Saturday, August 17, 2019

RAIS DK. JOHN POMBE MAGUFULI AKABIDHIWA UENYEKITI WA SADC, ATEMA CHECHE NCHI ZA AFRIKA SIYO MASIKINI

Rais wa Namibia Hage Geingob na Mwenyekiti wa zamani wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika (SADC) akimkabidhi uenyekiti Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za SADC kwenye mkutano ulioanza leo katika ukumbi wa Julius Nyerere  leo Jumamosi Agosti 17, 2019 jijini Dar es salaam, kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa SADC na kushoto ni Katibu Mtendaji Mkuu wa SADC,Dr. Stergomena L. Tax.
Rais wa Namibia Hage Geingob na Mwenyekiti aliyemaliza muda wake wa oungozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika (SADC) akimpongeza  Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dk. John Pombe Magufuli baada ya kumkabidhi uenyekiti kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za SADC  ulioanza leo katika ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Jumamosi Agosti 17, 2019  kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa SADC na kushoto ni Katibu Mtendaji Mkuu wa SADC,Dr. Stergomena L. Tax.
(PICHA NA JOHN BUKUKU-FULLSHANGWEBLOG)
………………………………………………………..
NA JOHN BUKUKU
MWENYEKITI mpya wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ambaye pia ni Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli amesema nchi za kiafrika si maasikini hivyo ziache kujitangaza kuwa ni duni mbele ya mataifa mengine.
“Tusikubali kusafirisha tu malighafi nje ya Afrika, hii inaatufanya tuwe tunasafirisha ajira. Nchi zetu si masikini, narudia tena nchi zetu si masikini tunao utajiri wa kutosha kwenye madini, mafuta na ardhi yenye rutuba. Vitu vyote vinavyotufanya tuwe matajiri tunavyo, kwanini tushindwe kupiga hatua,” alisema Rais Magufuli.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa jumuiya hiyo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam leo, Rais Magufuli amesema mbali ya kuwa na rasilimali nyingi lakini bado Afrika inalalamika hali duni ya kiuchumi.
Rais Magufuli amesema Tunaagiza sukari, magari na mafuta katika nchi za mbali huku tukijua baadhi ya mataifa ya SADC yanaweza kuuza bidhaa hizo kwa bei nafuu. Ndio maana katika mwaka wangu wa uongozi nimeamua kuongozwa na kaulimbiu ya mazingira bora ya viwanda, ufanyaji biashara na kutengeneza ajira.
Vievile, fursa nyingi za kibiashara zinapelekwa katika mataifa ya mbali huku baadhi ya nchi zinazozalisha bidhaa nzuri ikiwemo magari na bidhaa nyingine za viwanda zikiachwa mbali ya kuwa na bidhaa bora na zilizo karibu.
Aidha, Rais Magufuli aliigeukia Sekretarieti ya SADC na kuitaka ieleze kwanini uchumi katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo unashindwa kufikia viwango vya kukua. Kwanini kwa miaka 10 lengo la kuondokana na tatizo la kiuchumi halijafikiwa.
Awali Rais Magufuli  akielezea changamoto zinazoikabili jumuiya hiyo na kushindwa kufikia baadhi ya makubaliano, Rais Magufuli alisema changamoto ya kwanza ni vurugu za kisiasa, kutokamilika ahadi za kubadili uchumi na ukosefu wa taarifa za fursa katika nchi wanachama.
“Bado hatujafanikiwa katika ukuaji wa uchumi, niseme kweli bado tunasuasua. Na tusipibadilika hatutaweza kufanikiwa katu. Bado tupo nyuma katika lengo letu la kiuchumi, uhaba wa taarifa unasababisha tunashindwa kujua wapi pa kuuza bidhaa zetu,” alisema Rais Magufuli.
Naye Mwenyekiti aliyemaliza muda wake ambaye pia ni Rais wa Namibia, Dk. Hage Geingob alisema katika vitu alivyovutiwa katika mkutano huu wa kawaida wa 39 ni namna viongozi wastaafu walivyohudhuria wote na kuonyesha mshikamano.
“Mmeonyesha mfano mzuri kwa nchi za kiafrika, hii ndiyo Afrika tunayoitaka kuona viongozi wanaachia madaraka kwa mujibu wa katiba na wote wanakuwa na maelewano. Ninamuona rais wa awau ya pili, ya tatu na ya nne. Huu ni utekelezaji mzuri maneno ya Mwalimu Julius Nyerere,” alisema Dk. Geingob.
Katika hotuba yake ya kukabidhi uongozi alisema, Jiji la Dar es Salaam litabaki kuwa eneo la kihistoria kutokana na kuwa kitovu cha vuguvugu la harakati za ukombozi kwa nchi za kusini mwa Afrika.
