
*************
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amesema kuanzia Julai Mosi mwaka huu Serikali itaanza kutekeleza Mpango
Kazi wa Utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara
nchini (Blueprint) kwa lengo la kurahisisha mazingira ya kufanya
biashara.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Ijumaa, Juni 28) wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, jijini
Dodoma. Amesema wakati kazi hiyo inaendelea Serikali itafanya
ufutialiaji kuhusu utekelezaji wa mpango huo na kutathmini kama lengo
limefikiwa.
”Utekelezaji wa mpango huo
unakwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya kurahisisha mazingira ya
kufanya biashara nchini, unaojidhihirisha kupitia sheria ya fedha ya
mwaka 2019 ambayo imefuta tozo kwamishi 54 zilizobainishwa kwenye mpango
huo.”
Waziri Mkuu ametaja tozo
zilizoondolewa au kupunguzwa ni pamoja na zinazosimamiwa na Shirika la
Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Mamlaka ya
Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Wizara ya Mifugo na Uvuvi
hususan kwenye Sekta ya Mifugo, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara
ya Maji
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema
katika kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unaleta tija, ameielekeza
Wizara ya Viwanda na Biashara ishirikiane na Ofisi ya Waziri Mkuu
kusambaza blueprint pamoja na Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa wizara zote
kwa ajili ya kusimamia utekelezaji katika maeneo yao.
Amesema kupitia mpango wa
bajeti ya 2019/2020, Serikali itaendelea kuweka mazingira rahisi ya
ufanyaji biashara kwa kutoa unafuu katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi
pamoja na shughuli nyingine jumuishi.
Wakati huohuo,Waziri Mkuu
amesema katika kukabiliana na kilimo tegemezi cha mvua hususani kwenye
zama hizi za mabadiliko ya tabia nchi, Serikali kwa sasa inaboresha
kilimo cha umwagiliaji kwa lengo la kuwatoa wananchi katika kilimo
hicho.
Amesema hatua zilizochukuliwa
hadi sasa ni pamoja na kuunda upya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ambayo
inalenga kuiwezesha tume hiyo kusimamia ipasavyo shughuli za
umwagiliaji. Pia Serikali imehamishia tume hiyo Wizara ya Kilimo ambayo
ndiyo yenye dhamana ya kuendeleza kilimo nchini.
”Ili tuweze kufikia lengo la
kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 475,056 za sasa
hadi hekta 1,000,000 ifikapo mwaka 2025, tayari nimeielekeza Wizara ya
Kilimo isimamia kwa karibu na kutekeleza majukumu yake kwa weledi.”
Waziri Mkuu amesema Wizara ya
Kilimo inatakiwa ihakikishe inasimamia vema miradi 22 ya umwagiliaji
inayoendelea sasa pamoja na miradi mipya minane itakayojengwa nchini
katika pindi cha mwaka wa fedha 2019/2020.
0 comments:
Post a Comment