati baadhi ya nchi wanachama
ziipokumbwa na majanga ya kimbunga ikiwemo Zimbabwe na Msumbiji.
Ameongeza kuwa “Tunavutiwa na
kasi ya ajabu ya ujenzi wa miundombinu hasa miundmbinu ya nishati, kwa
mfano hivi karibuni Tanzania imeonyesha mfano kwa kuanza mradai wa kufua
umeme wa Nyerere HP katika Mto Rufiji. Mradi huu ukikamilika utazalisha
Megawati 2,115 za umeme ambapo ni miongoni mwa mikakati ya SADC
kuhuisha ukuaji wa uchumi kwa kuweka uhakika wa upatikanaji umeme kwa
nchi wanachama,” alisema Dk. Tax.
Rais wa Namibia Hage Geingob
na Mwenyekiti wa wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika
(SADC) aliyemaliza muda wake akihutubia kwenye mkutano wa wakuu wa nchi
za SADC katika mkutano ulioanza leo ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar
es salaam leo Jumamosi Agosti 17, 2019.
Rais wa Jamhuri ya Muungano ya
Tanzania na Mwenyekiti mpya wa SADC Dk. John Pombe Magufuli akipongezwa
na baadhi ya Wakuu wa nchi mbalimbali za Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC).
Wakuu wa nchi za Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC wakiwa katika picha ya pamoja mara
baada ya mkutano huo kumalizika siku ya leo.
Mabalozi na wageni waalikwa
mbalimbali wakiwa kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Kiuchumi
Kusini mwa Afrika SADC uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Julius Nyerere
jijini Dar es salaam.
Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiwa katika mkutano huo.
Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya
Maendeleo ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika (SADC) Rais wa Jamhuri ya
Muungano ya Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akizungumza kwenye mkutano
wa wakuu wa nchi za SADC kwenye mkutano ulioanza leo katika ukumbi wa
Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa SADC
Rais Dkt.Hage Geingob wa Namibia akipongezana na Katibu Mtendaji Mkuu wa
SADC,Dr. Stergomena L. Tax mara baada ya kukabidhi uenyekiti kwa
mwenyekiti mpya wa SADC Rais Dk. John Pombe Magufuli wa tatu kutoka
kulia.
Katibu Mtendaji Mkuu wa SADC,Dr. Stergomena L. Tax akitoa salamu zake kwa wakuu wa nchi za SADC wakati wa mkutano huo.
Baadhi ya wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC wakiwa katika mkutano huo.
Baadhi ya wajumbe mbalimbali wakiwa katika mkutano huo.
Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC wakiwa katika mkutano huo.
Baadhi ya maofisa na waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
0 comments:
Post a Comment