Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisalimiana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce
Ndalichako wakati alipowasili katika Ukumbi wa Nkrumah uliopo Chuo Kikuu
cha Dar es salaam kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuiya ya
Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), Agosti 10,
2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiongozana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa, Joyce
Ndalichako (kulia) na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salam,
Utawala, Profesa David Mfinanga (kushoto) wakati alipoingia katika
Ukumbi wa Nkrumah uliopo Chuo Kikuu cha Dar es salaam kufungua Mkutano
Mkuu wa Mwaka wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu
Tanzania (TAHLISO), Agosti 10, 2019. Wa pili kulia ni Mwenyekiti wa
TAHLISO, Peter Niboye
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisoma hati ya kiwanja ambacho kitajengwa Ofisi ya Jumuiya ya Wanafunzi
wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) kilichopo eneo la Mtumba
jijini Dodoma kilichotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas
Katambi (kushoto) Agosti 10, 2019 wakati Waziri Mkuu alipofungua Mkutano
Mkuu wa Mwaka wa TAHLISO katika Ukumbi wa Nkuruma uliopo Chuo Kikuu cha
Dar es salaam. Kulia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia,
Profesa Joyce Ndalichako na wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa TAHLISO,
Peter Niboye.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano
Mkuu wa Mwaka wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu
(TAHLISO) wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua
Mkutano huo katika Ukumbi wa Nkrumah uliopo Chuo Kikuu cha Dar es
salaam, Agosti 10, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akihutubia wakati alipofungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuiya ya
Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO) katika Ukumbi wa Nkrumah
uliopo Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Agosti 10, 2019. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
………………
BODI YA MIKOPO TAFAKARINI VIGEZO VYA KUTOA MIKOPO KWA WANAFUNZI-MAJALIWA
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
ameutaka uongozi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)
kutafakari namna ya kurekebisha baadhi ya dosari zilizopo likiwemo suala
la kuwanyima mikopo wanafunzi kwa kutumia kigezo cha kusoma katika
shule binafsi.
Amesema kuna baadhi ya
wanafunzi ambao wamefaulu vizuri kidato cha nne na wamekosa nafasi
katika shule za Serikali na wanatoka katika familia zisizokuwa na uwezo,
hivyo wanatafuta wafadhili ambao wanawasomesha kwenye shule binafsi.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo
leo (Jumamosi, Agosti 10, 2019) wakati akifungua mkutano Mkuu wa Mwaka
wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO)
kwenye ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Amesema kitendo cha bodi hiyo
kuwanyima mikopo baadhi ya wanafunzi kwa kigezo cha kusoma katika shule
binafsi bila ya kujiridhisha kama wanatoka kwenye familia zenye uwezo au
zisizokuwa na uwezo kinawanyima wanafunzi hao fursa za kuendelea na
masomo.
Waziri Mkuu ametumia fursa
hiyo kuwaonya wakuu wa vyuo vikuu ambao wanatumia vibaya fedha za mikopo
ya wanafunzi kwa kuzipeleka katika miradi mbalimbali baada ya kuzipokea
kutoka HESLB na kuwacheleweshea wanafunzi stahiki yao.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu
amewaagiza viongozi wa vyuo vikuu kuimarisha mafunzo kwa njia ya vitendo
kwani tafiti nyingi zinazohusu mambo ya ajira zimebainisha umuhimu wa
mafunzo ya vitendo katika kumuwezesha mhitimu kuwa na uelewa na ujuzi
mpana wa kile alichokisoma kwa njia ya nadharia.
“Vyuo viongeze umakini na
ufuatiliaji wa karibu wa vijana wetu wanapokuwa kwenye elimu kwa vitendo
ili kuhakikisha kwamba wanapata maarifa na ujuzi uliokusudiwa katika
mitaala yao. Pia natoa wito kwa waajiri wa sekta ya umma na binafsi
watoe ushirikiano wa dhati kwa wanafunzi wanaotafuta nafasi za kufanya
mafunzo kwa njia ya vitendo kwenye taasisi zao.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
TAHLISO, Bw. Peter Niboye amesema miongoni mwa changamoto
zinazowakabili wanafunzi wa elimu ya juu ni ucheleweshwaji wa mikopo kwa
baadhi ya vyuo licha ya HESLB kuwasilisha fedha hizo mapema, hivyo
ameiomba Serikali kuwasaidia katika kutatua tatizo hilo.
Kadhalika, Mwenyekiti huyo wa
TAHLISO, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt.
John Magufuli kwa ushirikiano mkubwa inaoipatia jumuiya hiyo hivyo
kurahisisha utendaji wake.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya
Dodoma, Bw. Patrobas Katambi alimkabidhi Waziri Mkuu hati ya kiwanja
kilichoko katika eneo la Mtumba jijini Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa
ofisi za TAHLISO, ambapo baada ya kupokea hati hiyo, Waziri Mkuu
aliikabidhi kwa Mkwenyekiti wa jumuiya hiyo Bw. Niboye.
Mkutano huo umehudhuriwa
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,
Bw. Godfrey Chongolo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Bw. Kisare Makori pamoja
na viongozi kutoka vyuo mbalimbali nchini vinavyounda TAHLISO.
0 comments:
Post a Comment