Daktari
Bingwa wa Magonjwa ya Kina mama wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),
Dkt. Vicenti Tarimo akizungumza na waandishi wa habari juu ya uboreshaji
wa wodi zinazolaza wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU). Kushoto
ni Mkuu wa Idara ya Ukunga na Uzazi wa MNH, Bi. Mugara Mahungururo
akiwa kwenye mkutano leo.
Baadhi ya waandishi wa habari
wakimsikiliza Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kina mama wa MNH, Dkt.
Tarimo kuhusu uboreshaji wa miundimbinu inayotumika kutoa huduma kwa
wagonjwa.
Meneja
wa Jengo la Wazazi namba Moja wa MNH, Suzana Ndambala akitoa ufafanuzi
katika kuhusu huduma inayopatikana katika ICU ya kina mama wajawazito
(MAICU) ina vitanda 10.
………………
Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH) imeongeza idadi ya vitanda katika wodi za
wagonjwa wanaohitaji huduma za uangalizi maalum (ICU) kutoka 25 hadi 78
ikiwa ni sehemu ya mkakati wa hospitali wa kuboresha miundombinu ya
kutoa huduma kwa wagonjwa.
Daktari
Bingwa wa Magonjwa ya Kina mama wa MNH, Dkt. Vicenti Tarimo amesema
lengo la kuboresha miundombinu inayotumika kutoa huduma ni kupunguza
vifo vya kina mama wanaofariki dunia kutokana na kifafa cha mimba.
“Hospitali
imetengeneza chumba cha kina mama wanaohitaji huduma ya uangalizi
maalum (MAICU) chenye vitanda 10, pia imeweka mashine tano za kusaidia
kupumua na ultrasound. Hivi sasa, huduma hii inapatikana kwenye jengo
lao ukilinganisha na zamani ambapo mama alipaswa kupelekwa ICU ya
kawaida ambayo ipo umbali wa mita 150. Hali hii ya upatikanaji wa huduma
ilikuwa inahatarisha uhai wa mama na mtoto. Maisha ya kina mama wengi
yameokolewa kupitia MAICU,” amesema Dkt. Tarimo.
Dkt.
Tarimo amefafanua kwamba kuwapo kwa huduma ya MAICU kumesaidia
kupunguza vifo vya kina mama kutoka 125 mwaka 2017/2018 hadi kufikia
vifo 86 Julai 2018 hadi Juni 2019.
Amesema
uboreshaji wa huduma MNH ni sehemu ya kutekeleza malengo ya Serikali
pamoja na malengo ya milenia ya kupunguza vifo vya kina mama.
“Hatua
hii inaifanya MNH kuwa Hospitali ya kwanza ya umma hapa nchini kuwa na
ICU ya kina mama wajawazito wenye kuhitaji uangalizi maalumu,” amesema
Dkt. Tarimo.
Dkt.
Tarimo amebainisha pia MNH ina ICU ya watoto wachanga (NICU) yenye
vitanda 18, PICU ya watoto wenye umri wa kuanzia mwezi yenye vitanda 12,
wodi ya wagonjwa wa tiba (MICU) ambayo ina vitanda 15, wodi ya wagonjwa
wa upasuaji wanaohitaji uangalizi maalum (SICU) yenye vitanda 18, wodi
ya wagonjwa wanaopandikizwa figo wanaohitaji uangalizi maalum ambayo ina
vitanda 5 na ICU ya kina mama wajawazito (MAICU) ambayo ina vitanda 10.
“Shirika
la Afya Duniani (WHO) linazitaka Hospitali kuwa na asilimia 10 ya
vitanda vya ICU. MNH ina vitanda 1,550 hivyo inatakiwa kuwapo kwa
vitanda 155 vya ICU. Hivi sasa MNH ina vitanda 78 sawa na asilimia 50 ya
takwa la WHO. Hizi ni jitihada kubwa za uboreshaji huduma kwa
wananchi,” amesema.
Dkt.
Tarimo amesema kwamba uwapo wa miundombinu ya ICU, imesadia watalaam
kutoka hospitali nyingine nchini kuja kujifunza namna bora ya kuanzisha
na kuendesha vyumba vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum kwa
makundi mbalimbali.
“Baadhi
ya hospitali za rufaa za mikoa zimeanza kuleta watalaam wake kujifunza
jinsi ya kutoa huduma kwenye ICU. Vilevile huduma hizi zitasaidia katika
utafiti wa mahitaji halisi ya huduma za ICU pamoja na gharama zake na
hivyo kusaidia Wizara ya Afya na Serikali kwa ujumla katika kuweka
mipango ya upanuzi wa huduma hii hapa nchini,” amesema Dkt. Tarimo.
Katika hatua nyingine, Hospitali imefanya ukarabati mkubwa katika wodi 3 hadi 6 za Mwaisela na kuweka mfumo wa oxygen pamoja
na vitanda 7 kila wodi sawa na vitanda 28 vya kutoa huduma kwa wagonjwa
maalum (HDU). Uboreshaji huu utawasaidia wagonjwa wa kiharusi kuonwa
kitalaam zaidi na kuwa kwenye uangalizi wa karibu ikilinganishwa na
awali walikuwa wakilazwa katika wodi za kawaida.
0 comments:
Post a Comment