Alisema, anayo furaha kuachiaa madaraka wakati nchi tano zilizo ndani ya SADC zilifanya uchaguzi huru na wa haki ukiofuata vigezo vyote vya jumuiya hiyo ndani ya kipindi chake.
“Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwa mara ya kwanza imefanya uchaguzi huru na wa haki tangu ipate uhuru miaka ya 1960, katika kipindi cha uongozi wangu nimeshuhudia mabadiliko ya kiuongozi katika nchi hiyo.
“Tukisema tunataka kufanikiwa kiuchumi lazima tuhakikishe tunaondokana na vurugu za kisiasa, ulinzi na amani ndiyo kitu cha kwanza katika kupata maendeleo,” alisema na kubainisha bado kunahitajika huduma muhimu katika jumuiya hiyo ikiwemo maji safi na salama.
Alisisitiza, vijaana wanahitaji kupewa kipaumbele katika maendeleo kwa kuwa wao ndio nguvu kazi. Pia aligusia suala la mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha uhaba wa chakula na vimbunga vilivyoharibu miundombinu kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kwenye baadhi ya nchi wanachama.
“Kujumuisha vijana katika utungwaji wa sera na kuhuisha ufanyaji biashara baina ya nchi wanachama ni baadi ya changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa haraka. Usafirishaji bidhaa katika mipaka ya nchi wanachama pia ni tatizo linalohitaji ufumbuzi wa haraka,” alisema Dk. Geingob.
Katibu Mtendaji wa SADC, Dk. Stergomena Tax alisema kwa muda wa mwaka mmoja uliopita Tanzania ndiyo iliyoonyesha mfano mzuri katika ukuaji uchumi na kufikia malengo ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.
Alisema, ukuaji wa uchumi kwa asilimia 7 umeonyesha mfano mzuri wakati baadhi ya nchi wanachama ukuaji wake uchumi ulikuwa chini ya asiimia tatu. Alisema, wameonyesha mfano mzuri kwa kutoa misaada ya kiutu wakati baadhi ya nchi wanachama ziipokumbwa na majanga ya kimbunga ikiwemo Zimbabwe na Msumbiji.
 Ameongeza kuwa “Tunavutiwa na kasi ya ajabu ya ujenzi wa miundombinu hasa miundmbinu ya nishati, kwa mfano hivi karibuni Tanzania imeonyesha mfano kwa kuanza mradai wa kufua umeme wa Nyerere HP katika Mto Rufiji. Mradi huu ukikamilika utazalisha Megawati 2,115 za umeme ambapo ni miongoni mwa mikakati ya SADC kuhuisha ukuaji wa uchumi kwa kuweka uhakika wa upatikanaji umeme kwa nchi wanachama,” alisema Dk. Tax.
Rais wa Namibia Hage Geingob na Mwenyekiti wa wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika (SADC) aliyemaliza muda wake akihutubia kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za SADC katika mkutano ulioanza leo  ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Jumamosi Agosti 17, 2019.
Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Mwenyekiti mpya wa SADC Dk. John Pombe Magufuli akipongezwa na baadhi ya  Wakuu wa nchi mbalimbali za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mkutano huo kumalizika siku ya leo.
Mabalozi na wageni waalikwa mbalimbali wakiwa kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika SADC uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiwa katika mkutano huo.
Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika (SADC) Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akizungumza kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za SADC kwenye mkutano ulioanza leo katika ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa SADC Rais Dkt.Hage Geingob wa Namibia akipongezana na Katibu Mtendaji Mkuu wa SADC,Dr. Stergomena L. Tax mara baada ya kukabidhi uenyekiti kwa mwenyekiti mpya wa SADC Rais Dk. John Pombe Magufuli wa tatu kutoka kulia.
Katibu Mtendaji Mkuu wa SADC,Dr. Stergomena L. Tax akitoa salamu zake kwa wakuu wa nchi za SADC wakati wa mkutano huo.
Baadhi ya wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC wakiwa katika mkutano huo.
Baadhi ya wajumbe mbalimbali wakiwa katika mkutano huo.
Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC wakiwa katika mkutano huo.
Baadhi ya maofisa na waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.

No comments:

Post a Comment