Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akiimba pamoja na Kwaya
ya Upendo kutoka Kanisa la Anglikana Musoma katika Siku ya maombi ya Dunia
yaliyofanyika Machi Mosi, 2019 katika Viwanja vya Parokia ya Yohana Mbatizaji
Nyamiongo Musoma kwa kujumuisha wanawake wa madhehebu ya Jumuiya ya Kikristo
Tanzania(CCT) na Wanawake WaKatoliki Tanzania(WAWATA) .
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kushoto) na Askofu
Jimbo Katoliki la Musoma Mhashamu Michael Msongazila wakifurahia jambo katika
Siku ya maombi ya Dunia yaliyofanyika katika Viwanja vya Parokia ya Yohana
Mbatizaji Nyamiongo Musoma kwa kujumuisha wanawake wa madhehebu ya Jumuiya ya
Kikristo Tanzania(CCT) na Wanawake WaKatoliki Tanzania(WAWATA) , Machi
Mosi, 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka( wa pili kushoto),
viongozi wa Kanisa na baadhi ya viongozi wa wanawake wakiwa ibada ya siku
ya maombi ya Dunia yaliyofanyika Machi Mosi, 2019 katika Viwanja vya Parokia ya
Yohana Mbatizaji Nyamiongo Musoma na kujumuisha wanawake wa madhehebu ya
Jumuiya ya Kikristo Tanzania(CCT) na Wanawake Wakatoliki Tanzania(WAWATA)
Na Stella Kalinga, Mara
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa wanawake, kuwa mstari wa mbele kuhimiza
jamii juu ya umuhimu wa kuwasomesha watoto, ili kuondokana mila potofu
zilizopitwa na wakati, ukiwemo ubaguzi wa kijinsia na mfumo dume.
Mtaka ametoa wito huo,
wakati wa siku ya maombi ya Dunia yaliyofanyika Nyamiongo Manispaa ya
Musoma Mkoani Mara ambako alikuwa mgeni rasmi, ambayo yaliwahusisha wanawake
kutoka katika madhehebu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania(CCT) na Wanawake Wakatoliki
Tanzania(WAWATA).
Amesema suluhisho la mila potofu zilizopitwa na
wakati kama mfumo dume, ubaguzi wa kijinsia na kuona watoto wa kiume ni bora
kuliko wa kike ni kuwasomesha watoto wote pasipo kujali kuwa ni wa kike au wa
kiume.
“Ukisomesha watoto wako vizuri wakafanikiwa kwenye
hiyo nyumba hakuna atakayesema yeye ni bora zaidi ya mwenziye, hakuna
atakayesema mimi ndiye mwanaume kwenye hii nyumba na huyu ni mwanamke,
somesheni watoto hayo mambo yote yaliyopitwa na wakati yataisha” alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka amewaomba wanawake na waumini wote wa
ujumla kuendelea kuliombea Taifa, Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli na viongozi wengine, ili nchi iendelee kuwa na amani na viongozi
waweze kufanya mazuri yaliyokusudiwa kwa ajili ya Watanzania wote.
Katika hatua nyingine Mtaka ametoa wito kwa
viongozi wa madhehebu ya dini pamoja na kusimamia kiroho wawe msaada kwa
makundi mbalimbali yaliyomo makanisani hususani vijana na wanawake, ili yaweze
kuendesha miradi ya maendeleo itakayowasaidia kubadilisha maisha yao kiuchumi.
Baadhi ya wanawake walioshiriki katika Maombi ya
dunia baada ya kusikia hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka ambaye alikuwa mgeni rasmi wamesema watahakikisha wanasimamia vema malezi
ya watoto wao na kuhakikisha wanasoma huku wakiunga mkono wazo la vikundi kuwa
na miradi ya maendeleo.
“ Kama mama nimejifunza mengi; moja ni kuwa
tukiwasomesha watoto wetu hakutakuwa na unyanyasaji, mfano kama kuna watu
wanafanya ukeketaji kwa watoto wa kike, jamii ikielimika haya hayatakuwepo na
tutahakikisha wanasoma mpaka vyuo vikuu; ujasiriamali nao tutafanya ili
tujikwamue kwenye umaskini” Devotha Charles mshiriki kutoka Mwisenge
“Baadhi ya wanawake katika makanisa yetu tulikuwa
hatua miradi na wengine waliokuwa nayo ilikuwa inaenda kwa kusuasua,
lakini baada ya ujumbe tulioupokea leo nina hakika utaleta mwamko kwa wanawake
wengi kuanzisha miradi ya kuwasaidia kupata kipato” Jackline Cheche mshiriki
kutoka Parokia ya Nyamiongo Musoma.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Katoliki la
Musoma Mhashamu Michael Msongazila amesema maombezi kwa ulimwengu yaendelee
kufanyika ili watu waweze kuheshimu uhai wa mwanadamu.
“Ombeeni ulimwengu uheshimu uhai wa mwanadamu
tumeumbwa katika sura na mfano wa Mungu, tumekabidhiwa dhamana hiyo ya uumbaji,
uhai huu tuulinde tuutetee na tuukuze kwa ajili ya kujenga ulimwengu, maisha
yetu yana nafasi ya pekee yanapokuwa na Mungu” alisema Askofu Mlonganzila.
Maombi ya Dunia kwa wanawake wa madhehebu ya
Jumuiya ya Kikristo Tanzania(CCT) na Wanawake Wakatoliki Tanzania(WAWATA)
hufanyika kila mwaka Machi Mosi yakiwa na lengo la kuombea familia, Taifa na
Dunia kwa ujumla juu ya amani na mahitaji mengine.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment