Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia
wananchi wakati alipotembelea maonyesho ya Nanenane yaliyofanyika
kitaifa kwenye viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu, Agosti 8, 2019.
Kulia ni Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, kushoto kwa Waziri Mkuu ni
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Tellak na kulia kwa Waziri Mkuu ni
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisaidiana
na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga (kulia) na Mkuu wa mkoa wa Simiyu,
Anthony Mtaka wa nne kulia) kupandisha pamba kwenye mzani wa
kielektroniki wakati alipokaguaununuzi wa pamba kwenye Chama cha
Ushirika cha Msingi cha Itemelo, eneo la Dutwa mkoani Simiyu, Agosti 8,
2019. Wa tatu kulia ni Katibu Mkuu wa CCM, Dkt Bashiru Ally.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua
pamba wakati alipotembelea Chama cha Ushirika cha msingi cha Itemelo,
eneo la Dutwa mkoani Simiyu, Agosti 8, 2019. Wa tatu kulia ni Katibu
Mkuu wa CCM, Dkt Bashiru Ally, Wa nne kulia ni Waziri wa Kilimo, Japhet
Hasunga na wa tano kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Japhet Hasunga.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akishuhudia kazi ya kupima pamba kwa njia ya
kielektroniki wakati alipokagua ununuzi wa pamba katika Chama cha
Ushirika cha Msingi cha Itemelo kilichopo eneo la Dutwa mkoani Simiyu,
Agosti 8, 2019 Kulia ni Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga na wa
tatu Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka. (Picha na ofisi ya
Waziri Mkuu)
……………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka
wanunuzi wa zao la pamba katika maeneo mbalimbali nchini wahakikishe
wanaongeza kasi ya ununuzi wa zao hilo ili wakulima waweze kupata fedha
zao kwa wakati.
Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa
Kilimo, Japhet Hasunga pamoja na Manaibu Waziri wake kubaki katika mikoa
yote inayolima zao la pamba hadi wakulima wote watakapolipwa fedha zao
na kuhakikisha pamba yote iliyomo mikononi mwa wakulima inauzwa.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Agosti 8,
2019) wakati alipotembelea Chama cha Msingi cha Itemelo kilichoko eneo
la Dutwa wilayani Bariadi, Simiyu kwa ajili ya kujionea mauzo ya zao la
pamba.
Waziri Mkuu amesema ataendelea kusimamia
mwenendo wa zao hilo kwa ukaribu lengo likiwa kuona wakulima wananufaika
kwa kupata tija. “Ilani ya CCM ya 2015/2020 inasisitiza kilimo na
inataka wakulima wapate masoko ya uhakika na tunalitekeleza jambo hilo
na pamba yote itanunuliwa.”
Amesema Serikali inataka kuona pamba yote
iliyoko kwa wakulima inatoka ili wakulima waweze kulipwa fedha ambazo
zitawawezesha kujikimu kimaisha pamoja na kununua pembejeo kwa ajili ya
maandalizi ya msimu ujao.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka viongozi
wa AMCOS wahakikishe wanawatambua wakulima kwa majina, maeneo
wanayoishi pamoja na ukubwa wa mashamba yao ili waweze kuagiza pembejeo
kulingana na mahitaji halisi.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewasihi
wakulima kufungua akaunti katika taasisi mbalimbali za kifedha lengo
likiwa ni kuhifadhi vizuri fedha wanazozipata kutokana na mauzo ya pamba
ili ziweze kuwasaidia baadaye.
Pia, Waziri Mkuu amewasisitiza wakulima
hao waendelee kutunza vizuri pamba yao na kuipeleka ghalani ikiwa katika
hali nzuri ya usafi na ubora wa hali ya juu, kwani kwa sasa pamba ya
Tanzania inasifika kwa ubora katika soko la dunia.
Kwa upande wa masoko hususan ya pamba,
Waziri Mkuu aliwasisitizia wananchi wa Dutwa na Watanzania kwa ujumla
kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli
inaendelea kuhakikisha uwepo wa masoko ya uhakika wa mazao yote hususan
yale ya kimkakati.
Pia, Waziri Mkuu ameongeza kuwa moja ya
agenda muhimu ya ziara yake ya Kiserikali aliyoifanya nchini Misri mwezi
Julai 2019 ilikuwa ni kutafuta masoko ya uhakika ya mazao ya Tanzania
likiwemo na zao la pamba.
Kwa upande wake, Katibu
Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally alipokaribishwa kuwasalimu wananchi
alimshukuru Waziri Mkuu kwa kutoa msukumo katika ununuzi zao la pamba.
Aidha alimuomba Waziri Mkuu aongeze msukumo zaidi ili wakulima walipwe
fedha zao kwa wakati.
Naye,Waziri wa Kilimo
Hasunga amesema kuwa hali ya malipo kwa wakulima wa zao la pamba kwa
sasa ni ya kuridhisha kwa kuwa wakulima katika maeneo mbalimbali
wameanza kulipwa.
Pia Waziri huyo amemuahidi Waziri Mkuu
kwamba wataendelea kubakia katika mikoa inayolima pamba kwa ajili ya
kufuatilia mwenendo wa mauzo ya pamba ili kuhakikisha wakulima wote
wanalipwa fedha zao kwa wakati.
Kuhusu suala la makato ya fedha za
pembejeo ambazo wakulima wanalalamikia kukatwa kiasi kikubwa kuliko
kiwango halisi wanachostahili, Waziri huyo wa Kilimo amesema
atalishughulikia.
Aidha,Mbunge wa jimbo la
Bariadi, Andrew Chenge amesema amefanya ziara katika kata 20 kati ya 30
kwenye jimbo hilo na changamoto kubwa ya wananchi ni mauzo ya pamba.
“Ujio wa Waziri Mkuu umeleta manufaa kwani wanunuzi wameanza kuja kwa
kasi”.
Mbunge huyo amemuomba Waziri Kuu
awafikishie salamu zao kwa Rais Dkt. John Magufuli kwamba wanamshukuru
kwa namna anavyowajali wakulima mbalimbali nchini wakiwemo na wa zao la
pamba.
Kwa upande wake, Mbunge
wa jimbo la Itilima, Njalu Silanga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni
ya Nsangali ambayo inanunua pamba amemuahidi Waziri Mkuu kwamba ifikapo
kesho (Ijumaa, Agosti 9, 2019) saa nane mchana atakuwa amelipa sh.
milioni 135 zinazohitajika na amcos ya Itemelo ili kulipia deni la pamba
iliyoko ghalani.
Awali, Katibu wa Amcos
ya Itemelo, Lucas Ephraim alimuomba Waziri Mkuu awasaidie kuyahimiza
makampuni mbalimbali yanayonunua yapeleke fedha kwa wakati ili kukidhi
makisio tarajiwa.
Katibu huyo alisema chama chao
kinahudumia vijiji vitano vikiwa na jumla ya wakulima 2,665 wa pamba
wenye jumla ya ekari 9,675. Pia chama chao kinahitaji sh. milioni
135.139 ili kulipia deni la pamba ambayo iko ghalani.
0 comments:
Post a Comment