Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka
wajasiliamali wa Wilaya ya Nkasi kuhakikisha fedha ya mkopo waliyopewa na
halmashauri hawazitumii katika matumizi binafsi bali wazielekeze katika
biashara ili ziweze kuwapatia faida na kuwainua kiuchumi na hatimae kupata
fedha za kujikimu kimaisha.
“Kwenye vikundi vyenu mna malengo mahususi na ili
haya malengo mahususi yaweze kutimia kwenye biashara hakuna kingine zaidi ya
kuwa bahili lazima muwe mabahili, lazima muwe watu ambao hamkubali kutoa fedha
hovyo hovyo, uskibali kutoa fedha ambayo haina mpango, leo unaambiwa kuna msiba
pale wewe unachukua fedha ya mkopo unapeleka, huu sio ubahili, weka fedha yako
vizuri, kama kuna shida tafuta hela nyingine,na ukichukua fedha inayotokana na
hapo labda ni faida,” Alisema.
Ameyasema hayo alipokuwa akikabidhi mikopo yenye
thamani ya shilingi milioni 53 ikiwa ni asilimia 10 ya fedha za mapato ya ndani
ya halmashauri kwa vikundi 15 vya halmashauri ya wilaya ya Nkasi ikiwa ni
utekelezaji wa kisheria chini ya Baraza la Taifa la
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) lililoanzishwa Mwaka 2005 chini ya sheria
na 16 ya mwaka 2004 yenye adhima ya kuwainua wananchi kiuchumi ili
kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Katika kulisisitiza hilo Mbunge wa jimbo la Nkasi
Kaskazini Mh. Ally Kessy alisema kuwa pesa hizo ni kodi za wananchi ambazo
halmashauri inapita kuzikusanya nahatimae asilimia 10 ya mapato hayo kuyagawa kama
mikopo kwa wajasiliamali wanawake, vijana na walemavu na kusisitiza kuwa fedha
hiyo irudishwa kadiri inavyotakiwa.
“Fedha hii ni mkopo na sio sadaka, isiwe kukopa
harusi na kulipa matanga, kulipa ni wajibu, hizi pesa sio sadaka ni kodi ya
wananchi na kodi ya wanachi haiendi bure, mnakopeshwa mkafanye maendeleo sio
muanze kununua magauni au kwenda harusini hakuna ni kufanyia mtradi, kama
unaona kikundi chako hakina uwezo na kulipa msichukue ili wapewe wengine,”
Alisisitiza.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri
hiyo Emanuel Sekwao wakati akiseoma taarifa alisema
kuwa Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Jumla ya vikundi 15 viliomba mikopo ya
Tshs. 68,292,000.00. lakini baada ya Kamati ya Mikopo kukaa na kupitia maombi
ya mikopo jumla ya kiasi cha Tshs 53,000,000 kiliidhishwa.
“Vikundi vitakavyokopeshwa ni 15 ambapo
Vikundi vya Vijana vitatu Jumla ya fedha Tshs 12,687,000 Kikundi cha Walemavu
kimoja, Jumla ya fedha Tshs 2,000,000 na Vikundi vya Wanawake kumi na moja,
jumla ya fedha Tshs 38,313,000. Vikundi hivyo vimetoka katika kata za Mashete,
Kipundu, Majengo, Sintali, Namanyere, Chala, Kipande, Kabwe, Kate, Kirando na
Kala.”
Nae mkuu wa wilaya hiyo Mh. Said Mtanda
alimuhakikishia mkuu wa mkoa kuwa watajitahidi kuhakikisha wanakusanya mapato
ya halmashauri kwa asilimia 100 na kutoa mikopo hiyo kwa vijana na kuwapa fursa
ya kujiajiri lakini pia kuongeza viwanda vidogovidogo kutokana na shughuli
mbalimbali za uzalishaji wanazojihusisha nazo wajasiliamali hao.
Katika kutoa shukrani mmoja wa vijana wa kikundi
cha Panda Miti Rukwa (PAMIRU) Uswege Mwasomola alisema kuwa lengo lao ni kuwa
na shamba la miti la kikundi ili kusaidia kutunza mazingira na kuongeza kuwa
kutokana na mkopo huo walioupata wataweza kutatua changamoto walizokuwa nazo
kwa asilimia 100.
“Mkuu wa Mkoa pamoja na viongozi wote nadhani mwaka
ujao hatutakuja kukimbizana kufuatilia mikopo zaidi tutakwenda kifua mbele kwa
kuhakikisha tunairudisha kwa muda muafaka ili tutoe fursa kwa vijana wengine,”
alisema.
Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi katika mwaka wa
fedha 2018/2019 inatarajia kukusanya jumla ya Tshs 2,304,000,000/= kupitia
vyanzo vyake vya ndani. Katika kipindi cha kuanzia Julai 2018 hadi Februari
2019 jumla ya Tshs 1, 511,915,838.67 ilikusanywa ambapo sawa na asilimia 65.62
ya bajeti ya mwaka wa fecha 2018/2019.
0 comments:
Post a Comment