METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, August 5, 2019

Katibu Mkuu Mtigumwe aiagiza Taasisi ya Utafiti Makutupora kuitisha Mkutano Maalum wenye lengo la kuleta maboresho makubwa ya Kilimo cha Zabibu


Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo. Eng. Mathew Mtigumwe akipata maelezo kutoka kwa Dkt. Cornel Massawe, Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti wa zao la zabubu Makutupora cha Mkoani Dodoma wakati alipotembelea mabanda ya Taasisi za Wizara anayoiongoza Wizara ya Kilimo

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Eng. Mathew Mtigumwe amesema Wizara ya Kilimo ipo kwenye hatua za mwisho za kufanya mageuzi makubwa katika kilimo cha zabibu kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.

Na kwa hatua ya haraka Eng. Mtigumwe ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa zao la zabibu Kanda ya Kati Makutupora kuandaa mkutano wa pamoja na wa haraka mara baada ya Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nane Nane kuisha ili kuwakutanisha Wataalam na Wadau wa muhimu kwa ajili ya kuja na Mkakati wa pamoja wenye lengo la kuleta mabadiliko kwenye kilimo cha zabibu kwa kuanzia mkoa wa Dodoma.

Katibu Mkuu ametoa agizo hilo alipotembelea Banda la Taasisi ya Utafiti Tanzania, Kituo cha Makutupola (TARI - Makutupora) wakati wa Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nane Nane yanayoendelea mkoani Simiyu.

Eng. Mtigumwe amesema kilimo cha zabibu kina fursa kubwa kwa Wakulima wa mikoa ya Kanda ya kati na kwamba huu ni wakati muhafaka wa kuwahamsha hali ya Wakulima ili waanze kulima kwa tija na faida na kuongeza kuwa ni aibu kwa nchi kama Tanzania kwa Wananchi kula zabibu zinazotoka Afrika Kusini.

“Ni vyema sasa tulete mabadiliko makubwa kwenye kuongeza uzalishaji wa zao la zabibu na ninyi Kituo cha Utafiti Makutupora wana vipando zaidi ya hamsini nan ne (54), nina amini Wakulima wakiamasishwa, wataongeza uzalishaji na kuongeza wigo wa masoko ili Watazania wale bidhaa zao na zilizozalishwa hapa nchini na zenye kiwango bora kuliko zile zinazotoka nje”. Amekaririwa Eng. Mtigumwe.

Katibu Mkuu Eng. Mtigumwe ametolea mfano wa zabibu ambazo zinaingizwa kutoka Afrika Kusini kuwa gramu mia tano zinauzwa shilingi elfu tisa (9,000) wakati zile za Tanzania zinauzwa kati ya shilingi elfu tano (5,000) tu kwa kilogramu moja.

Baada ya maelezo kutoka kwa Msimamizi wa Kituo cha Utafiti Makutupora, Eng. Mtigumwe ameagiza Taasisi hiyo kuanda Mkutano mkubwa na wa haraka kwa kushirikiana na Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Halmashauri zake ili kukutana, kuandaa Mkakati wa pamoja wa maendeleo ya zao la zabibu.

Kwa upande wake Mtafiti wa zao la Zabibu katika Kituo cha Makutupora Dkt. Cornel Massawe amesema Kituo cha Utafiti wa Zabibu kimefanya juhudi za kuingiza zaidi ya vipando aina 54 mpaka sasa na kuongeza kuwa zabibu aina ya Black Rose, Muscat Italia (Maalum kuliwa kama Tunda), Makutupora Red (Maalum kwa Mvinyo) na Syrah (Maalum kwa kukausha) ndiyo zimekuwa zikipendwa na kulimwa na Wakulima wengi wa mikoa ya Kanda ya Kati.

Dkt. Massawe amesema agizo la Katibu Mkuu limepokelewa na litafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo kwa kuwa linalenga kuleta mapinduzi ya zao la zabibu kwa Wakulima wengi wa mikoa ya Kanda ya Kati na Tanzania kwa ujumla.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com