Na.Alex Mathias,Mpwapwa
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa
uhuru kwa mwaka 2019 Mzee Mkongea Ally amegoma kuzindua mradi wa maji wa
Mzase uliopo wilayani Mpwapwa kutokana na kasoro mbalimbali za mradi
huo, ikiwamo kukosekana kwa vielelezo vya majibu ya vipimo vya mabomba
kutoka maabara ya serikali.
Akizungumza mara baada ya kukagua
miundombinu ya mradi huo Mkongea amesema baada ya ukaguzi wao wameona
kuna baadhi ya vitu walivyoomba kwenye mradi huo havipo lakini fedha
zinaonyeshwa zilitengwa.
“ Tulifanya ukaguzi kwa pamoja
tumeona kuna baadhi ya vitu vielelezo vyake havipo kama test za nondo
kutoka maabara ya serikali haipo,test za zege haipo,test za bomba kutoka
maabara ya serikali hazipo,ubaya wa hapa ni kwamba kazi hazikufanyika
lakini kwenye certificate fedha zimelipwa,”amesema Mkongea.
Amesema kutokana na kasoro hizo
inaonyesha utaratibu ulikiukwa kwa kufanya malipo hewa hivyo Mwenge wa
Uhuru 2019 hauwezi kuzindua mradi huo.
Kutokana na kasoro hizo amemtaka
mkuu wa Wilaya hiyo Jabir Shekimweri kumpa taarifa za mradi mkuu wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa(TAKUKURU)wilaya ili ajiridhishe
na matumizi ya pesa zilizotumika.
“Tunajua mkuu wa wilaya hili sio
kosa lako wala sio kosa la waheshimiwa wabunge,kuna wataalam ambao
wanataalum ya injinia kuweza kusimamia miradi hii ndio wanakiuka
utaratibu,mh mkuu wa wilaya tunakukabidhi taarifa ya mradi ili umkabidhi
afisa Takukuru,kila eneo liangaliwe ili kujiridhisha matumizi ya fedha
na baada ya wiki mbili taarifa itumwe makao makuu ya Takukuru,”amesema.
Pamoja na kasoro hizo Mkongea
amesema wameangalia ubora wa maji kwa mujibu wa vipimo vya maabara na
vimeonyesha kwamba maji ni salama kwa matumizi hivyo wananchi waendelee
kuyatumia.
Kwa upande wake waziri wanchi
ofisi ya makamu wa Rais Muungano na Mazingira George Simbachawene
amesema kitendo hicho kimekuwa ni fundisho kwa wao wanaoongoza jamii na
kwa wataalam ili wanapoyasikia mapungufu hayo waweze kusema na katika
vikao vya halmashauri.
Simbachawene ambaye ni mbunge wa
Kibakwe ametumia nafasi hiyo kusisitiza wananchi kutunza vyanzo vya maji
kwa kuheshimu sheria iliyopo ya kutofanya shughuli za kibinadamu ndani
ya mita 60 kutoka katika vyanzo vya maji.
Akizungumza baada ya maelekezo
hayo Shekimweri amesema wamepokea taarifa ya ukaguzi na watazingatia
maelekezo yaliyotolewa na kuyafanyia kazi.
Mradi huo umegharimu kiasi cha sh
mil 432.2 ukihusisha baadhi ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa
kisima,nyumba ya mashine,ujenzi wa tanki la kuhifadhi maji,ujenzi wa
mlango,ofisi ya jumuiya ya watumiaji maji na njia ya umeme mpaka eneo la
kisima.
0 comments:
Post a Comment