METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, December 13, 2020

WAZIRI MHAGAMA: KAMILISHENI USIMIKAJI WA MFUMO WA VIBALI VYA KAZI KWA WAKATI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (katikati) akizungumza na Wakuu wa Menejimenti ya Ofisi yake pamoja na taasisi zilizopo chini ya ofisi hiyo alipokutana nao Jijini Dodoma, Disemba 12, 2020. Kulia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi na Kushoto ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Nderiananga.

Sehemu ya wakuu wa Menejimenti kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizopo chini ya ofisi hiyo wakifuatilia kwa makini maelezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokutana nao katika ukumbi wa mikutano uliopo Ofisi ya Waziri Mkuu, Ngome Jijini Dodoma.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi akizungumza na Wakuu wa Menejimenti Ofisi ya Waziri Mkuu na Wakurugenzi wa Taasisi wakati wa kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (aliyekaa katikati). Kulia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Nderiananga.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewataka watendaji wa wizara yake kuhakikisha wanakamilisha mfumo wa vibali vya kazi kwa raia wa kigeni haraka ili kuondokana na changamoto zilizopo katika utoaji wa vibali hivyo.

Kauli hiyo ameitoa Jijini Dodoma Disemba 12, 2020 wakati alipokutana na Menejimenti ya wizara yake na taasisi zilizopo chini ya ofisi hiyo ambapo alieleza kuwa usimikaji wa mfumo wa kielektroniki wa kushughulikia vibali vya kazi itasaidia kuimarisha ushughulikiaji wa maombi ya vibali vya wageni.

“Idara ya Kazi kwa mujibu wa sheria inajukumu la kuratibu ajira za wageni nchini, hivyo kutokana na changamoto zilizopo katika utoaji wa vibali hivyo hivyo suluhisho pekee la kutoa vibali kwa wakati ni kuharakisha mfumo wa kielektroniki ambao utashughulikia vibali vya kazi,” alieleza Waziri Mhagama

Aliongeza kuwa, Mfumo huo wa kielektroniki ambao unaandaliwa utakuwa na manufaa ikiwemo kuongeza ufanisi katika kushughulikia maombi ya vibali vya kazi na kuokoa muda wa kushughulikia maombi ya vibali hivyo.

Aidha, Waziri Mhagama alisisitiza suala la uboreshaji wa sheria za kazi ili ziendane na mfumo huo unaoandaliwa.

“Hakikisheni mnafanya mapitio sheria za kazi kwa kushirikisha wadau ambao wanahusika katika uandaaji wa mfumo huo ili kuboresha utoaji wa huduma katika kushughulikia maombi ya vibali,” alisema Mhagama

Sambamba na hayo, Mheshimiwa Mhagama ameagiza kuwepo na utaratibu wa kushughulikia malalamiko mbalimbali yanayohusu vibali vya kazi ambayo yanatolewa na wadau.

Waziri Mhagama amekutana na Menejimenti ya ofisi yake pamoja na Taasisi zilizopo chini ya ofisi hiyo lengo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuwa anafungua Bunge la 12 na pia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi katika kipindi cha Miaka mitano (2020 – 2025).

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com