METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, July 20, 2018

Kituo kipya cha umeme kujengwa mkoani Geita

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na Mkandarasi wa anayejenga kituo cha kupoza umeme mkoani Geita,  Lane Lei wa Kampuni ya China CAMC Engineering Co Ltd, wengine ni watendaji mbalimbali walioambatana na Waziri wa Nishati.
Baadhi ya Transforma 7 zilizotolewa na Serikali kwa Mkoa wa Geita kwa ajili ya kufungia wachimbaji wadogo wanaojishughulisha na kazi ya uchejuaji madini mkoani Geita.
Wananchi wa kata ya Nyamwilolelwa wilayani Geita wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani)
Na Rhoda James - Geita
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa changamoto ya uwepo wa umeme mdogo mkoani Geita itakwisha baada ya Serikali kuamua kujenga kituo cha kupoza umeme chenye uwezo wa megawati 98.
Waziri Kalemani aliyasema hayo akiwa mkoani Geita katika ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini Awamu ya Tatu (REA III) pamoja na miradi mingine ya umeme.
Dkt. Kalemani alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho cha kupoza umeme umeshaanza na mkandarasi ambaye ni China CAMC Engineering Co Ltd, atakamilisha kazi ndani ya miezi mitano.
Alieleza kuwa, kwa sasa Geita inapata Umeme kutoka katika Vituo vya Sengerema mkoani Geita, Nyakato mkoani Mwanza na  Kahama mkoani Shinyanga.
Aliongeza kuwa, lengo la kujenga kituo cha kupoza umeme mkoani Geita ni kuuunganisha Mkoa huo na Gridi ya taifa kutoka katika Kituo cha Shinyanga ili kuweza kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika.
Aidha alisema kuwa, kwa kutambua mahitaji makubwa ya umeme kwa wachimbaji wa madini, Serikali imepeleka transfoma Saba ili zitumike kwa shughuli za uchenjuaji na kuuagiza Mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM) kuanza kutumia umeme wa TANESCO kama ilivyo kwa wachimbaji wengine.
“Wachimbaji wasilalamike umeme hautoshi, bali waombe umeme zaidi kwa ajili ya shughuli zao na Transforma hizi pia zitumike kwa wananchi wa kawaida wanaozunguka maeneo hayo ili wasione kama wametengwa ,” alisema Waziri Kalemani.
Kuhusu mradi wa REA III mkoani Geita, alisema kuwa jumla ya vijiji 262 vitasambaziwa umeme katika mzunguko wa kwanza unaokamilika Juni, 2019, aidha, Awamu ya Pili itakuwa na vijiji takriban 110 ili kukamilisha vijiji vyote vya mkoa wa Geita.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa  wa Geita,  Mhandisi Robert Gabriel, alisema kuwa, nishati ni muhimu kwa uanzishaji wa viwanda mkoani humo na mitambo mbalimbali ya kuzalisha dhahabu iliyopo  mkoani humo inahitaji umeme wa kutosha.
 “Tatizo lililopo kwa sasa ni upungufu wa umeme, lakini tukilifanyia kazi basi tutakuwa hatuna shida, ” alisema Mhandisi Gabriel.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com