Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wananchi, baada ya kufungua Ofisi na Tawi la Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB), katika jengo la PSSSF jijini Dodoma, Juni 24.2019 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
...........................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema sekta ya fedha inapaswa kuwa imara na kuhakikisha huduma zake
zinawafikia wananchi wengi katika maeneo ya mijini na vijijini ili iweze
kutoa mchango unaokusudiwa katika kuinua uchumi wa nchi na ustawi wa
jamii.
Ameyasema hayo leo (Jumatatu,
Juni 24, 2019) wakati alipofungua Ofisi Ndogo na Tawi la Benki ya
Biashara ya TIB jijini Dodoma. Amesema ukuaji wa sekta ya huduma za
kifedha ni muhimu sana katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini.
Waziri Mkuu amesema benki
ndicho chombo kikuu cha kutolea huduma za kifedha kwa wananchi, hivyo,
benki zinatakiwa kuzingatia mahitaji ya wananchi, kuwahamasisha na
kuwaelimisha umuhimu wa kutumia benki.
“Wananchi nao pia wana wajibu
wa kuzitumia benki hizi kwa kutunza akiba zao na kukopa wakati
wanapohitaji kuwekeza kwa malengo yaliyokusudiwa. Suala la msingi ni
kuwa mnapokopa mkumbuke pia kurejesha kulingana na makubaliano.”
“Sifurahishwi sana na takwimu
zinazoonesha kwamba ni asilimia 16.7 tu ya Watanzania wote ndiyo
wanaopata huduma za kifedha kupitia mifumo halali ya kibenki, huku
asilimia 48.6 wakipata huduma za kifedha kupitia mitandao ya simu na
asilimia 35 ya waliosalia kutopata kabisa huduma rasmi za kibenki.”
Waziri amesema hali hiyo
haikubaliki kwenye nchi kama Tanzania ambayo inakabiliana na ujenzi wa
uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, hivyo ametoa wito kuwa benki zote
ziendelee kubuni mikakati na mbinu zitakazowawezesha Watanzania wengi
zaidi kupata huduma rasmi za kibenki tena kwa gharama nafuu ili waweze
kujiongezea kipato na kujikwamua kutoka kwenye umaskini.
Hata hivyo, Waziri Mkuu
amesema tozo za mabenki kwa wateja bado ni kubwa na haziwasaidii
wananchi wa kawaida, kwa hiyo, zipunguzwe. “Riba kwa wakopaji nazo ziko
juu sana ukilinganisha na mfumuko wa bei, pia nazo zipunguzwe.”
Kuhusu changamoto ya riba
kubwa inayotozwa kwa mikopo ya benki, Mheshimiwa Majaliwa amesema tayari
Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imefanikiwa kupunguza riba ya
hati fungani za Serikali, pamoja na ile inayotozwa kwa mabenki
yanayokopa Benki Kuu. Moja ya lengo la kufanya hivyo ni kutaka riba za
mabenki zipungue.
“Naomba mabenki yaunge mkono
jitihada hizo za Serikali kwa kupunguza riba zinazotozwa hasa kwenye
mikopo ya watu binafsi na biashara ndogo ndogo kwani hawa wakipata
unafuu wataweza kukuza biashara zao na hivyo kupelekea kuongezeka kwa
uzalishaji.”
Akizungumzia suala la baadhi
ya benki kuwa na tawi moja au mawili jijini Dar-es-Salaam tu, Waziri
Mkuu amesema tayari Serikali imeshaiagiza Benki Kuu ya Tanzania kupitia
Wizara ya Fedha na Mipango kuzitathimini upya benki za aina hiyo.
“Leo narudia tena kuiagiza
Benki Kuu ya Tanzania kuzisimamia benki zetu ili zifungue matawi yake
hadi vijijini waliko wenye uhitaji.! Kwanini? benki nyingi zimejikita
katika kutafuta faida pekee bila kuwekeza kwa faida ya nchi yetu? Hadi
sasa tuna benki ambazo zimekuwa siku zote na tawi moja tu tena liko
Dar-es-Salaam. Benki Kuu ya Tanzania isisite kuchukua hatua za kisheria
kurekebisha hali hiyo.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya Biashara ya TIB, Frank Nyabundege amesema kwa
kipindi cha miaka minne benki hiyo imeweza kukuza mtaji kutoka sh.
bilioni 206 wakati inagawanywa mwaka 2015 mpaka kufikia sh. bilioni 409
mwishoni mwa mwaka 2018 sawa na ukuajia wa aslimia 98.5.
Mkurugenzi huyo amesema mbali
na kufanikiwa katika kukuza mtaji, pia benki hiyo imeweza kukuza amana
za wateja kutoka sh. bilioni 110 mwaka 2015 mpaka sh. bilioni 338 mwezi
Disemba 2018, sawa na ukuaji wa asilimia 207.
“Mafanikio mengine yabenki ya
TIB katika kipindi cha miaka minne ni pamoja na kuanza kutengeza faida
angalau ya sh. bilioni 1.3 mwaka jana (2018), kutoa mchango stahiki
katika Mfuko Mkuu wa Serikali kiasi cha sh. milioni 250.”
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa
benki hiyo imetoa mikopo na dhamana kwa taasisi za umma hadi kufikia
shilingi bilioni 224.35 kwa kipindi kilichoishia Machi 2019, kulipa kodi
Serikalini kiasi cha sh. bilioni 19.2 tangu benki ianzishwe na kutoa
mikopo kwenye sekta ya viwanda jumla ya sh. bilioni 65.12.
0 comments:
Post a Comment