Katibu wa NEC, Itikadi
na Uenezi Ndg Humphrey Polepole
Na Mathias Canal,
Dar es salaam
Chama Cha
Mapinduzi Kimefuta Uchaguzi katika Kata 44 kati ya kata 3727 zilizofanya Uchaguzi katika ngazi
Mbalimbali kutokana na kukiuka taratibu za Uchaguzi ikiwa Ni ishara ya Kuelekea
kuwa na CCM mpya na Tanzania Mpya.
Kufutwa kwa
uchaguzi katika Kata hizo Ni matokeo ya ukiukwaji wa Kanuni za Uchaguzi na
katiba ya CCM, kuendeleza makundi baada ya Uchaguzi, Kupanga safu za Uongozi
kwa maamuzi ya Nani awe kiongozi Jambo ambalo Ni kinyume na utaratibu wa
Uchaguzi.
Akitangaza Kufutwa
kwa uchaguzi katika Kata hizo mbele ya waandishi wa habari katika mkutano
uliofanyika katika Ukumbi mdogo wa CCM wa (OND)-Lumumba Katibu wa NEC, Itikadi
na Uenezi Ndg Humphrey Polepole alisema kuwa hiyo Ni Awamu ya kwanza ya kufanya
maamuzi lakini wale wote waliosababisha kadhia hiyo watachukuliwa Hatua kwa
mujibu wa taratibu za Chama.
Alisema kuwa wapo
wagombea wengine walipokuwa Viongozi katika Awamu zilizopita walishindwa kutoa
usimamizi wa Mali za Chama lakini bado wamerejeshwa katika uongozi huku wengine
wakiwa si wakazi wa maeneo husika walipoomba nafasi za Uongozi.
Sababu nyingine Ni
pamoja na baadhi ya maeneo wajumbe wa vikao kutopewa taarifa sahihi za wagombea
Jambo ambalo lilipelekea kuchagua viongozi wasiokuwa na sifa.
Polepole alisema
kuwa Kwa mujibu wa Katiba ya Chama Cha Mapinduzi imetoa mamlaka kwa Katibu Mkuu
kutoa Maelekezo ya kufuta Uchaguzi kwa mashauriano na Mwenyekiti wa CCM hivyo
kupitia mashauriano Kati ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli na Katibu ya Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
Ndg Abdulrahiman Kinana kufuta Uchaguzi na kuagiza kurejea upya Uchaguzi huo
baada ya kusikiliza malalamiko na kero za kiuchaguzi.
Polepole alizitaja
kata hizo kuwa ni Buguruni, Liwiti, Kariakoo, Manzese, Makuburi, Mabibo,
Kigamboni, Kiburugwa, Mchafukoge, Gerezani, Segerea, Pugu, Pugu Stesheni, Ilala, Kijitonyama (Tawi la Mwenge), Mbagala kuu,
Mianzini, Ndugumbi, Kilungule, Makumbusho, Kitunda, Ukonga, na Msasani katika
Mkoa wa Dar es salaam.
Nyingine Ni Kata
ya Mapinga iliyopo Mkoa wa Pwani, Kata ya Lumemo Mkoani Morogoro, Kata zote 18
za Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara sambamba na Kata ya Seria kwa vijana iliyopo Kondoa
Vijijini Mkoani Dodoma.
Polepole alitoa
Rai kwa Viongozi wote wa Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya zake kuendelea
kusimamia katiba, Kanuni na maadili katika kipindi chote Cha Uchaguzi wa ndani
wa Chama kwa kupiga Vita rushwa kadhalika na ubadhilifu wa Mali za umma.
Alisema kuwa CCM
inaongozwa kwa mujibu wa Katiba na kanuni hivyo kama kuna kiongozi atabainika
kukiuka taratibu na maadili ya Chama atachukuliwa Hatua ya kuhojiwa na kamati
ya maadili na kupitia vikao Hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yake.
Aliongeza kuwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli anawakumbusha watendaji wa chama katika ngazi zote kuzingatia, katiba, kanuni na kutenda haki kwa kila kutakopokuwepo na malalamiko, yasikilizwe na kutatuliwa kwa wakati kwani kwa mujibu wa katiba na kanuni viongozi na watendaji watakaoshindwa kushughulikia kero ya malalamiko kwa wakati watalazimika kuwajibika kama viongozi na watendaji
MWISHO
0 comments:
Post a Comment