Serikali imetoa zaidi ya shilingi
milioni 969 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya shule kongwe ya
sekondari Galanos iliyopo mkoani Tanga.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknlolojia William Ole Nasha alipotembelea shule hiyo
kukagua maendeleo ya ukarabati wa miundombinu ambapo amesema fedha hizo
zimetolewa kupitia mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) katika
mpango unaolenga kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika
shule hiyo kongwe.
Ole Nasha amesema fedha hizo ni
sehemu ya fedha zilizopelekwa katika shule kongwe nchini ambazo
zinafanyiwa ukarabati mkubwa lengo likiwa ni kuzirudisha katika hadhi
yake ya awali ili ziwe na mazingira mazuri yanayomwezesha mwanafunzi
kujifunza na kufaulu vizuri
Katika hatua nyingine, Naibu
Waziri huyo amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Daudi Mayeji
kufuatilia kwa karibu sababu zilizopelekea kukiukwa kwa masharti ya
mkataba wa muongozo wa ukadiriaji majenzi (BOQ) ambao ulielekeza kuwekwa
chuma katika varanda za madarasa zinazoruhusu hewa na badala yake
yamewekwa matofali ya kuchoma.
“Galanos tumeleta fedha zaidi ya
shilingi milioni 696 kwa ajali ya kukarabati miundombinu, baada ya
kukagua maendeleo ya ukarabati nimegundua kuna mapungufu makubwa ya
kimakusudi, Mfano kwenye madarasa kulitakiwa kuwekwe chuma lakini badala
ya kuweka chuma wameweka matofali ya kuchoma bila hata kufuata taratibu
wa kufanya mabadiliko” amesema Ole Nasha.
Amesema inashangaza kwani Mhandisi
alishiriki katika uandaaji wa BOQ hiyo na ni mmoja wa walioshauri
kuwekwa kwa chuma lakini katika utekelezaji wa BOQ hiyo iliyopitishwa
amebadili maelekezo, hata baada ya kamati ya ujenzi kumkatalia na
kumtaka kufata BOQ inavyotaka lakini bado aliendelea na utaratibu wa
kuweka matofali hayo badala ya chuma.
“Ndio maana nimemwelekeza
Mkurugenzi wa Jiji afuatilie kwanini kuna ukiukwaji wa makusudi wa
kuacha kufuata BOQ na nimemwelekeza achukue hatua kwa yeyote anayehusika
kubadilisha maelekezo ya BOQ” amesisitiza Ole Nasha
Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Daudi
Mayeji ameahidi kufatilia suala hilo la uwekwaji wa matofali badala ya
chuma na kwamba atachukua hatua kwa wale wote waliohusika katika
kubadili maelekezo yaliyopo katika mkataba wa ukadiriaji majenzi (BOQ).
0 comments:
Post a Comment