METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, December 12, 2020

CHINA NA TANZANIA KUIMARISHA ZAIDI USHIRIKIANO

Said Said Nguya, CCM

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally Kakurwa  amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China Nchini Tanzania Bi. Wang Ke. Mazungumzo hayo yamelenga katika kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo tarehe 12 Desemba, 2020 katika Ofisi za  Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma.

"China tumeongea na Katibu Mkuu wa CCM kuhusu malengo yetu ya kiuchumi ya muda mfupi na muda mrefu, na Katibu Mkuu ametueleza malengo ya maendeleo  ya Tanzania kwa mwaka 2021-2025 na 2021-2030, tumepata kufahamiana vema kila mmoja wetu na  sasa ushirikiano wetu utaimarika zaidi." Balozi Wang Ke

Balozi ameongeza zaidi kwa kusisitiza kuendeleza ushirikiano kati ya Chama Cha Kikomunisti cha watu wa China (CPC) na CCM, na China wanautazama ushirikiano wetu kama ni wenye manufaa makubwa kati ya mataifa haya mawili kwa siku za mbeleni.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu akifafanua kwa ufupi mazungumzo hayo, ameeleza kuwa, yamelenga agenda ya maendeleo katika nchi yetu na ushirikiano wetu wa kihistoria kati ya China na Tanzania na kati ya CPC na CCM, hasa ushirikiano katika sekta za uwekezaji, Afya na Elimu ya ufundi ili kukuza soko la ajira, kama Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 ilivyoahidi.

Aidha, Katibu Mkuu amepokea salama za pongezi  kutoka serikali ya China kwa ushindi mkubwa wa CCM na kwa kuendesha uchaguzi wetu kwa gharama za ndani, jambo ambalo ni geni kwa mataifa mengi ya Afrika.

Huu ni utaratibu wa viongozi wa Chama kuendelea kujenga  na kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na mataifa mengine yenye dhamira na nia njema kwa Nchi yetu.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com