Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.Jenista Mhagama akihutubia washiriki wa Warsha ya Mafunzo kuhusu Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda kuja Tanga yaliyofanyika katika Ukumbi wa Tanga Beach Resort Machi2, 2019.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.Jenista Mhagama akizungumza na baadhi ya watendaji wa Serikali wakati uzinduzi wa warsha hiyo mkoani Tanga.
Katibu Mtendaji, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi.Beng’i Issa akizungumza jambo wakati wa kikao cha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama pamoja na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Tanga alipokutana nao wakati wa Warsha ya Mafunzo kuhusu Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) Machi 2, 2019.
NA.MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.Jenista Mhagama leo Machi 2, 2019 amefungua warsha ya mafunzo kuhusu Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda kuja Tanga, Tanzania.
Warsha hiyo iliwakutanisha zaidi ya wadau 70 wakiwemo viongozi Waandamizi na Watendaji Wakuu wa Mkoa wa Tanga, Wafanyabiashara wa mkoa huo pamoja na wanahabari na kufanyika katika ukumbi wa Tanga Beach Resort mkoani Tanga.
Akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo ambayo itafanyika kwa muda wa siku mbili (Machi 02 na 03, 2019),Mhagama alisema Serikali inaendelea kuhimiza wananchi kutumia fursa ya mradi huo katika kujiletea maendeleo yao nan chi kwa ujumla.
“Mkutano huu wa leo ni matumaini kuwa, utaleta mageuzi makubwa ya mipango mikakati yetu ili kuangalia fursa za ujio wa mradi huu kwa kuzingatia ni moja kati ya mradi unaotarajiwa kuwa na manufaa mengi kwa nchi katika kuzalisha ajira, kuendeleza urithishaji wa ujuzi na teknolojia pamoja na ubia kati ya makapuni ya Tanzania na wageni,”alisema Mhagama
Waziri aliongezea kuwa, inawapasa wananchi kutumia warsha hiyo kujadili na kuweka mikakati bora ya kuzitumia fursa zitakazotokana na mradi kwa kuzingatia malengo mahususi ikiwemo kujadili maendeleo ya mradi na fursa za ushiriki wa Watanzania katika ujio ya mradi pamoja na kuwa na majadiliano kati ya Sekta Bonafsi ya Umma ili kuchochea maendeleo endelevu ya kiuchumi
Aliongezea kuwa, mradi huo utasaidia jamii kushiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo kwa kuzingatia kuwa, ni zaidi ya robo tatu ya Bomba hili litapita Tanzania na kuwanufaisha wananchi wake.
“Matarajio ni makubwa kwa kuzingatia mradi huu unatarajiwa kupita katika mikoa 8 ikiwemo Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga ambapo litapita katika Wilaya 24, Kata 134 na Vijiji zaidi 180 hivyo hatuna budi kuchangamkia fursa kwa kuongeza jitihada za ongezeko la ushiriki wetu,”alisistiza Mhagama
Naye Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Martine Shiga aliendelea kuhimiza watendaji wake kushiriki kikamilifu katika hatua zote za maandalizi kama Mkoa ili kuona namna bora za kushiriki katika fursa hiyo kubwa ya kujileea maendeleo yao.
Naye Katibu Mtendaji, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi.Beng’I Issa alieleza jitihada za Baraza ikiwemo kuanzishwa kwa kanzi data ya nguvu kazi ambayo inachukua takwimu za wafanyabiashara ili kiuwatambua kwa lengo la kushirikisha katika program na kuona namba bora ya kuwashirikisha katika fursa hizo.
“Niwaombe watanzania kuendelea kujisajili katika kanzi data ya nguvu kazi ili tuweze kuwatambua, uwezo na changamoto zenu na kuwashirikisha katika miradi mbalimbali ukiwemo huu wa bomba la mafuta pamoja na kutatua changamoto hizo,” alisisitiza Beng’i
Warsha ya mafunzo hayo imeratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa ufadhili wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) kupitia BEST Dialogue Tanzania kwa lengo la kuwezesha viongozi na Wafanyabiashara wa Mkoa huo kufahamu maendeleo na fursa zitakazotokana na mradi huo.Bomba hilo la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki lina urefu wa KM 1,443 kati ya hizo KM 296 zipo nchini Uganda na KM 1,147 zipo Tanzania
0 comments:
Post a Comment