Mkurugenzi wa Idara ya
Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt.Hassan Abbasi akifafanua
jambo kwa Waandishi wa Habari ( hawapo pichani), kuhusu utekelezaji wa
Serikali kwenye sekta mbalimbali, katika Mkutano na Waandishi wa Habari
uliofanyika Jijini Dar es Salaam, leo Alhamisi 30. Mei. 2019.
Mkurugenzi wa Idara ya
Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt.Hassan Abbasi,
Akizungumza na Waandishi wa Habari, kuhusu utekelezaji wa Serikali
kwenye sekta mbalimbali, katika Mkutano na Waandishi wa Habari
uliofanyika Jijini Dar es Salaam, leo Alhamisi 30. Mei. 2019.
Mkurugenzi wa Idara ya
Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt.Hassan Abbasi,
akionyesha nakala ya Jarida la Nchi yetu lililochapisha habari za (Sekta
ya Madini) linalotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni, kwa Waandishi wa
Habari katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika Jijini Dar es
Salaam, leo Alhamisi 30. Mei. 2019.
(Picha na Paschal Dotto-MAELEZO).
………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu,- MAELEZO- DAR ES SALAAM
SERIKALI imesema maono na mtazamo
yakinifu wa Rais Dkt. John Magufuli katika usimamizi na ufuatiliaji wa
sekta ya madini, umewezesha ongezeko maradufu la makusanyo ya mapato ya
sekta hiyo kutoka Tsh Bilioni 210 mwaka 2015/16 hadi kufikia Tsh Bilioni
302 kwa mwaka 2018/19 na kuifanya Tanzania kuzidi kujijenga Kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa
vyombo vya habari leo Alhamisi (Mei 30, 2019) Jijini Dar es Salaam,
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali,
Dkt. Hassan Abbasi, alisema Serikali ya Awamu ya Tano inafanya kazi
kisayansi na itahakikisha rasilimali za nchi zinaendelea kulindwa ili
ziweze kuleta manufaa kwa Watanzania wote.
Dkt. Abbasi alisema mara baada ya
Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani Novemba 2015, ilifanya
mageuzi mbalmbali katika usimamizi na ufuatiliaji wa rasilimali za
madini, kwani huko nyuma Serikali ilikuwa ikipoteza kiasi kikubwa cha
fedha na kuamua kuchukua hatua stahiki ikiwemo kufanya mabadiliko katika
Sheria ya Madini ya mwaka 2010.
“Tulipofanya marekebisho katika
sheria yetu ya madini mwaka 2017, matokeo tumeanza kuyaona kwani
tumedhibiti mianya yote ya upotevu wa mapato yetu na kuanza kusimamia
kwa umakini mkubwa utoroshaji mkubwa wa madini ambapo ilisababisha
Serikali kupoteza kiasi kikubwa cha mapato” alisema Dkt. Abbasi.
Akitolea mfano Dkt. Abbasi
alisema kufuatia agizo la Rais Dkt. John Magufuli la kuanzishwa kwa
masoko ya madini ambayo ni utekelezaji wa sheria ya madini ya mwaka
2017, hadi sasa kuna jumla ya masoko 24 ambayo yamekuwa yakithibiti
ubora, thamani na takwimu za madini nchini, ambapo soko la kwanza
lilianzishwa Mkoani Geita, mwezi Machi mwaka huu.
Aidha Dkt. Abbasi alisema Takwimu
za jumla za uzalishaji wa dhahabu katika kipindi cha miezi miwili ,
mkoani Geita kuanzia mwezi Machi hadi Mei, mwaka huu zinaonyesha kuwa
uzalishaji umeongezeka kwa kiasi kikubwa na kufikia kilo 312.65 za
dhahabu ukilinganisha na uzalishaji wa dhahabu kilo 259.12 zilizokuwa
zikizalishwa kabla ya masoko hayo.
“Mwezi April, pekee uliweka
rekodi ya Geita kwa kuzalisha kilo 200 ambazo hazijapata kufikiwa mkoani
humo kwa wachimbaji wadogo na wa kati na kwa Takwimu za Mei mwezi mwaka
huu zinazidi kuthibitisha kuwa Watanzania wanapaswa kuendelea kumuombea
na kumuunga mkono Rais Magufuli” alisema Dkt Abbasi.
Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi alisema
eneo lingine la mageuzi yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano
katika sekta ya madini ni pamoja na maamuzi iliyochukua ya kujenga ukuta
kuzunguka eneo la wachimbaji wa Madini ya Tanzanite Mkoani Manyara
ambao Serikali iliweka mifumo ya masoko na ukaguzi, na hivyo kuchangia
ongezeko la mapato ya wachimbaji wadogo na Serikali kwa ujumla.
Akifafanua zaidi Dkt. Abbasi
alisema uzalishaji wa madini ya Tanzanite kutoka kwa wachimbaji wadogo
ulioripotiwa kwa mwaka 2016 ulikuwa kilo 164.6 na kilo 147 kwa mwaka
2017, ambapo Serikali iliweka kukusanya kiasi cha Tsh Milioni 71 (2016)
na Tsh Milioni 166 (2017), lakini uzalishaji huo uliongezeka maradufu
mara baada ya Serikali kujenga ukuta huo.
“Uzalishaji uliongeza sana mara
baada ya ujenzi wa ukuta kwani Kilo 781.2 zilizalishwa mwaka 2018 na
kuiingizia Serikali mapato ya Tsh Bilioni 1.43 na uzalishaji kwa mwaka
2019 katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Mei ulikuwa kilo 1086.05
zenye thamani ya Tsh Bilioni 1.422” alisema Dkt. Abbasi.
Aliongeza kuwa mabadiliko hayo
yameanza kuleta faida kwa nchi ambapo kwa sasa nchi nyingi za Afrika
zimeanza kuiga mageuzi yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ikiwemo
kupitia upya mikataba na wawekezaji na pia watafiti mbalimbali
wanairejea Tanzania inayogeuza “laana” ya madini kuwa “Baraka” ya
Madini.
0 comments:
Post a Comment