Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Constantine Kanyasu akizungumza na wachimbaji wadogo katika eneo
la Mataba ndani ya Shamba la miti la Biharamulo- Chato linalosimamiwa
na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania( TFS) kuhusu umuhimu wa kufuata
sheria na taratibu za kuchimba madini ndani ya Hifadhi hiyo katika mkoa
Geita.
Baadhi ya wachimbaji wadogo wa
madini ambao wanaendesha shughuli zao za uchimbaji madini katika Shamba
la miti la Biharamulo-Chato wakinyoosha mikono juu ikiwa ni ishara
kukubali maagizo aliyayatoa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.
Constantine Kanyasu kuwa wanapaswa kufuata taratibu na sheria za
uhifadhi wakati wanapochimba madini ndani ya hifadhi hiyo ya Misitu
mkoani Geita.
Mbunge wa Chato ambaye pia ni
Waziri wa madini Dkt.Medard Kalemani akizungumza na wachimbaji wadogo
katika eneo la Mataba ndani ya Shamba la miti la Biharamulo- Chato
linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania( TFS) kuhusu
umuhimu wa kufuata sheria na taratibu kabala ya kumkaribisha Naibu
Waziri Mhe, Kanyasu kuzungumza nao.
Baadhi ya Wachimbaji wadogo wa
madini ambao wanaendesha shughuli zao za uchimbaji madini katika Shamba
la miti la Biharamulo-Chato wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu kuhusu umuhimu wa kuunda
vikundi vya wachimbaji madini ili serikali iweze kuwatambua na wawe na
leseni na kisha waombe kibali kutoka TFS.
Mkuu wa wilaya ya Chato. Eng.
Mtemi Msafiri akizungumza na wachimbaji wadogo katika eneo la Mataba
ndani ya Shamba la miti la Biharamulo- Chato linalosimamiwa na Wakala wa
Huduma za Misitu Tanzania( TFS) kuwa hakuna Wawekezaji watakaowasumbua
wakati wa kuchimba madini yao kwa sasa hadi pale trakapowapa taarifa
rasmi.
Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Mhe, Constantine Kanyasu akizUngumza na baadhi ya watumishi wa
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wa kanda ya Ziwa wanaosimamia
Shamba la Miti la Biharamulo- Chato kabla ya kutembelea eneo la Mataba
ambako Wachimbaji wa madini wamezuiwa kuanzisha makazi mapya pamoja na
kuongeza maeneo ya uchimbaji mbali na yale waliyopo kwa sasa katika mkoa
wa Geita.
( Picha na Wizara ya Maliasili na Utalii)
**************
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhe.Constantine Kanyasu ameiagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (
TFS) kupitia Menejimenti ya Shamba la Miti la Biharamulo- Chato
mkoani Geita idhibiti upanuzi wa Uchimbaji madini unaofanywa na
Wachimbaji wadogo nje ya yale maeneo ambayo yanatambulika kwa shughuli
hiyo katika Shamba hilo.
Aidha, Mhe.Kanyasu ameiagiza TFS idhibiti
uanzishwaji wa makazi mapya pamoja na ukataji ovyo wa miti unaoendelea
hadi pale Kamati ya Mawaziri nane itakapotoa ripoti iliyokuwa imeundwa
na Rais John Pombe Magufuli kufuatia maombi yaliyokuwa yamewasilishwa
na wilaya ya Chato kupitia Mbunge wao, Dkt. Medard Kalemani ya kuomba
ardhi yenye ukubwa wa hekta 25 nje ya hifadhi hiyo ili kuwawezesha
Wachimbaji hao kuanzisha makazi yao ya kudumu.
Hatua hiyo inakuja kufuatia uwepo wa leseni saba
zilizotolewa na Wizara ya madini na kati ya hizo saba ni leseni moja tu
ndo ambayo imeshalipiwa kibali cha kufanya shughuli hiyo ndani ya
Shamba hilo
Agizo hilo amelitoa leo wakati akizungumza na
wachimbaji wadogo wapatao 2000 katika eneo la Matabe ndani ya Shamba
hilo, na kuwataka Wachimbaji hao wafuate sheria na taratibu
zinazotakiwa za kuchimba madini ndani ya shamba hilo.
Katika shamba hilo Wachimbaji wadogo wamekutwa
wakiendelea kuchimba dhahabu katika eneo la Matabe, Ilyamchele na
Nyantimba ambapo wengi wao wakiwa hawana leseni wala kibali cha
kuchimba kutoka TFS.
Amewataka Wachimbaji hao wajiunge katika vikundi
visivyopungua watu watano ili waweze kukidhi vigezo vya kupewa leseni na
badaye
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) itoe kibali cha kuwawezesha kufanya tathmini katika maeneo ya leseni hiyo.
Amesema kitendo cha Wachimbaji hao kukosa vibali
vya kuchimba madini ndani yua Shamba hilo kunaikosesha serikali mapato
kwa vile hawatambuliki.
Aidha, Mhe.Kanyasu amewaonya wachimbaji hao
kuacha tabia ya kukata miti ovyo kwa ajili ya shughuli za machimbo
pasipo kuomba kibali kutoka TFS
” Tutakapokubaini unakata miti kwa ajili ya
machimbo tutachukua sheria kali dhidi yako kwa kulipa faini au jela
miaka miwili” alilisitiza Kanyasu.
Kwa upande wake Mbunge wa Chato ambaye pia ni
Waziri wa Madini, Dkt.Medard Kalemani amewaeleza Wachimbaji hao kuwa nia
ya serikali sio kutaka kuwafukuza ila inawataka wafuate sheria na
taratibu ili waweze kutambulika na serikali
” Serikali inataka ninyi Wachimbaji wadogo
mnufaike wakati huo huo Serikali nayo inufaike hivyo lazima mjiunge
kwenye vikundi ili mtambulike kisheria.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Chato,
Mhandisi.Mtemi Msafiri amewaonya Iponya Nybihabi wanaodai kuwa wao ndo
wamiliki wa leseni waache kuwasumbua Wachimbaji wadogo kwani ofisi yake
haiwatambui
Kufuatia malalamiko mengi kutoka Wachimbaji
wadogo kuwalalamikia Wachimbaji hao Wakubwa, Mkuu wa wilaya hiyo
alilazimika kumuamuru Mkuu wa Polisi kuwakamata Wachimbaji hao wakubwa
na kisha kuondoka nao.
Naye ,Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo, Emanuel
Juang amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa licha ya kusumbuliwa mara kwa
mara na Wachimbaji Wakubwa katika eneo la Mataba lakini wapo tayari
kufuata sheria na taratibu zinazotakiwa ikiwemo suala kununua miti kwa
TFS kwa ajili ya uchimbaji madini.
0 comments:
Post a Comment