METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, August 6, 2019

WAZIRI MKUU: MAONESHO YA SADC NI FURSA PEKEE KWA WATANZANIA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa George Lous Chuwa kuhusu bidhaa mbalimbali wakati alipotembelea banda la Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika Maonyesho ya Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Viwanda kwa Nchi za SADC kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Agosti 6, 2019. Wapili kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Maofisa Habari wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) , Jamila Mbarouk (kulia) na Ben Mwanantala wakati alipotembelea banda la TRC katika Maonyesho ya Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Viwanda kwa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Agosti 6, 2019. Wapili kushoto ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocenti Bashungwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Wickled Msian ambaye ni Meneja wa Kudhibiti Ubora wa Bidhaa wa Kampuni ya Ital shoe (wa pili kulia) wakati alipotembelea banda la kampuni hiyo katika Maonyesho ya Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Viwanda kwa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Agosti 6, 2019. Wa pili kushoto ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocenti Bashungwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Dkt William Mugisha wakati alipotembelea banda la Taasisi ya Mifupa (MOI) katika Maonyesho ya Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Viwanda kwa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dr es salaam, Agosti 6, 2019. Wapili kushoto ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocenti Bashungwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama picha yake iliyochorwa kwa kutumia shanga na Bw. Aman Greon (kulia) wakati alipotembelea Maonyesho ya Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Viwanda kwa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Agosti 6, 2019. Wa pili kushoto ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea Maonyesho ya Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Viwanda kwa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Agosti 6, 2019. Wa pili kushoto ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocenti Bashungwa. Wengine kutoka kushoto ni Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema wiki ya maonesho ya nne ya viwanda ya nchi za SADC ni fursa pekee ya kutangaza bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Agosti 6, 2019) wakati akizungumza na waandishi wa habari mara ya kukagua mabanda kwenye maonesho hayo yanayoendelea kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Maonesho hayo ambayo yalifunguliwa jana na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, yanafanyika katika maeneo matatu ambayo ni ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere, viwanja wa Gymkhana na viwanja vya Karimjee.
“Nimekuja kufanya ufuatiliaji wa maandalizi ya mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za SADC, nimekuta yanaendelea vizuri. Nimekuja kuangalia mwitikio wa wajasiriamali wa pande zote mbili za Muungano pamoja na wajasiriamali kutoka nchi wanachama wa SADC, na pia mwitikio wa wananchi wetu ukoje,” amesema.
Waziri Mkuu amesema fursa hiyo ni muhimu kwa Watanzania kuonesha bidhaa za ndani ili wageni wanaokuja wajue kuna bidhaa zipi zinazozalishwa nchini. “Tumetoa fursa kwa nchi za SADC zote nao pia waoneshe bidhaa zao. Maonesho haya ni ya wazi, Watanzania wanayo nafasi ya kuja kuona na kujifunza,” amesema.
Amesema mbali ya fursa ya masoko, Tanzania inayo pia fursa ya kupata teknolojia mpya na za Kisasa ikiwa ni pamoja na wawekezaji wa viwanda vya usindikaji bidhaa mbalimbali. “Tumeona utaalamu unaotumika kutengeneza bidhaa mbalimbali, hii maana yake ni kwamba tunajifunza na teknolojia zinazotumika,” amesema.
“Tunayo fursa ya kukaribisha viwanda kutoka nje ya nchi, wote hapa wameleta bidhaa zao. Pia tunawakaribisha waje waanzishe viwanda kwa ubia na Watanzania. Sisi tunayo ardhi, tunazalisha mazao mengi tu, kwa hiyo mbia wa nje anaweza kuunganisha mtaji na Mtanzania na wakajenga kiwanda hapa nchini,” amesema.
Mbali ya fursa za kiuchumi kwao binafsi, Waziri Mkuu amewataka washiriki wa maonesho hayo, watangaze vivutio vya utalii vilivyopo nchini ambavyo vitasaidia kuwafanya wageni wanaoshiriki mkutano huo watamani kubaki nchini na kuvitembelea.
“Watanzania tutumie nafasi hii kutangaza vivutio vingine tulivyonavyo. Mbuga za wanyama tunazo nyingi, tunao Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu kuliko yote barani Afrika na huwezi kuupanda kutokea popote. Ili uupande, ni lazima uje Tanzania,” amesema.
“Pia tuna eneo maarufu la Olduvai Gorge ambalo ni chimbuko la binadamu wa kwanza duniani, na hili liko eneo liko Ngorongoro. Tuna fukwe nzuri, zenye mchanga mzuri ambazo ukikaa wala huwezi kuchafuka, zina urefu wa zaidi ya km. 1,400 kutokea Tanga hadi Mtwara,” ameongeza.
Mapema, Waziri Mkuu alifanya kikao na Mawaziri wa Mambo ya Nje, Utumishi na Utawala Bora, Viwanda na Biashara wa SMT, Viwanda, Biashara, Wazee na wa Zanzibar (SMZ), Naibu Mawaziri wa TAMISEMI, Mambo ya Nje na Mifugo na Uvuvina kuwapa maelekezo ya kuboresha maandalizi hayo. Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Makatibu Wakuu wa wizara hizo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com