Tanzania ikiwa ni nchi mwanachama wa
Umoja wa Mataifa inaungana na Mataifa mengine Duniani kuadhimisha Siku
ya Kimataifa ya Kupambana na Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya kwa
lengo la kuikumbusha jamii juu ya tatizo kubwa lilipo katika jamii yetu
juu ya Biashara na Matumizi ya Dawa za hizo.
Kitaifa Maadhimisho haya kwa mwaka huu
yatafanyika jijini Tanga siku ya Jumatano tarehe 26 mwezi Juni, 2019
katika viwanja vya Tangamano na Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Mheshimiwa George H. Mkuchika (Mb).
Kauli mbiu ya Kimataifa ya maadhimisho haya kwa mwaka huu inasema Waathirika wa Dawa za Kulevya Wana Haki ya Kupata Huduma za Afya.
Kwa kuzingatia Kauli mbiu hii inakumbusha kuwa mapambano dhidi ya
Tatizo la Dawa za Kulevya yanahitaji mikakati mtambuka na jumuishi
ikiwemo suala la tiba kwa waathirika. Ni muhimu kwa Waathirika wa Dawa
za Kulevya kupata tiba stahiki na zilizothibitishwa kisayansi (evidence
based practices) ili kuweza kupunguza madhara ya dawa hizo kwa waraibu
na jamii inayowazunguka.
Baada ya tiba hizo, huduma endelevu za
Stadi za Kazi pamoja na Ushauri Nasaha kuzingatiwa ili kuwasaidia
waathirika wasirudi kwenye matumizi ya dawa za kulevya. Aidha, mkakati
huu unaenda sambamba na mkakati wa utoaji wa elimu kwa vijana ili
wasiingie kwenye matumizi ya Dawa za Kulevya pamoja na Udhibiti wa
wafanyabiashara wa Dawa hizo.
Maadhimisho haya ni fursa kwa umma wa
Watanzania kwa vile Tatizo la Dawa za Kulevya linaathiri nchi yetu
katika nyanja za kiafya, kijamii, kiuchumi pamoja na kutishia ulinzi na
usalama wa nchi yetu. Katika maadhimisho haya Watanzania wataweza kupata
elimu na kukumbushwa kuwa matumizi na biashara ya dawa za kulevya yana
athari kubwa kwa mtumiaji, kwa jamii na kwa mustakabali wa maendeleo ya
nchi yetu.
Tatizo la dawa za kulevya husababisha
madhara kiafya ikiwa ni pamoja na kuchochea kuenea kwa maambukizi ya
virusi vya UKIMWI, virusi vya homa ya ini aina ya B na C, Kifua Kikuu,
magonjwa ya akili, pamoja na usugu wa tiba ya kifua kikuu na UKIMWI.
Aidha, baadhi ya dawa za kulevya husababisha matatizo ya uzazi ikiwemo
upungufu wa nguvu za kiume, kuharibika kwa mimba, kuzaliwa kwa watoto
wenye matatizo ya akili pamoja na kuenea kwa kansa mbalimbali kama vile
kansa ya koo, mapafu na mara nyingine husababisha vifo ghafla vya
kutokana na dozi kuwa kubwa “overdose”.
Aidha Serikali imeendelea kusimamia
utoaji tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya ili kupunguza madhara
yanayotokana na matumizi ya dawa hizo, na kufanikiwa kuongeza idadi ya
waathirika wa dawa za kulevya katika vituo vya tiba kutoka wagonjwa
2,400 mwaka 2015 hadi wagonjwa 7000 mwaka 2018. Hali hii imeasaidia
kupunguza maambukizi ya UKIMWI kwa waraibu wa dawa za kulevya
wanaojidunga kutoka 35% mwaka 2015 hadi 18.5%.
Pia, Serikali inamtaka kila mwananchi kwa
nafasi yake katika jamii kushirikiana na vyombo vya dola kutoa taarifa
endapo kutabainika kuwepo kwa matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
Pamoja na hilo Serikali inatoa wito kwa viongozi wa dini kulikemea suala
la matumizi ya dawa za kulevya misikitikini na makanisani. Sambamba na
hilo, Serikali inawakumbusha Viongozi wa dini zote kuwa wana nafasi
kubwa katika jamii ya kuhakikisha watoto, vijana pamoja na jamii yote
kwa ujumla wanapata mafunzo ya kuwajenga kiroho, kimwili na kisaikolojia
ili wawe na tabia njema katika jamii na mfano wa kuigwa kwa matendo
mema.
Serikali inaikumbusha jamii kushiriki
kikamilifu katika kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya,
kujenga malezi bora kwa watoto katika ngazi ya familia, na kuwapeleka
kwenye matibabu watumiaji wa dawa za kulevya. Vilevile, Serikali
inasisitiza Jamii kuzitambua, kuzienzi na kuziendeleza tamaduni zetu
nzuri ili kuinusuru Wananchi wote hasa vijana ambao ndo nguvu kazi ya
taifa na matumizi ya dawa za kulevya.
0 comments:
Post a Comment