Waziri wa Nishati, Dkt Medard
Kalemani (katikati) akikata utepe kuashiria uwashaji rasmi umeme katika
Kijiji cha Isenegeja wilayani Igunga.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard
Kalemani (katikati) akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Uswaya
wilayani Igunga wakati alipofika kukagua kazi ya usambazaji umeme kwenye
Kijiji hicho.
…………………
Na Hafsa Omar, Tabora
Waziri wa Nishati, Dkt Medard
Kalemani ameendelea na ukaguzi wa kazi ya usambazaji umeme vijijini ili
kuhakikisha kuwa lengo la Serikali la kuhakikisha kuwa vijiji vyote
vinafikiwa na nishati ya umeme ifikapo mwaka 2021 linafanikiwa.
Tarehe 21 Agosti, 2019, alikagua
kazi hiyo katika Kijiji cha Mwisi, Uswaya na Isenegeja wilayani Igunga
ambapo aliwasha umeme katika Kijiji cha Isenegeja.
Aidha, akizungumza na wananchi kwa
nyakati tofauti, alilisisitiza kuhusu wananchi kulipia gharama ya
shilingi 27,000 tu, na bila kujali aina ya nyumba wanazomiliki.
“ Umeme ndiyo nguzo kuu ya
maendeleo, hivyo nawasisitiza kuchangamkia huduma hii inayotolewa na
Serikali ili muweze kujifanyia shughuli mbalimbali za kiuchumi, kama
tulivyosema umeme hautachagua nyumba, umeme wa Serikali hii unapelekwa
kwa watanzania wote bila kujali masikini, tajiri au mtanzania wa
kawaida.”alisema Dkt Kalemani.
Aidha, Dkt Kalemani aliwaagiza
wakandarasi kuacha tabia ya kuchelewa kuwaunganishia umeme wananchi “
nimeshasema ni marufuku kuchelewa kuunganishia umeme wananchi, mtu
akishalipia muunganishie umeme ndani ya siku Saba bila kisingizio
chochote.”
Kuhusu hali ya umeme nchini,
alisema kuwa, hali ya umeme ni nzuri na endapo kunatokea kukatika kwa
nishati hiyo, ni kwasababu ya hitilafu tena ya dharura ama kwasababu ya
matengenezo.
Kwa nyakati tofauti wananchi wa
Vijiji hivyo waliishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kusambaza
nishati ya umeme vijijini na kueleza kuwa itawawezesha kufanya shughuli
mbalimbali ikiwemo kuanzisha mashine za kukoboa nafaka ambapo hapo awali
walilazimika kutumia dizeli ili kuziendesha lakini kwa sasa watatumia
nishati ya umeme na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji.
0 comments:
Post a Comment