*******************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) itafute mbinu bora zaidi na
kuvijengea uwezo vyuo vikuu binafsi ili visaidie kuongeza udahili.
“Tume itafute mbinu bora zaidi
ikiwa ni pamoja na kuvijengea uwezo vyuo vikuu binafsi ili visaidie
kuongeza udahili. Ni wakati muafaka kwa Tume kujipambanua kwenye
uwezeshaji na ushauri ili kuondoa taswira hasi miongoni mwa jamii kwamba
kazi kubwa ya TCU ni kuvifungia vyuo vikuu badala ya kuvisaidia kutatua
changamoto zinazovikabili,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo
leo, (Jumatano, Julai 17, 2019) wakati akifungua maonesho ya 14 ya Elimu
ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mnazi
Mmoja, jijini Dar es Salaam. Maonesho hayo yatafungwa Julai 20, mwaka
huu.
Amesema Serikali inatambua
kwamba vyuo vikuu binafsi ni washirika muhimu wa maendeleo ya sekta
ndogo ya elimu ya juu nchini. “Naomba nieleweke vizuri kwamba hakuna
mbadala wa elimu bora bali nasisitiza Tume ivisaidie vyuo vikuu kufikia
viwango vinavyotakiwa na siyo kuwapunguzia viwango vya matakwa ya
usajili,” amesema.
Akitoa ufafanuzi kuhusu idadi
ndogo ya wahitimu wa elimu ya juu, Waziri Mkuu amesema takwimu za
kimataifa za ushiriki wa elimu ya juu zinaonesha kwamba kufikia mwaka
2017 ni asilimia moja hadi tatu tu ya Watanzania kwa kila Watanzania 100
wenye umri chini ya miaka 25 wanapata elimu ya Chuo Kikuu.
“Idadi hii ni ndogo zaidi ya
majirani zetu wa Kenya wenye asilimia nne, Zambia asilimia nne na
Namibia asilimia 14. Bado tunayo kazi kubwa sana ya kufanya. Natoa
maelekezo kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iongeze jitihada na
mikakati ya kuboresha uwiano huu ambao upo chini ikilinganishwa na
majirani zetu,” alisisitiza.
Amesema ili kuongeza idadi ya
Watanzania wanaopata nafasi ya elimu ya juu, ni lazima tupange mikakati
yetu kama nchi kwa kushirikiana na sekta binafsi, ambao ni wadau wakubwa
katika elimu ya juu. “Taarifa nilizonazo ni kwamba, kati ya wahitimu
wote wa vyuo vikuu kwa mwaka, asilimia 25 wanatoka katika vyuo vikuu
binafsi. Mchango huu si mdogo, na ningetamani uongezeke zaidi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amewapa changamoto wakuu wa vyuo vikuu nchini wabadilishe mtazamo
wao juu ya upimaji wa ufanisi wa wahitimu na badala yake upimaji wao
ujielekeze kwenye kutoa suluhisho na kubadilisha maisha ya Watanzania
badala ya kutumia machapisho ya kitaaluma.
“Kipimo cha ufanisi katika
taaluma ilikuwa ni machapisho ya kitaaluma, ambapo mengi ya hayo, jamii
pana haifaidiki nayo. Sasa ni wakati mwafaka kutafakari iwapo kipimo
hicho kinatosheleza. Kwa vyuo vikuu ambavyo mmehudhuria hapa leo, naomba
niwape mtazamo tofauti. Kipimo cha ufanisi wa wanataaluma wa Tanzania,
kuanzia sasa kinafaa kiwe ni kiasi gani taaluma yao inawafikia na
kubadilisha maisha ya wananchi, na kiwango cha bidhaa na hatimiliki
(patents) zilizozalishwa na kusajiliwa na wasomi wetu waliopo vyuo
vikuu.”
Amesema matarajio ya Serikali
ni kuona kwamba tafiti na vipimo vya ufanisi kwenye vyuo vikuu viwe ni
kiasi gani vyuo hivyo vinatoa bidhaa mbalimbali za kuleta ajira pamoja
na kukabiliana na matatizo ya kijamii. “Ningefurahi iwapo kuanzia sasa
kipimo cha ufanisi wa vyuo vikuu vyetu iwe katika kupima jitihada za
vyuo vyetu kuisaidia Serikali katika azma yake ya kufikia kwenye uchumi
wa kati,” amesema.
“Huu ni wakati muafaka kuanza
kupima ufanisi wa wakuu wa vyuo kwa kuangalia kiasi gani mazao ya Chuo
Kikuu hicho yamewafikia wananchi na pia katika utekelezaji wa mikakati
ya maendeleo ya Serikali, hasa mapinduzi ya viwanda,” amesisitiza.
Mapema, akielezea kuhusu
maonesho hayo, Mwenyekiti wa TCU, Prof. Jacob Mtabaji aliwataka wahitimu
wa kidato cha sita wanaoomba kujiunga na vyuo vikuu, wasome kwa umakini
mwongozo uliowekwa kwenye tovuti na wasikubali kupitia mawakala
wanaodai kuwa wanaweza kufanya usajili kwa niaba yao. Pia aliwataka
wazingatie kalenda ya udahili.
Akielezea changamoto za elimu
ya juu nchini, Prof. Mtabaji alisema kuna uhaba wa wahadhiri wenye sifa
stahiki katika vyuo vikuu vingi na akawaomba wakuu wa vyuo hivyo
wawasomeshe wahadhiri katika ngazi mbalimbali ili wakirudi wajiunge na
vyuo husika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
TCU, Prof. Charles Kihampa alisema taasisi 81 za elimu ya juu
zimeshiriki maonesho hayo ambapo taasisi 15 ni za nje ya nchi na taasisi
66 ni za hapa nchini.
Akitoa shukrani, Mwenyekiti wa
Kamati ya Watendaji Wakuu wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki
(CVCPT), Prof. Raphael Chibunda alisema anaishukuru Serikali ya awamu ya
tano kwa uboreshwaji uliofanywa kwenye upatikanaji na upelekwaji kwa
wakati wa fedha kutoka Bodi ya Mikopo. “Zamani, sauala hili hiloi likuwa
ni chanzo cha migomo mingi vyuoni lakini kwa sasa limekwisha,” alisema.
Pia aliishukuru Serikali kwa
kukubali kurudisha jukumu la udahili wa wanafunzi katika Seneti za Vyuo
Vikuu kwani hapo nyuma lilikuwa sehemu ya mgogoro baina ya TCU na vyuo
vikuu.
0 comments:
Post a Comment