METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, June 26, 2026

Ziara ya Eng. Masaka Yatoa Mwelekeo Mpya wa Uzalishaji wa Mbegu ASA


















Na Mwandishi Wetu, Arusha

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Eng. Innocent Masaka, amesema wakala huo umejipanga kuboresha mashamba yake ya uzalishaji wa mbegu yaliyopo katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuwekeza katika miundombinu ya kisasa na kuyaendesha kwa mtazamo wa kibiashara ili kuongeza ufanisi wa uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima.

Eng. Masaka ameyasema hayo Juni 26, 2026, alipofanya ziara katika Shamba la Mbegu za Kilimo la ASA Arusha–Ngaramtoni lenye hekta 450 za uzalishaji wa mbegu, kwa lengo la kujionea hali ya uzalishaji wa mbegu pamoja na maendeleo ya uboreshaji wa miundombinu mbalimbali inayotekelezwa katika shamba hilo.

Alisema maboresho hayo yataongeza uwezo wa mashamba ya ASA kuzalisha mbegu bora na zenye ubora unaokidhi viwango vinavyohitajika, hatua itakayowezesha wakulima kupata mbegu kwa wakati na kwa bei nafuu. Aliongeza kuwa kuimarika kwa uzalishaji wa mbegu kutachochea ongezeko la tija katika sekta ya kilimo, kuinua kipato cha wakulima na kuchangia juhudi za Serikali za kuhakikisha usalama wa chakula nchini.

Aidha, Eng. Masaka alimpongeza Meneja wa Shamba la ASA Arusha–Ngaramtoni pamoja na watumishi wa shamba hilo kwa usimamizi mzuri na juhudi wanazozifanya katika kuendeleza uzalishaji wa mbegu bora. Aliwataka kuendelea kufanya kazi kwa weledi, ubunifu na uwajibikaji ili kuhakikisha ASA inaendelea kutekeleza jukumu lake la kuzalisha na kusambaza mbegu bora zinazokidhi mahitaji ya wakulima na kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com